Habari

Polisi Wang’ang’ania ‘Computer’ Ya Mansour

Na Mwinyi Sadalla – Mwananchi

Posted Jumatano Agosti 13, 2014

JESHI LA POLISI Zanzibar, linaendelea kuishikilia ‘laptop’ ya waziri wa zamani wa Zanzibar Mansour Yussuf Himid aliyekamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kupatikana na bunduki na risasi 407 kinyume cha sheria.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi alisema laptop hiyo iko mikononi mwa polisi, tangu ilipokamatwa Agosti 2, mwaka huu.

Msangi alisema polisi inaendelea kuifanyia upekuzi ili kujua yaliyomo ndani yake na imehifadhi vitu vya aina gani na iwapo hakutakuwa na vitu vya kuvunja sheria itarejeshwa kwa mhusika.

Alisema endapo watabaini kuwapo kwa vitu vyovyote vya kuvunja sheria itatumika kama kielelezo na kwamba kazi ya kuipekua inaendelea:

“Ni kweli laptop tunaendelea kuifanyia uchunguzi bado ni mapema kuwaeleza nini tumekiona na hakuna sababu ya kueleza hivi sasa kwa kuwa kazi hiyo bado haijakamilika,” alisema Msangi.

Hata hivyo, alisema hatua za awali za uchunguzi zimeonyesha kuna mambo alikuwa akiyatuma kwenye mitandao ya kijamii na kushiriki hatua mbalimbali za mijadala inayohusu siasa na maendeleo ya jamii.

Alisema siyo kosa mtu kushiriki na kutoa maoni katika mitandao ya kijamii lakini kuna mambo zaidi ya hapo yanahitaji kuchunguzwa.

Mbali na hilo, Polisi walifanya upekuzi katika nyumba nyingine ya waziri huyo wa zamani iliyopo katika Kijiji cha Kiboje, kilomita 12 kutoka mji Zanzibar.

MANSOUR KUPATA DHAMANA JUMATATU (kutoka Mzalendo.net)

Wakati huo huo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Abraham Mwampashi amesema kwamba Mahakama hiyo haina pingamizi ya kutoa dhamana kwa Mansour Yussuf Himid ambaye ameshtakiwa kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume cha sheria za nchi.

Baada ya kusikiliza hoja za kisheria kutoka pande zote mbili za mawakili wa Serikali na Utetezi, Jaji Mwampashi amesema: “Mahakama Kuu haina pingamizi na ombi la dhamana kwa Mansour kwa sababu limezingatia vigezo vyote vya kisheria,”.

Jaji Mwampashi alisema hayo jana wakati alipokuwa akisikiliza ombi la dhamana lililowasilishwa kwenye Mahakama hiyo na Mawakili wanaomtetea Mansour. Mshtakiwa huyo amerudishwa rumande.

Adha, Jaji huyo amesema ombi la dhamana hiyo litatolewa uamuzi siku ya Jumatatu, Agosti 18, mwaka huu siku ambayo pia, inatarajiwa kuanza kusikilizwa kwa kesi ya msingi ya mshtakiwa huyo.

Mansour ambaye alikuwa katika madaraka ya Serikali ya Zanzibar ya awamu ya sita na ya saba, alikamatwa na kuwekwa rumande mapema mwezi huu.

MKUTANO WA CUF KIBANDAMAITI (mzalendo.Net – Video)

Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad alisema Jumapili iliyopita kwenye mkutano wa hadhara wa Kibandamaiti, Unguja kwamba kadhia iliyomkuta Mansour, ni ishara njema:

“Njia zile zile walizompitisha Maalim Seif…Maalim Seif kwanza alifukuzwa Chama hicho hicho cha Mapinduzi…wakamtafutia shtaka halina dhamana wakamuweka jela kwa muda watakao wenyewe…ulipofika muda…wenyewe wakasema toka,” alisema Maalim Seif.

Alisema: “Tumeanzisha CUF mkutano wa kwanza tumeufanya Malindi…mimi nipo kama Makamu Mwenyekiti lakini ndiyo nimeshonwa mdomo…nikaja kwenye jukwa nikatoa mkono tu hivi basi imetosha.”

Alisema: “Wakenda wenyewe mwisho wakasema sasa kesi tunaifuta…sasa Maalim Seif yule yule ni Makamu wa Rais wa Zanzibar.”

Alisema: “Nakumbuka kulikuwa na askari wakinipeleka jela walivyokuwa wakinitukana na kuninyanyasa mie kimya mmh…mmh. Mungu si Athman wala si Mfaki…mmoja yuko Dar es Salaam sasa hivi akiniona mmnhh.”

“Kwa hivyo nasema la Mansour ni ishara njema…Hatujui huko mbele Mwenyezi Mungu kamuandikia nini…lakini najuwa kamuandikia mambo mema tu Inshaallah,” alisema na kuongeza:

“Lakini papo hapo niseme…nataka niamini kwamba Mansour hakukamatwa kwa sababu yeye si mwanachama tena wa Chama cha Mapinduzi…Nataka niamini kwamba Mansour kakamatwa kwa sababu katoka hadharani kuunga mkono Mamlaka Kamili kwa Zanzibar.”

Alisema: “Nataka niamini kwamba Mansour hakukamatwa kwa sababu kasema wazi wazi atamuunga mkono Maalim Seif mwakani katika kupigania uchaguzi.”

“Nataka niamini kwamba Mansour hakukamatwa kwa sababu kasema atagombea Jimbo la Kiembe Samaki kwa tiketi ya CUF…Nataka niamini hizo sizo sababu ambazo zilizomfanya Mansour akamatwe,” alisema Maalim Seif.

Alisema: “Nataka niamini kwamba Mansour atatendewa haki kama raia yeyote yule mwingine katika nchi hii na kwamba yale mashtaka yote yanayomkabili…lakini sheria itachukuwa mkondo wake pasipo na shinikizo za kisiasa.”

Alisema: “Mimi ilikuwa kesi yangu inaamuliwa kama kesho kwenda mahakamani kwanza watu wanakutana katika Ofisi ya Waziri Kiongozi pamoja na Hakimu aliyohusika kuzungumzia kesho tutafanya nini kwa maalim Seif…sasa nataka niamiani hayo hayatatendeka kwa Mansour.”

Maalim Seif ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema Mahakama iliyohuru itaweza kabisa kabisa kusikiliza shtaka lililoko mbele yake na kuamua kwa mujibu wa sheria za Zanzibar.

Alisema: “Kwa sababu sasa hivi siyo tena mwaka 64…sasa hivi siyo tena 74 sasa hivi siyo tena 84 sasa hivi tunapiga makelele sote viongozi kwamba tunataka utawala wa sheria…hatutaki utawala kwamba Maalim Seif ni Makamu wa Kwanza wa Rais…basi aseme mkamate huyo akakamatwa tutoke huko.”

Alisema: “Huyu huyu Mheshimiwa Mansour…si wakimpigia suluti si alikuwa ni waziri si alokuwa karibu yao mwenzao sasa kama watu wamekula njama ‘wajue na wa-wajue-na-wajuee’ kwamba Mwenyezi Mungu anahukumu dunia hapa hapa akhera inakwenda hesabau…kwa hivyo yaliyomfika Mansour yanaweza kumfika mtu yeyote.”

Alisema: “Kama kuna watu mimi sijui wamekula njama kwamba Mansour akae ndani basi nasema wakati mwingine ukilitandika godoro ukalitia miba ili mwenzako aje alale basi iko siku godoro lile utalilalia wewe,”..

Share: