Habari

RAIS KIKWETE NA SHEIN YATAFAKARINI YA BURUNDI

Wahenga walinena ya kwamba ukiona mwenzako ananyolewa basi na wewe tia maji. Lakini pia Wahenga hawa hawa hawakuishia hapo walienda mbele zaidi na kunena kwamba mkataa ya Mussa (moses) basi hupata ya Mjomba Firaun .

Kinachoendelea hivi sasa Burundi ni mwendelezo wa Viongozi wa Afrika ambao hujitoa fahamu na kuipindisha demokrasia ya kweli kwa Wananchi wao. Viongozi hawa hujidanganya au kudanganywa na baadhi ya Wahafidhina walio karibu nao eti wao ndio wanaomiliki hati miliki ya kuongoza Nchi na sivyenginevyo.

Ni vyema kwa Marais wetu wote wawili kuyaelewa haya kwamba ujanja wa kutawala kwa kutumia nguvu,ghilba,jeuri,udanganyifu,uonevu pamoja na kupindisha haki kwa kutumia vyombo vya Dola ni mambo yaliopitiwa na wakati katika karne hii tulio nayo.

C.C.M na Serikali zake hazina budi kuyaelewa haya. Nasema hivi ni kiwa na hisia ya kwamba hali inavyokwenda hasa kwa Upande wa Zanzibar tunaelekea kubaya. Dalili zote zinaonesha ya kuwa Wananchi walio wengi wameshachoka na uonevu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar.

Inasikitisha kuona leo hii Zanzibar,Mzanzibar ananyimwa hata haki zake za msingi kama vile kupata kitambulisho cha kupigia kura na kuchagua kile chama anachotaka kwa mujibu wa katiba ya Nchi.Udanganyifu unaofanywa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Kwa kushirikiana na makada wa Chama cha Mapinduzi kitaipeleka Zanzibar na Watu wake pahala pabaya.

Nimalizie kwa kusema kwamba ni bora kutafuta kinga ya maradhi kuliko kuhangaikiwa dawa huku mgonjwa akiwa kitandani.Wahafidhina wataipeleka NCHI YETU pabaya. Muungwana husoma nyakati pamoja na matokeo yanayotokea.Jee sisi tunaelekea wapi ? Jee wale masheikh wa uamsho ambao ni Wananchi wenu vile munavyowatendea ndio haki yao ya kimsingi. Urais una mwisho wake lakini pia hata sisi Binaadamu hapa tunapita njia tu,kwa mola wetu tutarejea,tujiandae na ya kujibu.

Inashangaza kuona kiongozi wa NCHI anatesa Raia wake na huku anajisifia.Ya Burundi naomba yawe ni mafunzo kwetu.

Share: