Habari

Serikali kuweka wazi taarifa za biashara

NOVEMBER 10, 2017 BY ZANZIBARIYETU

NA HAFSA GOLO

WIZARA ya Biashara, Viwanda na Masoko, inaandaa utaratibu wa kuweka wazi taarifa za kibiashara hasa zinazohusiana na masoko na bei za kimataifa kwa bidhaa za Zanzibar.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Juma Ali Juma, alieleza hayo alipokua akifungua warsha ya siku mbili kwa wafanyabiashara wakubwa na wakati.

Miongoni mwa taratibu zitakazowekwa kwenye mfumo huo, alisema ni pamoja na kuvutia mitaji itakayoongeza uwekezaji kwenye sekta ya biashara.

Alisema lengo ni kurejesha hadhi ya Zanzibar kama kituo kikuu cha biashara katika eneo la Afrika Mashariki.

Alisema utekelezaji wa suala hilo umefanywa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na serikali ya Jamuhuri ya Tanzania, Shirika la Kimataifa la Biashara Duniani (WTO) na Kituo cha Kuendeleza Biashara cha Kimataifa (ITC).

Nae Ofisa biashara kutoaka wizara hiyo, Zuwena Abdalla Hilali, alisema serikali imeona umuhimu wa kuwapatia taaluma wafanyabiashara ili kutambua fursa zilizopo.

Alisema warsha hiyo pia imelenga kuweka mikakati itakayoharakisha ufanyaji biashara na udhibiti wa changamoto zinazojitokeza.

Mkufunzi kutoka wizara viwanda, biashara na uwekezaji, Tawi Kilumile, alisema changamoto zinazojitokeza katika eneo la biashara zinatokana na mlolongo mkubwa wa vibali.

Alisema changamoto nyengine ni kukosekana uwazi kwa wafanyabiashara kuhusu taratibu na vibali vinavyotakiwa pamoja na ushirikiano mdogo kati ya serikali na wafanyabiashara.

Kwa upande wake mfanyabiashara, Fikirini Hamza, alisema, changamoto ya sheria za kodi baina ya Zanzibar na Tanzania Bara, ulipaji ushuru bandarini ambao hauna mfumo maalumu bado ni changamoto kubwa kwao.

Zanzibar Yetu

Share: