Habari

Prof. Rai aiomba Iran kuiunga mkono SUZA

February 12, 2018

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) Prof. Idris Rai, ameiomba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuendelea kuiunga mkono Zanzibar hasa katika masuala ya elimu na utamaduni.

Akifungua mkutano kuhusu uhusiano wa utamaduni na lugha baina ya Zanzibar na Iran uliofanyika kampasi ya Vuga, Prof. Rai alisema kuna maeneo mengi yanayofanana kati ya Zanzibar na Iran hasa suala la utamaduni, hivyo kuna haja ya kufanywa utafiti wa pamoja ili matokeo yatakayopatikana yasaidie pande zote mbili.

“SUZA tunataka kuandika vitabu vya Kiswahili na kufanya utafiti katika eno hilo, tunahitaji kuungwa mkono na wenzetu wa Iran ili kazi hii ilete matokeo mazuri katika kustawisha utamaduni wetu,” alisema.

Alisema SUZA inahitaji ushirikiano wa karibu kutoka Iran ikiwemo kujengewa uwezo wafanyakazi wake hasa katika suala la elimu na ujuzi.

Mapema Prof. Abdulaziz Lodhi, alisema bado wasomi wa Zanzibar hawajafanya utafiti kuhusu asili ya Wazanzibari hali ambayo inasababisha wananchi kujiita Wazanzibari wakati wao ni Wafarsi kutoka Iran.

“Binaadamu asiejua msingi wa asili yake ni sawa na mnyama, kuna haja ya kufanya tafiti za kina kujua wapi tulikotoka, wapi tulipo na wapi tunakokwenda,” alisema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Tanzania, Ali Bagheri, alisema Iran itaendelea kuimarisha uhusiano na Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo utamaduni, kwa sababu utamaduni wa pande hizo una historia moja.

Mkutano huo uliandaliwa kwa pamoja baina ya skuli ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ya SUZA na ubalozi wa Iran nchini na kuwahusisha wataalamu wa masuala ya utamaduni na Kiswahili pamoja na wanafunzi.

Zanzibar leo

Share: