Habari

Rais na Serikali wanaitetea CCM, badala ya Watanzania

10433107_10203120011545080_1166280403585172565_n

Jumatano,Novemba12 2014

Viongozi wamepoteza maana ya uongozi hata kama wanaapa mbele ya umma. Na wakati huohuo CCM inatumia kauli nzuri kuwasadikisha wananchi kama vile, ‘Tanzania bila CCM haiwezekani”, kumbe ukweli ni kuwa inawezekana na itapendeza sana.

Wakati Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ilipokabidhiwa madaraka, iliapa kuilinda Katiba, kuongoza nchi kidemokrasia na kuwa na utawala bora.

Pia, Serikali hiyo iliapa mbele ya umma kwamba italinda raia wake na mali zao pamoja na kuwatetea kwa kila namna.

Hata hivyo, leo hii CCM inaonekana imepoteza mwelekeo. ‘Imekula mwereka’ kama alivyosema katibu wa kwanza wa CCM, marehemu Horace Kolimba kabla ya kifo chake.

Kauli hii imeendelea kupuuzwa na karibu wana-CCM wote, ingawaje inaonekana kukitafuna chama hicho siku hata siku.

Rais na Serikali yake wanadhihirisha kukitetea chama chao kwa nguvu zote, akili zote na uwezo wote na kwa gharama yoyote kuliko kuwatetea wananchi maskini wa Tanzania. Jambo hili linasikitisha sana.

Watanzania wamebakia kama kondoo bila mchungaji isipokuwa wale walio karibu na vigogo na wenye madarakani serikalini na katika taasisi.

Hii imetokana na kupuuza na kuachana na misingi iliyojengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Wananchi ndiyo walikuwa walengwa wa chama hiki cha mapinduzi na alama pekee mwalimu Nyerere aliyopendekeza ilikuwa ni ‘jembe na nyundo’.

Alama hizi ziliashiria kuwa Tanzania ni Taifa la ‘wakulima na wafanyakazi’ chini ya sera ya ‘ujamaa na kujitegemaa’ ikisaidiwa na ‘Azimio la Arusha’ ambalo lilikufa mwaka l992 kule Zanzibar na likaletwa ‘Azimio la Rushwa na Ufisadi.’

Sasa ingependeza kama vingetafutwa viashiria vya ‘Azimio la Rushwa na Ufisadi’ halafu viwe ndiyo alama muhimu za taifa letu katika nyakati hizi za rushwa na ufisadi.

Matukio makubwa ambayo Serikali ya CCM inakabiliwa nayo kwa sasa ni uchakachuaji wa mchakato wa Katiba Mpya, kejeli na kashfa za Samuel Sitta kwa maaskofu, utata wa fedha kwenye akaunti ya Tegeta Escrow na wa kura za kupitisha Katiba Inayopendekezwa.

Lakini bomu kubwa ni tuhuma za biashara haramu na usafirishaji wa meno ya tembo kwa kutumia ndege ya Rais wa China wakati alipozuru nchini miezi 18 iliyopita. Hapo kwa kweli Serikali imevuliwa nguo wala hili si suala la kufanyia kejeli na utani.

Yaani tembo 142,000 badala ya kuongezeka zaidi wamepungua hadi kufikia 55,000 hivi hapo unaelezaje? Pamoja na juhudi zote za Waziri wa Mambo ya Nje, Membe kujitahidi kukanusha kuwa hizo ni habari za kupikwa, lakini wahenga husema ‘panapofuka moshi pana moto’.
Rasilimali hizi zingesaidia kuboresha maisha ya kila Mtanzania, kama alivyosema Rais Jakaya Kikwete wakati anaingia madarakani mwaka 2005, katika sekta ya elimu, afya na miundombinu kwa mfano.

Utetezi wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ni masuala ya propaganda za kisiasa. Kusema kwamba Marekani ina wivu na China kwa Tanzania haitoshi kabisa kuhalalisha kwamba ni habari za kupikwa. Wananchi ni lazima ifike mahali wajue kwamba sasa Serikali ya CCM haina muda wala mpango wa kuwatetea bali ina kazi moja tu kukitetea chama chao ili kiweze kuendelea kushika madaraka hata kama hayawasaidii wananchi.

Viongozi wamepoteza maana ya uongozi hata kama wanaapa mbele ya umma. Na wakati huohuo CCM inatumia kauli nzuri kuwasadikisha wananchi kama vile, ‘Tanzania bila CCM haiwezekani”, kumbe ukweli ni kuwa inawezekana na itapendeza sana.

Watanzania lazima wajue kwamba sasa muda wa mabadiliko umefika na ni uwendawazimu kuendelea kukishabikia chama tawala ambacho hakiwajali wananchi wake.

Sasa ni muda mwafaka kuungana bila kujali itikadi za kisiasa, dini, kabila, ukanda na kuleta mabadalikio yanayohitajika. Ni vyema mkatambua kuwa ‘ushindi umo mikononi mwa wananchi wenyewe.

Serikali ya CCM imejidhihirisha haina pesa ya kukabiliana na majanga kama ya ujangili wa kuuawa kwa tembo mamia kwa mamia.

Haina uwezo wa kukabiliana na wizi wa pesa za umma kama Epa, Escrow na kadhalika. Bali inazo fedha nyingi za kukabiliana na vyama pinzani vya kisiasa na wakosoaji wa Serikali yake kwa nguvu zote.

Serikali hii ina fedha za kugharimia mbinu na fitina na vurugu za michakato ya chaguzi mbalimbali. Serikali ina uwezo wa kugharimia magari ya maji ya kuwasha wakati wa uchaguzi au kuzima maandamano ya wapinzani au kikundi chochote kinachodai haki zake kwa kisingizio cha ‘kulinda amani na utulivu’.

Inasahau kuwa amani na utulivu havilindwi kwa mtutu wa bunduki bali kwa mioyo yenye utu na heshima kwa maisha.

Serikali hii hii ina uwezo na pesa za kugharimia mchakato ‘hewa’ wa Katiba Mpya ulioweka nyuma masilahi ya wananchi.

Kwa kifupi, Serikali inao uwezo, nguvu na pesa za kugharamia mipango mingi ya gharama kubwa ili kuua demokrasia nchini Tanzania.

Mfano kuwahusisha polisi katika mambo ya kisiasa hasa kampeni za uchaguzi kwa kutumia gharama kubwa sana inayovuruga amani ya nchi.
Nimalize kwa kusema sasa Watanzania kupitia hili ‘vuguvugu la mabadiliko’ na ujenzi wa ‘Tanzania Tuipendayo’ kila mwananchi amuamshe mwenzake aliyelala. Tazama, takafakari na chukua uamuzi kupitia sanduku la kura, Serikali za mitaa, kura ya maoni ya Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu 2015. Tafakari usemi wa Mwalimu Nyerere “Wakati ni huu.” Nimalize kwa kusema, mabadiliko yaanze na wewe…kifikra.

(kiakili) halafu vitendo.”

MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA,CCM OYEE
Chanzo Mwananchi

Share: