Habari

RC wa zamani Pemba adaiwa kugonga kwa gari na kuua

RC wa zamani Pemba adaiwa kugonga kwa gari na kuua

IMEANDIKWA NA MWANDISHI WETU-PEMBA

MTU mmoja aitwaye Zuhura Khamis Suleiman, miaka 38 mkaazi wa Mchangamrima Mbuzini, amefariki dunia baada ya kugongwa na gari iliokuwa inasemekana ikiendeshwa na Dadi Faki Dadi katika barabara ya Ole- Kianga Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Kamanda wa Polis Mkoa wa Kusini Pemba Hassan Nassir Ali alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 4:30 asubuhi.

Alisema kuwa, gari hiyo lenye namba za usajili Z963 DH liliacha njia na kugonga mti wa Mlimau uliokuwa pembeni na hatimae kumgonga mama huyo akiwa kando kando ya barabara.

“Inasemekana mama huyo alikwenda kununua samaki na ilikuwa ni mbali na barabara kuu, lakini baada ya gari hilo kushindwa kupinda kona, ilikwenda kugonga mlimau na kisha kumgonga marehenu ambae alifariki papo hapo”, alisema.

Aidha Kamanda huyo alimtaja dereva aliekuwa akiendesha gari hilo kuwa ni Dadi Faki Dadi mwenye miaka 57, ambae alikuwa akitokea Micheweni kwenda mjini Chake Chake.

Kamanda alisema chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi, ambapo dereva wa gari hilo alishindwa kupinda kona na hatimae kusababisha kifo cha mama huyo.

Aliwataka madereva kuacha tabia ya kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi, ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.

Katika kuondosha ajali za barabarani, Kamanda huyo alisema, wamekuwa wakifanya operesheni katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo, ili kudhibiti hali hiyo.

Kuhusu kumshikilia dereva huyo, Kamanda alisema awali baada ya tukio aliripoti kituo cha Polisi Micheweni, ingawa ameshaagiza aletwa Mkoa wa kusini Pemba kwa mahojiano.

“Kwa vile dereva ni mkaazi wa wilaya ya Micheweni, baada ya ajali alionekana kuripoti kule anakoishi, wilaya ya Micheweni Mkoa wa kaskazini, lakini taratibu za kuletwa Mkoa wa kusini tukio lilikotokea zimeshaanza,”alifafanua.

Hata baadhi ya mashuhuda waliokataa kutaja majina yao yachapishwe, walisema waliiona gari hiyo, ikiwe kwenye mwendo kasi, na baada ya muda mfupi ikayumba na kuingia kando ya barabara.

Walisema iliyumba kutokana na dereva kuonekana kushindwa kuiweza kona, na ndio ikagonga mti na kisha kumgonga mwanamke huyo aliefariki.

Kwa mujibu wa ripoti mwaka 2017 ya uhalifu na usalama barabarani ya Jeshi la Polisi Tanzania, imesema kuwa, kwa upande wa Zanzibar Mkoa wa Mjini Magharibi uliongoza kwa matukio 8,529 na, ambapo mikoa iliokuwa na idadi ndogo ya matukio ilikuwa ni Kusini Pemba 2,265 na Kaskazini Pemba 2,134.

Aidha ripoti hiyo ikaeleza kuwa, kwa mikoa miwili ya Pemba, kuliripotiwa watu 15 waliofariki kwa ajali za usalama barabarani, ambapo Mkoa wa kaskazini kuliripotiwa watu wanane na kusini watu saba.

Ripoti hiyo ikaeleza sababu tatu zinazopelekea ajali za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na za kibanadamu iliobainika kuchukua asilimia 86.4, ubovu wa vyombo vya moto imechukua asilimia 7.7. pamona na sababu ya kimazingira iliobeba asilimia 5.9.

Mwisho
PembaToday

Share: