Habari

Serikali kujenga miji 18 ya kisasa

AUGUST 5, 2018 BY ZANZIBARIYETU

KATIBU Mtendaji Tume ya Mipango Juma Hassan Reli amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina mpango wa kujenga miji mipya 18 ya kisasa kwa ajili ya makaazi ya wananchi.

Alisema mpango huo umekusudia kuendeleza sera ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Amani Karume itakayosaidia kuleta suluhisho la uvamizi wa maeneo ya kilimo nchini.

Alieleza hayo alipokua akizungumza na madiwani na mashekha wa wilaya za Magharibi ‘A’ na ‘B’ katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni.

Aidha alisema, miongoni mwa mkakati wa mpango wa kupunguza umasikini (MKUZA) ni pamoja na kuthibiti matumizi mabaya ya ardhi hasa ikizingatiwa ndio rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchini yoyote duniani.

Alisema serikali kwa kutambua hilo, inaendeleza juhudi za uimarishaji wa miundombinu mbali mbali ikiwemo suala zima la ujenzi wa nyumba za maendeleo, maeneo ya kilimo na uvugaji, maji safi na salama ili kuhakikisha wananchi wanaondokana na umasikini uliokithiri.

Alisema mkakati huo unahitaji kupewa nguvu za pamoja baina ya viongozi wa halmashauri, wilaya na wananchi kwani bila ya mashirikiano ni vigumu kufikia malengo.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohammed katika alisema, serikali kupitia wizara hiyo, itahakikisha sekta zote miradi inayoekezwa Zanzibar inafuata taratibu na malengo ya serikali kwa ajili ya kuleta maendeleo na ukuaji uchumi.

Alisema katika hilo, serikali haitokuwa na mzaha kwa wizara au taasisi ambayo itakiuka taratibu zilizopangwa hasa ikizingatiwa imetumia fedha nyingi za serikali.Dk.Khalid alisisitiza suala la uadilifu,uwazi na kuheshimu taratibu kwa watendaji katika dhamana walizokabidhiwa na serikali kwani kufanya hivyo ndio dira ya upatikanaji wa maendeleo na upatikanaji wa huduma za kijamii nchini.

Pia alisisitiza ushiriki wa watu wote katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya serikali ambapo alisema ndio msingi mkubwa wa ukuzaji wa uchumi na kuondokana na tatizo la umasikini.

Chanzo: Zanzibar Leo

Share: