Habari

Rasimu ya Warioba ‘yachanwachanwa’

Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano ya Bunge la Katiba, Hamad Rashid akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana. Kulia ni makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Assumpta Mshana. Picha na Emmanuel Herman
Na Neville Meena na Sharon Sauwa, Mwananchi

Jumatano,Agosti20 2014 saa 9:2 AM

• Kamati nyingi zatupilia mbali mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba

• Baadhi ya wajumbe wa CCM wakerwa, wahoji Katiba ya serikali mbili iliyoboreshwa

Dodoma. Kuna kila dalili kwamba mabadiliko mengi yaliyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba yakigusa miundo ya taasisi nyeti za umma yatawekwa kando na huenda Bunge Maalumu likatoa Katiba isiyokuwa na mabadiliko makubwa kama ilivyotarajiwa.

Gazeti hili limebaini kuwa kamati nyingi za Bunge hilo zimebadili mapendekezo mengi hasa yanayowagusa viongozi na taasisi nyeti kama Bunge, tofauti na ilivyopendekezwa katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba.

Miongoni mwa mambo ambayo yamependekezwa kurejeshwa kama yalivyokuwa ni muundo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo kwa mujibu taarifa kutoka kwenye kamati mbalimbali, ni kuendelea na muundo wa sasa unaowajumuisha wabunge kutoka Zanzibar.

Katika maelezo yake, Jaji Warioba alisema moja ya kero za muungano katika eneo la Bunge ni malalamiko kwamba wabunge kutoka Zanzibar wamekuwa wakishiriki katika Bunge la Muungano na kushiriki kujadili mambo yanayohusu Tanzania Bara.

Kupitia mfumo wa Serikali tatu, Rasimu ilikuwa na mapendekezo ya kuwapo kwa Bunge la Muungano lenye wabunge 75, lakini mapendekezo hayo pia yamefutwa katika kamati karibu zote na kurejesha mfumo wa sasa pamoja na uwapo wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Mwenyekiti wa Kamati Namba Tano, Hamad Rashid Mohamed alisema jana kuwa suala la muundo wa Bunge lilisababisha mvutano mkubwa katika kamati yake na baadhi ya wajumbe walikuwa wakihoji uwakilishi mkubwa wa wabunge wa Zanzibar katika Bunge la Muungano hata kwa mambo ya Tanzania Bara.

Hata hivyo, alitetea hali hiyo akisema uwapo wa wabunge kutoka Zanzibar ni moja ya masharti yaliyowekwa na Katiba. “Hata Katiba ya sasa imeweka sharti la idadi ya wabunge wa Zanzibar, hilo nalo ni sharti la Katiba huwezi kuliondoa, kama unataka kuliondoa unapotunga Katiba maana yake ni lazima uvunje muungano.”

Alisema mwaka 1964 mambo yote ya Tanganyika yaliingizwa kwenye Serikali ya Muungano… “Kwa hiyo ni lazima ukafumue Muungano, useme haya ni ya Tanganyika na haya ni ya Muungano,” alisema.

Hamad alisema katika hadidu ya rejea, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikatazwa kugusa mambo ya Muungano. “Hivi wabunge 70 wanaokuja kutoka Zanzibar wakazungumzia mambo ya Bara, hivi kuna dhambi gani, sioni kosa kabisa.” Mwenyekiti huyo alisema kamati yake imebaini kwamba Rasimu ya Warioba ina upungufu mwingi kwani hata baadhi ya kero zilizotajwa zilishafanyiwa kazi na Serikali.

Hoja ya ushiriki wa Wazanzibari katika masuala ya Tanzania Bara iliripotiwa kuibuka katika Kamati Namba Moja ambako mmoja wa wajumbe, Ally Keissy alinikuliwa akihoji sababu za wajumbe wa Zanzibar kushiriki mambo ambayo wao siyo sehemu yake.
Mbali na muundo wa Bunge, kamati nyingi pia zimefuta mapendekezo kadhaa yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo ni pamoja na wabunge kutokuwa mawaziri, ukomo wa ubunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano mitano, wabunge kuwajibishwa na wananchi, kupunguzwa kwa madaraka na kinga ya rais.

Katika Kamati Namba Tano, Hamad alisema suala la wananchi kumuondoa mbunge lilikataliwa. “Hivi ni kigezo gani ambacho kinaonyesha mbunge hakuweza kuwaletea wananchi maendeleo. Nini utatumia cha kupima ufanisi wa huyu mbunge?”

Alisema kuliweka jambo hilo katika Katiba ni kuleta matatizo na kwamba wameliacha suala hilo mikononi mwa vyama vya siasa kuangalia kama mbunge anafanya kazi ya ilani zao au la.

Mgawanyiko mpya

Habari zaidi zinasema kuwekwa kando kwa mapendekezo mengi yaliyolenga kurekebisha mifumo ya uongozi na utawala, kumesababisha mgawanyiko hasa miongoni mwa wajumbe watetezi wa muungano wa serikali mbili, ambao awali, waliahidiwa kwamba muundo huo usingekuwa na sura yake ya sasa, bali ungeboreshwa.

Mmoja wa wabunge wa CCM alisema jana kwamba: “Tutawapa wapinzani sifa maana umma utaamini kwamba bila wao hakuna kinachoweza kubadilika, sasa kama tunarejesha kila kitu ambacho kiko kwenye Katiba tuliyonayo kuna maana gani ya kuwa na mchakato?”

Mmoja wa wenyeviti wa kamati za Bunge Maalumu naye alisema kinachoendelea ndani ya kamati nyingi ni kufuta mapendekezo ya Rasimu na kuleta mapendekezo mapya ambayo ni sawa na yaliyomo kwenye Katiba ya sasa.

“Ndani ya chama (CCM) tuliamua kupinga mapendekezo ya serikali tatu baada ya kuahidiwa kwamba tutakuja na muundo wa serikali mbili zilizoboreshwa, lakini hata hizo hatuzioni. Kwa hiyo wananchi wataamini kwamba kilichosemwa na Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), ni cha kweli,” alisema mwenyekiti huyo.

Utata wa akidi

Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis Michael aliamua kuahirisha kikao jana saa tano asubuhi kutokana na kile alichokiita kuwa ni kuwapa muda wajumbe waende kusoma zaidi sura ya tisa ambayo inahusu muundo wa Bunge.

Hata hivyo, habari ambazo zilikuwa zimelifikia gazeti hili mapema zinasema kuahirishwa kwa kikao hicho kulitokana na akidi kutotimia, taarifa ambazo Dk Michael alizikanusha kwa kuonyesha idadi ya wajumbe ambao walikuwa wamesaini karatasi ya mahudhurio.

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo alikiri kwamba hadi ilipotimu saa 4:00 asubuhi jana kamati yake ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa wajumbe wanne, hivyo waliwapigia simu na kubaini kwamba walikuwa katika shughuli nyingine ikiwamo kumpokea Rais Jakaya Kikwete.

“Baadhi ya wajumbe ni mawaziri kwa hiyo baada ya kukamilisha majukumu yao walifika na saa tano hivi akidi ilikuwa imetimia,” alisema Dk Michael.

Chanzo Mwananchi

Share: