Habari

Sera mpya ya Chadema yarudisha serikali tatu

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (wa pili kushoto) akiwa na viongozi waandamizi wa chama hicho wakionyesha kitabu cha sera mpya ya chama chao baada ya kuizindua mjini Dar es Salaam jana. Kuanzia kulia ni Naibu Katibu Mkuu (Zanziba), Salum Mwalimu, Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji na Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika. Picha na Said Khamis

By Kalunde Jamal – Mwananchi
Sunday, October 28, 2018

Sera mbadala za Chadema zilizozinduliwa mwezi uliopita zinaendelea kusambazwa na kujadiliwa. Sambamba na hatua hiyo chama hicho kikuu cha upinzani kinaendelea na operesheni yake ya ‘Chadema ni msingi’ ya kufungua mashina yake ili kuwa karibu na wananchi.

Miongoni mwa mambo yanayojitokeza katika sera mbadala na kuibua mjadala nchini ni pamoja umuhimu wa kufanyika mabadiliko ya katiba na hata kubadili aina ya muungano kuwa wa serikali tatu.

Katika uzinduzi huo wa sera hiyo pamoja na mambo mengine Chadema ilieleza kwa kina namna ambavyo serikali tatu zitafanya kazi tofauti na serikali mbili zilizopo sasa, kwa mujibu wa sera ya chama tawala, CCM.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anasema chama hicho iwapo kitachukua madaraka kinakusudia kutekeleza maoni ya wananchi kuhusu muundo wa Muungano kutoka mfumo wa serikali mbili kwenda wa serikali tatu.

Sera hiyo ambayo haitofautiani sana na ilani ya chama hicho ya 2015-2020, inakusudia kujenga muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao unadumisha Serikali tatu; Serikali ya Shirikisho ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.

Sera hiyo itasema, muungano chini ya Chadema utakuwa wenye uhalisia na uwazi kuhusu mambo ya muungano. Chadema inataka masuala ya msingi ya jumla yashughulikiwe na Serikali ya Shirikisho ya Jamhuri ya Muungano.

Mambo hayo ni katiba ya shirikisho, mambo ya nje, ulinzi na usalama, uraia, sarafu na Benki Kuu, mfumo wa elimu, Mahakama ya katiba na bunge la shirikisho.

Sera hiyo inabainisha kuwa Chadema itajenga mamlaka ya nchi ya kila mshirika wa Muungano katika kumiliki na kutumia rasilimali na maliasili zake.

Chini ya mfumo huo, “wananchi watanufaika kwa kuwa kutakuwa na matumizi makini ya rasilimali za nchi na Muungano utaimarika.”

Akifafanua, Mbowe anasema muundo unaokusudiwa unatokana na maoni ya wananchi waliyoyatoa mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya jaji Joseph Warioba. Maoni hayo yaliingizwa katika rasimu ya kwanza, lakini yalibadilishwa na Bunge Maalumu la Katiba.

Mbowe anasema sera hiyo mbadala imeweka wazi kuwa ukuu wa mamlaka ya kila nchi katika kumiliki, kugawa na kutumia rasilimali za umma na Chadema itaheshimu mamlaka ya nchi ya kila mshirika wa muungano katika kumiliki na kutumia rasilimali zake.

Kupitia sera hiyo moja kwa moja Chadema imerudisha hoja ya serikali tatu mezani kwa mjadala.

Mwanasiasa wa kwanza kuijadili ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia anayesema kuwa maoni ya wananchi yanapaswa kusikilizwa kwa kuwa ndio wenye mamlaka na taifa lao na ndio wanaopaswa kuamua wanataka kuongozwa vipi.

Mbatia ambaye pia alikuwa mjumbe wa Bunge la Katiba, anasema wananchi tayari walishaamua kuwa wanataka kuongozwa na Serikali tatu, na wametoa maamuzi hayo mara nyingi.

Anasema kuwa wakati wa awamu ya kwanza, chini ya Mwalimu Nyerere mwaka 1984, Makamu wa kwanza wa Rais, Aboud Jumbe alipendekeza kuwapo kwa serikali tatu.

Anasema wakati wa utawala wa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi mwaka 1991, kulipokuwa na vuguvugu la vyama vingi, Tume ya Jaji Francis Nyalali ilikuja na majibu hayohayo kutoka kwa wananchi.

Anakumbusha pia kuwa wakati wa utawala wa awamu ya tatu chini ya Benjamin Mkapa, Tume ya Jaji Robert Kisanga mwaka 1998 ilipendekeza vilevile na wakati wa Jakaya Kikwete katika awamu ya nne, Tume ya Warioba pia ilipendekeza.

“Mtu gani wa kujadili vinginevyo, ilhali wenye nchi yao wanataka kuongozwa kwa serikali tatu,” anasema Mbatia na kuongeza:

“Maoni yamekusanywa na majaji, wengine wamewahi kuwa kwenye nafasi kubwa kabisa katika nchi hii, walikuja na maoni hayo kutoka kwa wananchi sasa nani ana haki ya kuhoji,” anasema.

Anasema historia inaonyesha kuwa Juni 11 na 12, 1991 siku ya Jumanne na Jumatano katika ukumbi wa Diamond Jubilee kwenye kongamano la kwanza la kamati ya taifa ya mabadiliko ya katiba, NCCR Mageuzi walipendekeza mfumo wa serikali tatu. “Sisi ndiyo tuliouzaa mfumo huo,” anasema Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo.

Anasema muungano uliopo ni mzuri sana lakini muundo wake una shida, na suluhisho ni kuwa na mfumo wa serikali tatu.

Katika mjadala huo, Katibu wa NEC ya CCM, (siasa na uhusiano wa kimataifa), Kanali Mstaafu, Ngemela Lubinga anaeleza sababu chama chake kutokuwa na ajenda hiyo kwa sasa.

Anasema CCM ni chama kinachoongoza nchi na kina vipaumbele vyake na miongoni ni kuhakikisha kinaondoa kero wanazopata wananchi.

Anazitaja kero hizo ni msongamano hospitalini, upungufu wa dawa, shule, madawati na elimu sawa kwa wote na kina mama kujifungua mahali pasipo salama na stahili.

Anafafanua kuwa kutokana na hilo, ndiyo maana serikali inayoongozwa na CCM imeanza na kuondoa kero hizo lakini; “Kwa sababu kwenye ilani yetu tulitaja kujadili katiba mpya, tutarudi huko baada ya kumaliza vipaumbele muhimu kwa nchi.”

“Hivyo, tutarudi kujadili katiba, kama wabunge wa bunge hilo watakaoteuliwa wataona miongoni mwa mada zilizowasilishwa kwao ni pamoja na kujadili serikali tatu, itajadiliwa na kutolewa majibu kulingana na mahitaji,” anasema Lubinga.

Anasema mjadala ni mjadala na unapofanyika lazima kuwe na majibu kulingana na mahitaji ya wakati huo; “Nadhani watakaoteuliwa kwenye bunge hilo watakuwa na majibu sahihi.”

“Mimi si miongoni mwao nimejibu kwa sababu kwenye ilani ya chama changu tumetaja kushughulikia suala la katiba katika kipindi cha miaka mitano yaani 2015-2020, lakini siyo kipaumbele chetu ndiyo maana hatujaanza nacho.”

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF upande wa Maalim Seif, Salum Bimani anasema nchi inahitaji mjadala wa kitaifa kuhusu hali ya siasa ilivyo hapa nchini, lakini si kuhusu suala la serikali mbili au tatu ambalo lilishaamuliwa.

Anasema serikali tatu wananchi walishaamua kuwa wanataka serikali tatu na maoni yao yalishakusanywa, walioharibu ni watawala kwa kuyakataa.

“Suala hilo ni la kikatiba, hivyo lazima litekelezwe sasa na si wakati mwingine, tena lifanywe haraka,” anasema Bimani.

Anasema “Kuna manufaa makubwa iwapo maoni ya wananchi yatapewa nafasi na kuwapo kwa serikali tatu, tume huru ya uchaguzi, uhuru wa habari na kujieleza, yote yamejadiliwa humo na wananchi wenyewe wenye nchi yao.”

Vilevile, Naibu Mkurugenzi, Mawasiliano wa Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Profesa Lipumba, Abdul Kambaya anasema suala la serikali tatu ndio msimamo wa chama chao.

Anasema msimamo wao ni kuwa na Serikali tatu kama kuna haja ya Muungano wenye tija , tofauti na huu usiokwisha malalamiko.

“Serikali tatu, yaani Zanzibar, Tanganyika na Serikali ya jumla, ambayo itakuwa kati ikiziita hizi serikali mbili kusikiliza kero zake na kuzipatia ufumbuzi,” anasema Kambaya.

Anasema serikali hiyo ndiyo itajadili kero hizo kila zitakapotokea, na kuleta tija kwa pande zote mbili.

“Hivi sasa Serikali ya Muungano pekee ndiyo inaitisha majadiliano, upande mmoja una chuki na kuona unaonewa, lakini zikiwa tatu haya manung’uniko ya kuonewa yatapungua kwa sababu yatapatiwa ufumbuzi kila yanapotokea,” anasema.

Anafafanua kuwa unahitajika mjadala mpana utakaohusisha wananchi, wanaharakati na vyama vya siasa kujadili faida za serikali tatu na athari za mbili zilizopo, ukilenga katika manufaa ya Muungano.

“Manung’uniko ya Muungano hayana majibu kwa sababu hakuna mtu wa kati anayeunganisha wengine. Serikali hiyohiyo ya Muungano ndiyo iitishe vikao kujadili malalamiko, lazima jibu la maana halitapatikana,” anahitimisha Kambaya.

Share: