Habari

Serikali yaipa MOBH fursa ya uwekezaji

September 20, 2018

NA OTHMAN KHAMIS, OMPR

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imetiliana saini na kampuni ya kimataifa ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group (MOBH) ya mjini Dubai, kwa lengo la kuunga mkono uimarishwaji wa uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Khalid Salum Mohamed alitia saini mkataba huo kwa niaba ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati kampuni ya Mohammed Omar Bin Haider Holding Group ikatiwa saini na mkurugenzi wa bodi akiwa pia meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Omar Mohammad Bin Haider.

Madhumuni ya mkataba baina ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kampuni hiyo ni kuunga mkoni jitihada za serikali katika kuunga mkono na kuimarisha uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi hapa Zanzibar.

Hafla hiyo fupi ilifanyika jana ambayo ilishuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi anayetokea nchini China kuhudhuria maonyesho ya 15 ya kimataifa ya China- Asean Expo 2018 yaliyofanyika katika mji wa Nanning katika jimbo la Guangxi.

Akizungumza baada ya utiaji saini mkataba huo waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Khalid Salum Mohamed alisema Zanzibar itatoa kila ushirikiano kuwa kwa kampuni hiyo yenye makao yake nchini Dubai inazitumia fursa za uwekezaji zilizopo Zanzibar.

Dk. Khalid alisema Zanzibar ilikuwa kitovu cha harakati za kibiashara iliyokuwa ikiunganisha bara la Asia na ukanda wa kusini na Mashariki mwa bara la Afrika lenye wakaazi zaidi ya milioni 360,000,000 hivi sasa imepania kuirejeshea hadhi yake kwa kutanua maeneo mengine ya uwekezaji.

Alisema miundombinu iliyoimarishwa katika sekta za mawasiliano ya anga, uvuvi wa bahari kuu, utalii na biashara ikiambatana na sera inayotekelezeka imezingatia kuwajengea mazingira bora wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza miradi yao katika mfumo watakaopenda ukiwemo ule wa ubia.

Zanzibarleo

Share: