Habari

RC: Majaji, mahakimu hukumuni kwa haki

February 11, 2018

NA HAJI NASSOR, PEMBA

MAJAJI na mahakimu nchini, wametakiwa kutoa uamuzi sahihi mahakamani, wenye kufuata misingi, kanuni na taratibu za sheria kama zilivyo na sio kumuonea mtu kwa sababu wanazozijua wao.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Hemed Suleiman Abdalla katika uwanja wa michezo Gombani Chakechake, alipokuwa akizungumza wanasheria na waendesha mashitaka, mara baada ya kumaliza matembezi, ikiwa ni shamrashamra ya kuelekea siku ya sheria Zanzibar.

Alisema majaji na mahakimu wamekuwa wakikumbana na kesi za aina mbalimbali na nyengine zikiwa na mvuto wa aina yake ndani ya jamii, hivyo lazima wakumbuke sheria na misingi yao ya kazi ilivyo.

Alisema suala la kutoa uamuzi mahakamani sio jambo jepesi, hivyo lazima wawe makini ili kujiepusha kuingia katika mgogoro na kundi moja la watu, kutokana na kufanyakazi kwa maslahi yao.

“Niwaombe sana majaji na mahakimu wetu wawe makini wanaposikiliza na kutoa uamuzi mahakamani, maana wapo wanaopindisha sheria na kufanya wapendavyo wakati wanaposikiliza na kutoa hukumu mahakamani”,alisisitiza.

Katika hatua nyengine mkuu huyo wa Mkoa, alisema lazima mkazo wa kutosha uwekwe kwa majaji na mahakimu hao, ili kusiwe na ucheleweshaji wa kesi na hasa za udhalilishaji.

Mapema mrajisi wa mahakam kuu Pemba, Hussein Makame Hussein, alisema mwaka mpya wa mahakama, utawapa nguvu na ari ya kufanya kazi vizuri.

Alisema wanasheria wote walioko mahakamani, walikuwa na mapunziko marefu ya kuanzia mwezi Disemba hadi Januari mwaka huu, hivyo kaunzia mwezi Febuari kazi itaendelea kwa ari kubwa.

Zanzibar leo

Share: