Habari

Rais Dk Shein afanya uteuzi wa viongozi taasisi za Serikali

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 29.09.2018

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo amefanya uteuzi wa viongozi katika Taasisi mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, Rais Dk. Shein amemteua Dk. Abdulla Mohamed Juma kuwa Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii ambaye anachukua nafasi ya Dk. Vuai Idd Lila ambaye atapangiwa kazi nyengine.

Katika uteuzi huo pia, Rais Dk. Shein amemteua Khalfan Sheikh Saleh kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Serikali wa Uchapaji na Mpigachapa Mkuu wa Serikali, ambaye anachukua nafasi ya Mohamed Suleiman Khatib ambaye atapangiwa kazi nyengine.

Aidha, Rais Dk. Shein amemteua Said Juma Ahmada kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Mjini Unguja, Mkurugenzi huyo wa Manipaa ya Mjini Unguja anachukua nafasi ya Aboud Hassan Serenge ambaye anastaafu kwa mujibu wa Sheria.

Pia, Rais Dk. Shein amemteua Amour Ali Mussa kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Magharibi “A”, Amour Ali Mussa anachukua nafasi ya Said Juma Ahmada ambaye amehamishiwa Manispaa ya Mjini.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein amemteua Ali Abdulla Said Natepe kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Magharibi “B”, Ali Abdulla Said Natepe anachukua nafasi ya Amour Ali Mussa ambaye amehamishiwa Manispaa ya Magharibi “A”. Uteuzi huo unaanza tarehe 1 Oktoba, 2018.

Zanzinews

Share: