Habari

Polisi Jamii yapigwa marufuku Mji Mkongwe

Na Mwandishi Wetu

Kuna habari kwamba Kikosi cha Polisi Jamii vijana wa ulinzi shirikishi wa Mji Mkongwe chenye makao makuu yao Malindi soko la samaki kimetimuliwa kwa amri ya kiongozi wa juu wa serikali ya Zanzibar.

Ingawa hatukuweza kuwapata waliokuwa wakiunda kikosi hicho kilichojizolea sifa kwa kurejesha nidhamu, usafi na huduma kwenye mji huo mkuu wa Zanzibar kwa kuwa sasa wameshambaratika, wakaazi wa Malindi wamemueleza mpasha habari wetu kwamba kikosi hicho hakipo tena.

Sababu kubwa iliyotajwa ya kufutwa kwa kikosi hicho kwa amri ya kiongozi wa juu serikalini ni tukio la tarehe 25 Agosti 2017, ambapo askari wa kikosi hicho cha kiraia waliingilia kati kile ambacho kinachoonekana kuwa zoezi la kuingiza biashara haramu kupitia bandari ya wavuvi ya Malindi.

“Siku hiyo mnamo majira ya saa 12 jioni, katika ofisi ya askari jamii kuna kuna geti linauzwa mkaa na limeandikwa mwisho wa huduma ni saa kumi na moja na nusu jioni ili kuepusha kupitishwa vitu visivyo halali kama bangi, unga, mirungi na hata silaha”, anasema mpasha habari wetu, ambaye hakutaka kutajwa jina.

Chanzo chetu kinatueleza kuwa kuna mtu ambaye anatambuliwa kuwa na asili ya Pembe ya Afrika na ambaye hata si raia wa Tanzania aliyefika hapo muda huo na kutaka kutoa polo la mkaa.

“Hapo ndipo sinema ilipoanzia kwa askari jamii hao kumzuwia asitoe polo hilo mpaka awepo askari polisi. Ndipo naye alipokataa na kuanza kukurupushana na vijana hao na vijana wakalieka polo hilo ndani lilipotokea,” anaeleza mpasha habari wetu.

Kilichoendelea ni kuwa raia huyo wa alimpigia simu kiongozi mmoja wa juu wa serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein akimwambia eti hawa polisi jamii wamemtukana kiongozi huyo na serikali kwa ujumla.

“Kiongozi alimuagiza kiongozi mwengine afuatilie na alipofuatilia huyo kiongozi mwengine alipiga simu kwa msimamizi wa polisi jamii na kumtaka raia huyo wa kigeni apewe polo lake na hapo polo likatoka kwa shingo upande bila ya kukaguliwa,” anaendelea mpashaji taarifa wetu akisema kuwa siku ya pili yake, raia huyo wa kigeni anayezungumza Kiswahili kwa tabu alikwenda kuwambia polisi jamii hao kuwa usiku wake wangelikiona.

“Na kweli, usiku walivamiwa na kikosi cha mazombi na kuwaeka chini wakitaka waseme alipo mkubwa wao. Hapo wakamteka mmoja wao na kwenda kuwaonesha anapokaa mkuu wao bila ya utaratibu wa kisheria na mazombi hao wakaingia ndani ya nyumba wakiwa na silaha kama mapanga, bunduki, visu na huku wakiwa wamelewa.”

Inaelezwa kuwa kwenye uvamizi huo walifanya upekuzi kwenye nyumba nzima lakini hawakumkuta waliyemhitaji, lakini walirejea siku ya pili, ingawa mara hii jeshi la polisi liliamua kutoa askari wa kwenda kumhami kwa siku tatu nzima.

“Lakini yule raia wa kigeni akawafuta tena polisi jamii hao na kuwaambia lazma kikundi akiuwe kisiwepo,” anaripoti mpasha habari wetu.

Mnamo tarehe 3 Oktoba, kikundi hicho kilisambatishwa na raia huyo wa kigeni anaripotiwa kutamba katika eneo zima la Malindi akipita na kufurahia huku akionyesha ishara ya matusi kwa mkono.

Kikundi cha polisi jamii cha Mji Mkongwe kilikuwa kikundi bora na cha kipekee kwa Tanzania nzima kiasi cha kupatiwa tuzo na aliyekuwa Mkuu wa Polisi wa Tanzania, IGP Said Mwema n ahata Rais Jakaya Kikwete kwa kukabidhiwa fedha taslim.

Miongoni mwa shughuli za kijamii kilichoshiriki ni kuokoa watu waliozama na meli zote mbili mwanzoni mwa utawala wa Dk. Ali Mohamed Shein na pia kuondoa makundi ya vijana waovu katika Mji Mkongwe na kurejesha hadhi ya mji na staha.

Katika mji ambao hata serikali ilikuwa imeshindwa kuuondoa uhalifu, ni kikosi hiki pia kilichomtafuta mtu aliyewachoma visu watalii watano katika mkahawa wa Luqman uliopo Mkunazini.

Kikundi hicho kilishiriki vyema katika kuokoa watu kwenye ajali za moto au kuungua nyumba pamoja na kwenda nje ya Zanzibar kunuokoa mtoto aliyeibiwa na kurudi naye.

Polisi Jamii Mji Mkongwe kilikuwa kikundi pekee chenye gari yao mali yao ambayo sasa serikali inataka ikabidhiwe gari hiyo.

Share:

3 comments

 1. abuu7 8 Oktoba, 2017 at 11:12

  dalili za uchafu waa kundi la wauwaji .liko ukingoni.CCM. mlitumiya mauwaji ya 64 kutoka mijitu yabara sasa mnafikiri. wakati ule ndio huu. hata mfanye nini wazawa wanakupigiyeni duwa kila siku.mtamalizika wenyewe.

  cha muhimu kila jirani sasa nikulinda mwenzake.weka simu karibu

 2. shawnjr24 9 Oktoba, 2017 at 01:27

  Mwandishi pia unatakiwa utaje na mabaya yao hawa wahuni niliwaona kwa macho yangu wakiwapiga. Watoto wa kike mikwaju kisa walipita pale Jamhuri garden wakiwaambia kama njia imefungwa. Mimi nilipark gari mmoja wao akanifata nimpe buku jero wala sikujua ndio nini hio buku jero mpaka mwenyeji wangu kunifahamisha.

 3. Papax 9 Oktoba, 2017 at 13:32

  Mimi ni mmoja kati ya wafanyajikazi maeneo ya malindi naijua, vizuri malindi kuazia funguni ,rasrema, mabanda ya papa, na kwengineko, kabla ya kuja hawa polisi, jamii, malindi ilikuwa ina tisha, laki tujiulizeni, huyu, mzee wa kisomali, mnaye mtuhumu, wao wana mjua fika, kwanini, wamzuile, kipolo, cha mkaa haliyakuwa wana mjua kuwa ni mzee wa mtaani, wasitafute, mchawi, wao walifuturu, ada, kwahio, tulio wafukuza ni sisi wazawa, sio, msomali kama mnavyodai, tunaju kuwa wengi kati ya hapolisi jami wao wenyewe wanavuta unga na bangi,wa nafanya kila aina ya uonevu, walikuwa wanajiona kama askarikweli

Leave a reply