Habari

RAZA AAPISHWA KUWA MWAKILISHI NA KUJILABU

Na Muhibu Said

Mwakilishi wa Jimbo la Uzini (CCM), Mohamedraza Raza, amesema msimamo aliona kwa miaka 20 iliyopita wa kutaka wananchi wa Tanganyika na Zanzibari, waheshimiane, kuvumiliana na kujadiliana katika Muungano, bado uko palepale, kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yule wa Zanzibar kila mmoja anaongoza nchi kamili na wote wako sawasawa kihadhi.

Raza alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Unguja jana, baada ya kuapishwa kuwa Mwakilishi wa jimbo hilo.

Alisema mshahara wa Sh. milioni nne atakaokuwa akilipwa kwa kazi yake ya Uwakilishi pamoja na mafao yake yote ya Sh. milioni 64 atakayolipwa baada ya kumaliza kazi hiyo, atayaelekeza katika kusaidia miradi ya maendeleo ya wananchi jimboni mwake ikiwa ni sehemu ya wajibu alionao hivi sasa wa kuhakikisha anatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama alivyoahidi wakati wa kampeni za kuomba kura.

Hata hivyo, alisema anaamini azma yake ya kutekeleza mambo hayo itafanikiwa tu iwapo atapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi jimboni kama walivyoonyesha imani kwake ya kumchagua kuwa mwakilishi wao katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Alisema katika kuonyesha kwamba ana dhamira ya dhati juu ya kuwatumikia, kuanzia sasa amejiwekea utaratibu wa kuwa anatangaza mshahara wake wa kazi ya Uwakilishi kila atakapokuwa akiupata na namna utakavotumika kugharimia miradi ya maendeleo jimboni.

Alisema aliwahi kuahidi kwamba, ndani ya miezi minne angekijenga kisasa Kituo cha Afya cha Umbuji kilichopo jimboni humo, lakini wakati akijiandaa kutimiza ahadi hiyo, Machi 14, mwaka huu, Wizara ya Afya ikamuandikia barua kumzuia kufanya hivyo kwa maelezo kwamba, imeshatiliana saini mkataba na Shirika la Orio wa ujenzi wa kituo hicho.

Alisema tayari amekwishachangia Sh. milioni 20 kwa Idara ya Barabara Zanzibar kwa ajili ya ujenzi wa barabara za ndani za Pagali-Umbuji; Ndagaa-Dongongwe; Kwa Kibawa-Matora na Dongongwe-Mkuku zilizokaguliwa katika jimbo la Uzini.

Pia alisema aliwasiliana na Idara ya Maji kujua tatizo la maji katika Jimbo lote la Uzini na kuelezwa kwamba zinahitajika Sh. 12.9 kwa ajili ya kunnua vifaa vitakavyosaidia kumaliza tatizo hilo na kuwa tayari amekwishaagiza vifaa hivyo kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa huduma ya maji katika jimbo lote la Uzini.

Alisema kamwe hatakubali kuteuliwa kuwa waziri au naibu waziri serikalini, badala yake akasisitiza kwamba anataka kuhakikisha anatekeleza ilani ya CCM..

Share: