Habari

Sarakasi za CUF darasa tosha kwa vyama vya upinzani

Julius Mtatiro, mchambuzi mahiri wa habari na matukio hususan ya kisiasa katika makala hii anaeleza kwa kuviasa vyama vya siasa nchini Tanzania kujijenga kitaasisi na mifumo badala ya kutegemea uwepo wa mtu katika uongozi wa vyama hivyo.

Mtatiro kabla ya kujiunga na CCM, alikuwa mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF), amabye aliweza kushika nafasi mbalimbali za uongozi ngazi ya taifa ya chama hicho.

Hadi alipoamua kuhama CUF na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM) takriban miezi 7 sasa, alikuwa akimuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Soma makala yake..

Na Julius Mtatiro – Mwananchi
Jumapili, March 31, 2019

Hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania ilihitimisha kesi kuu ya msingi miongoni mwa mashauri mengi ambayo upande mmoja wa Chama cha Wananchi (CUF) uliufungulia upande mwingine wa chama hicho.

Kabla sijaendelea na makala hii nikiri kuwa kabla sijaachana na siasa za CUF na upinzani, nilikuwa mmoja wa watu waliokuwa na upande kwenye sarakasi hizo.

Sarakasi hizo zilitokana na sababu nyingi ambazo haziwezi kumalizika kirahisi.

Nyingi na hasa zilizokuwa zinaigusa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa zimezungumzwa hadharani na watu mbalimbali na wachambuzi wa kila aina, hizo siwezi kuzirudia mahali hapa.

Mimi nataka kujikita kuzungumzia sababu za ndani ambazo kwa uzoefu wangu wa siasa za upinzani zilishajihisha kukua na kutotatulika kwa mgogoro huo.

Ujenzi wa taasisi imara

Hapa namaanisha uwezo wa kuvifanya vyombo mbalimbali vya ndani ya taasisi kufanya maamuzi na usimamizi wenye tija au utekelezaji kwa jambo fulani bila kutegemea uwapo wa watu.

Yaani, unapokuwa na taasisi imara mahali fulani, hata kama mkuu wa taasisi hiyo anaondoka unao uhakika kwamba haitayumba na badala yake itakuwepo na kusonga.

Hata hivyo, kwa namna vyama vya upinzani vilivyojitengeneza Tanzania, kiongozi wa chama anao uwezo na nguvu kubwa kuliko chama chenyewe.

Tangu enzi za kina Mrema na Marando, vilijijenga katika misingi ya watu kuliko taasisi. Ukianza kuvikagua utakiri hilo bado ni jambo kubwa linaloviathiri na ni kikwazo kwa vyama hivyo.

Mfano, pale alipojiuzulu Profesa Ibrahim Lipumba mwaka 2015 na kurejea mwaka 2016, chama chake kikaparaganyika pande mbili. Pande hizo ni kiashiria cha namna vyama vya upinzani vilivyo na safari ndefu.

Upande wa Maalim Seif Hamad ulikuwa na watu wengi zaidi huku kwa Lipumba ukibakia na watu wachache ambao wasingeliweza kufanya chochote katika siasa za ushindani.

Yanayotokea sasa

Hali ya sasa ya Maalim Seif na watu wake kuhamia ACT-Wazalendo ni kiashiria kingine kuwa CUF ilikuwa inategemea watu, haikuwa inategemea taasisi.

Na mtu aliyekuwa na nguvu kuliko taasisi yenyewe anapohama, taasisi hiyo inabakia majengo na bendera – lakini tunafahamu chama siyo bendera wala majengo, ni watu.

Kwa vyovyote vile, sarakasi hizi za CUF zitaisha rasmi mwaka 2020. Kwa sasa CUF inapokea takribani Sh138 milioni kama ruzuku kila mwezi kutoka serikalini, inapata pia michango ya wabunge wa kila mwezi wa wastani wa Sh2 milioni.

Na ukiuangalia vizuri mgogoro huu wa CUF unaweza kusema kuna upande una ruzuku na upande wenye watu. Upande wenye watu umeondoka, upande wenye ruzuku umebakia. Tusisahau kuwa ruzuku siyo jambo la kudumu sana, linaisha mwaka 2020.

Vyote hivyo vinatokana na juhudi za chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, juhudi za namna hiyohiyo zinahitajika mwaka 2020 ili chama hicho kipate wabunge wengi zaidi.

Chama hicho kinapaswa kupata ruzuku kubwa zaidi au inayokaribiana na ya 2015; madiwani na halmashauri vivyo hivyo.

Je, itawezekana?

Si rahisi. Ngome kubwa ya CUF iko Zanzibar (na hasa Pemba), wabunge takribani 22 kati ya 32 wa kuchaguliwa wanatoka Zanzibar.

Wabunge wengine 10 ni wa Viti Maalumu. Kama ngome kubwa ya CUF imehamia ACT, manufaa yoyote ambayo yatapatikana Zanzibar kisiasa yatakwenda huko.

Bila shaka ACT itakuwa chama kikuu cha upinzani mwaka 2020 – 2025 kwa upande wa Zanzibar ambako kwa vyovyote vile CUF haiwezi kupata kiti hata kimoja cha udiwani au ubunge.

Kwa upande wa Tanzania Bara, ni wazi kuwa CUF hii mpya haitaweza kupata mbunge hata mmoja, ngome kuu za ubunge za CUF upande wa Tanzania Bara ni Tanga Mjini, Tandahimba, Mtwara Mjini na Kilwa Kusini.

Ngome zote naziona zikielekea CCM na takwimu za hivi karibuni zinaonyesha hivyo. Wananchi wa maeneo hayo wameanza kuiamini CCM baada ya kuona vyama vya upinzani vinakosa mielekeo sahihi.

Majimbo mengine ya CUF kama Kaliua, Mchinga na Kilwa Kaskazini; hata CUF isingelikuwa na mgogoro yangelirejea CCM.

Vyama vya vijifunze

Vyama vya upinzani visipoanza kujiendesha kitaasisi na kutegemea mifumo yake ya ndani kuliko majina ya viongozi wake, vitaishia kubaki na bendera na majengo.

Leo CCM ipo ilipo kwa sababu haitegemei majina ya kiongozi mmoja mmoja badala yake ina mifumo ya ndani ya chama.

Sarakasi hizi za CUF ni somo tosha kwa vyama vya upinzani kujenga mifumo imara itakayo zalisha taasisi imara ndani ya vyama hivyo.

Share: