Habari

Seif abariki Hamad kutoswa

Saturday, 31 December 2011 22:09

Katibu Mkuu wa Chama cha wananchi(CUF) Maalim Seif Shariff Hamadi akijiandaa kufungua kikao cha kamati tendaji ya chama hicho kujalidili la suala la mgogoro na Hamadi Rashid Mbunge wa Wawi mjini Zanzibar jana.Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Bara Julius Mtatiro na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar,Ismail Jussa Picha na Talib Ussi
Baraza Kuu kukutana Jumatano
Hamoud Said, Zanzibar na Geofrey Nyang’oro
MKUTANO wa Kamati ya Utendaji ya Taifa ya Chama cha Wananchi(CUF) uliomalizika jana visiwani Zanzibar umewaweka kitanzini wanachama 14 wa chama hicho akiwemo Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid kwa kosa la kupanga njama za kukidhoofisha chama hicho.Baada ya kumalizika kwa mkutano huo wa ndani uliokuwa chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad, Naibu Katibu Mkuu (Bara) Julius Mtatiro aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Baraza la Uongozi limejadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na suala la uvunjaji wa katiba ya chama lililokuwa likimkabili Rashid na wanachama wengine 13.


”Kamati ya Nidhamu ya chama na Kamati ya Maadili, ilileta kesi hii kwa kwa Baraza la Uongozi, baada ya kulijadili ilipendekezwa kuwa maamuzi yakatolewe katika mkutano wa Baraza Kuu la CUF litakalokutana Jumatano ijayo. Mkutano ujao utajadili tuhuma na kufanya uamuzi, “alisema Mtatiro baada ya siku mbili za mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Mazson.

Alisema kuwa Baraza hilo lilishawishika kwamba watuhumiwa hao 14 wakiongozwa na Hamad Rashid, walikiuka kifungu cha 63 cha Katiba ya chama hicho.

Makada hao ambao huenda wakatimuliwa uanachama ni pamoja na yeye mwenyewe Hamad Rashid Mohamed, Doyo Hassan Doyo, Shoka Khamis Juma, Juma Said Saanani, Yasin Mrotwa, Mohamed Albadawi, Mohamed Masaga, Doni Waziri, Yussuf Mungiro, Ahmed Issa, Tamim Omar, Amir Kirungi, Ayub Kimangale, and Haji Nanjase.

Hata hivyo, Mtatiro hakutaka kujibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari huku akisisitiza kwamba maswali na ufafanuzi zaidi utatolewa baada ya mkutano wa Jumatano.

Kauli ya Hamad Rashid

Akizungumza na Mwananchi Jumapili , Hamad Rashid alisema uamuzi uliofikiwa na Kamati ya Utendaji ya chama hicho wa kumfukuza, aliutarajia, hivyo atakwenda mahakamani kufungua kesi kupinga uamuzi huo.

Alisema kikao hicho cha siku mbili kililenga kupitisha mapendekezo yaliyokuwa yametolewa na Maalim Seif.

“Mimi nilijua kuwa wangefikia uamuzi huo,na hiyo ndiyo sababu nilikataa kuhojiwa na Kamati ya Maadili, kamati ile ilikuja ikiwa imepangiwa hatua za kuchukua dhidi yangu, ilikuja kutekeleza mapendekezo ya Katibu Mkuu,” alisema,

Aliongeza; “Imeteuliwa naye na kupewa maelekezo ya kufanya lakini zaidi hata kikao cha leo,kilichokutana kubariki madai ya kuwa mimi nilivunja katiba, kimekaa chini ya uenyekiti wake,

‘’Katika mazingira hayo ni dhahiri hata kikao cha dharura cha Baraza Kuu la chama kinachotarajia kukutana Januari 4 mwaka huu kitapitisha maamuzi hayo, ngoja tukae tusubiri”.

Hamad Rashid, alisema kwa sasa hatachukua hatua yoyote hadi kikao cha Januari 4 kitakapokaa na kutoa maamuzi yake.

Hata hivyo akasisitiza kuwa hatua yake ya awali ni kwenda mahakamani kupinga uamuzi huo.

Utabiri unatimia

Wachunguzi wa mambo ya siasa walitafsiri mkutano huo chini ya Maalim Seif dhidi ya hasimu wake kisiasa Hamad Rashid, ni sawa na kwamba ameshika kitanzi kitakachoamua hatma ya uhai au ukomo wa mwanasiasa huyo ndani ya CUF.

Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Maadili ya chama hicho, Abdul Kambaya, juzi alilieleza gazeti hili kwamba watuhumiwa hao wakipatikana na hatia, kamati hiyo inaweza kutoa mapendekezo kwa Baraza Kuu la kutoa onyo, karipio ama kuwafukuza uanachama.

Kambaya, alisema kamati hiyo imemaliza kuwahoji watuhumiwa 12 na mmoja ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu kutoka Mbeya, hakufika kuhojiwa.

Yaliyojiri mkutanoni

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kikao hicho cha siku mbili kilianza kwa kupokea taarifa mbalimbali za hali ya kisiasa nchini na ndani ya chama hicho, ikiwemo taarifa ya Kamati ya Nidhamu na Maadili , iliyowahoji wanachama 12, akiwemo Hamad Rashid ambao kwa pamoja waliipinga kamati hiyo kwa kuwa haipo kisheria.

Kikao hicho ambacho hufanyika mara moja baada ya miezi miwili, kilijadili kwa kina taarifa za kamati hiyo ya Nidhamu kupitia kwa Mwenyekiti wake ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Hamis Machano pamoja na Katibu wake Hamis Hassan ambao kwa pamoja walitoa taarifa za Kamati huku baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utendaji wakihoji kama taarifa hiyo ilizingatia masuala ya kiufundi.

Inaelezwa kuwa baada ya kutokea mvutano huo, ajenda hiyo iliahirishwa hadi jana, ambapo yalitolewa maamuzi kwamba hatma ya makada hao 14 itolewe na Baraza kuu Jumatano ijayo.

Chanzo Mwananchi newspaper.

Share: