Habari

SALIM BIMANI AICHAMBUA AFRO SHIRAZI NA MIAKA 41 YA CCM ZANZIBAR.

Akizungumza leo na Waandishi wa Habari pamoja na Vijana wa Vyuo Vikuu katika Ofisi za Chama Vuga Mjini Zanzibar, Mkurugenzi wa Habari wa Chama cha Wananchi CUF, Mh. Salim Bimani ameitofautisha miaka 41 ya CCM na malengo ya Afroshirazi, huku akidai kua, CCM Zanzibar imeshindwa kusimamia malengo hayo yaliyoasisiwa na Chama cha Afroshirazi Chini ya M’kiti wake Mzee Abeid Amani Karume.

Mkutano huo na Waandishi wa Habari umekuja kufuatia maombi ya Vijana wa Vyuo Vikuu wa CCM wakiomuomba Mkurugenzi huyo kuyatolea ufafanuzi baadhi ya mambo waliyoambiwa na Viongozi wa CCM juzi Alhamis tarehe 01/02/2018 katika Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu wa CCM lililofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili kupata uhakika wa mambo kama vijana wasomi.

Bimani amesema kua, “Tumefanya kikao hichi leo kutokana na maombi tuliyoyapata kutoka kwa Vijana wa Vyuo Vikuu wa CCM wakitaka tuyatolee ufafanuzi baadhi ya mambo waliyoelezwa juzi Alhamisi tarehe 01/02/2018 katika Kongamano la Vijana wa Vyuo Vikuu lililofanyika katika Ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakiliahi. Tunashukuru kuona Vijana wa Vyuo, sasa wanatumia upeo wao kuchambua mambo”.

Akitolea ufafanuzi wa mambo hayo, Mh. Bimani alionyesha maeneo matano ambayo yaligusa katika maswala ya Maendeleo ya Kiuchumi, huduma za kijamii kama vile elimu, matibabu, maji na makazi, Umoja na Mshikamano, Utawala bora na hadhi ya Zanzibar ndani ya mfumo wa Muungano na namna maeneo hayo yalivyokua yakisimamiwa na Chama cha Afroshirazi na yalivyoshindwa kusimamiwa na CCM kwa zaidi ya miaka 41 sasa.

Akizungumzia swala la maendeo ya kiuchumi, Mh. Bimani amesema kwamba, Afroshirazi ilisimamia vyema uchumi wa Zanzibar kwa kuimarisha Viwanda, huku akitaja Viwanda kadhaa vilivyokuepo Zanzibar kwa wakati huo na kuonyesha namna Viwanda hivyo vilivyohujumiwa na Viongozi wa CCM.

Bimani amesema kua, licha ya Afroshirazi kusimamia vyema Uchumi wa Zanzibar, pia ilifanikiwa kuhakikisha kua Zanzibar haidaiwi na nchi yoyote duniani, tofauti na sasa ambapo Serikali ya CCM hata kukopesheka haikopesheki.

Katika hatua nyengine, Mh. Bimani ameeleza kua, Afroshirazi ilitekeleza ahadi zake za kuwapatia Wazanzibari huduma zote za kijamii bure, kama vile, elimu bora bure, matibabu bure, maji bure na makaazi bure, huku akitolea mfano wa nyumba kadhaa zilizojengwa na Mzee Abeid Amani Karume ndani ya Visiwa vya Zanzibar kwa lengo la kuwapatia Wazanzibari Makaazi.

Akionyesha mfano wa nyumba hizo, Mh. Bimani alitaja nyumba za Michenzani ambazo pia zimejengwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba kama Vile Makunduchi, Micheweni, Chake Chake na maeneo mengine na kusema kua, licha ya nyumba hizo kujengwa kwa lengo la kuwapatia makaazi bure Wazanzibari, kwa sasa wakaazi wa nyumba hizo wanatozwa kodi kubwa sana huku nyumba nyengine wakimilikishwa Viongozi wa CCM.

Kwa upande wa elimu, Mh. Bimani amesema kua, Chama cha Mapinduzi sio tu kimeshindwa kutoa elimu bure kama ilivyokua kwa Mzee Abeid Amani Karume, bali pia kimeshindwa kusimamia sera bora za elimu jambo ambalo limepelekea Wanafunzi wa Shule za Zanzibar siku zote kutokea wa mwisho katika mitihani yao.

Akitolea mfano swala hilo, Mh. Bimani amesema kua
“Katika matokeo ya kidato cha nne yaliyotoka hivi karibuni, Zanzibar imetoa Shule 6 katika shule 10 zilizofanya vibaya Tanzania”.

Akiendelea kulichambua swala la huduma za kijamii, Mh. Bimani amesema kua, miaka 41 tokea kuasisiwa kwa Chama cha Mapinduzi swala la maji ni tatizo ndani ya Visiwa vya Zanzibar. Mh. Bimani amesema, kwasasa huduma ya maji ni lazima ulipie, huku akidai kua, licha ya Wananchi kulipia huduma hiyo yako maeneo ambayo huduma hiyo haipatikani. Bimani pia amesema, ni aibu kwamba CCM inatimiza miaka 41 sasa lakini watu wa Mjimkongwe wanakunywa maji chumvi na wengine wanatumia maji ya visima ambavyo vilifukiwa miaka mingi sana nyuma ambayo kwa mujibu wa Mh. Bimani, maji hayo sio salama.

Kwa upande wa Umoja na Mshikamano, Mh. Bimani alisema kua, lengo la Afroshirazi lilikua ni kuwaunganisha Wananchi wote pasi na kujali itikadi zao za kisasa na kusema kua, lengo hilo kwasasa limepuuzwa na Viongozi wa CCM.

Bimani amesema kua, kuwalisha Wananchi kasumba, kuhuribiri chuki na kuwagawa Wananchi ndiyo mambo yanayosimamiwa na Chama cha Mapinduzi kwasasa. “Tumeshuhudia chuki zikiwa zimeenea kila sehemu kuanzia katika nafasi za ajira na hata katika fursa za masomo, Watu wanabaguliwa kwasababu ya itikadi zao za kisiasa jambo ambalo Afroshirazi hawakua wakilifanya kipindi hicho”.

Akisistiza zaidi swala hilo, Mh. Bimani amesema kua, Ni aibu kwa Chama cha Mapinduzi ndani ya karne hii ya 21, karne iliyojaa wasomi kuhubiri Chuki na kuwagawa Wananchi, huku akisema kua hoja ya kurejeshwa kwa Sultan ni hoja ya kijinga. “Hoja ya kurejeshwa Sultan ni hoja ya kijinga kabisa,ivi CCM wanamdharau hadi Raisi wao mstaafu Dr. Salmin Amour ambae alitangaza hadharani katika sherehe za Mapinduzi kipindi kile kua Jemshid bin Abdallah amehusu Zanzibar na siku yoyote atakayoamua kurudi kwao arudi na anakaribishwa”.

Kwa upende wa swala la kupigania hadhi na maslahi ya Zanzibar, Mh. Bimani amesema kua, Afroshirazi ilihakikisha kua inasimamia maslahi yote ya Zanzibar ndani ya mfumo wa Muungano ambapo Chama cha Mapinduzi kwasasa kimeshindwa kufanya hivyo.

Akitolea mfano wa swala hilo Mh. Bimani amesema kua, CCM iliipoteza wenyewe hadhi na nafasi ya Raisi wa Zanzibar kua Makamo wa raisi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano. Pia Bimani alisema kua, CCM Zanzibar hadi sasa imeufyata na haijatoa taarifa yoyote ya kuitetea Zanzibar baada ya kutolewa kwenye shirikisho la Soka la CAF, badala yake imeendelea kukaa kimya na kupiga makofi tu.

Akitolea ufafanuzi zaidi swala hilo Mh. Bimani amesema kua, hata mambo ya Muungano kipindi cha Mzee Abeid Amani Karume hayakuzidi 11 lakini mara baada ya Chama cha Mapinduzi kuasisiwa mambo hayo yamekua yakiongezwa moja moja hadi sasa yamekua hayajulikani idadi yake huku CCM Zanzibar ikishindwa kusema chochote.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Mh. Bimani alisema kua CCM kwa sasa imepoteza muelekeo na kudai kua kusema CCM wamerithi Malengo ya Afroshirazi ni kuwadanganya Vijana.

CCM kesho tarehe 05/02/2018 inatimiza miaka 41 tokea kuasisiwa kwake ambapo Mh. Bimani amewataka CCM kuacha kuwadanganya Vijana, badala yake iwape ufafanuzi wa mambo hayo yamefikia wapi, ambayo kwa mujibu wa Bimani mambo hayo ni miongoni mwa mambo ambayo Afroshirazi waliyapigania bila ya kuhofu upande wa pili wa Muungano.

Mwisho, Mh. Bimani aliwataka Vijana wa Vyuo Vikuu kuendelea kukiunga mkono Chama cha Wananchi CUF na kuwaomba Vijana hao, waende wakawaelimishe na Vijana wengine Vyuoni kuhusu ukweli na umuhimu wa mambo hayo ambyao wameomba kupatiwa ufafanuzi.

Abeid Khamis Bakar
N/Mkurugenzi Habari na uenezi
JUVICUF Taifa

Share: