Habari

Shamrashamra Miaka 54 ya mapinduzi

Miradi 54 kuzinduliwa, kuwekwa mawe ya msingi

NA KHAMISUU ABDALLAH

MIRADI 54 inatarajiwa kuzinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika shamra shamra za maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza na vyombo vya habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed ofisini kwake Vuga alisema miradi hiyo ni pamoja na umeme, barabara, vituo vya afya, skuli na maji safi na salama.

Alisema miradi hiyo itazinduliwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na vingozi wengine wa serikali.

Alisema uwekaji wa mawe ya msingi na ufunguzi wa miradi hiyo utaanza rasmi Januari mosi hadi Januari 11 katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba ikiwemo uzinduzi wa umeme katika kisiwa cha Fundo.

Alisema lengo kuzinduliwa kwa miradi hiyo ni kuleta mabadiliko makubwa katika visiwa vya Unguja na Pemba na kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo, kuondosha ubaguzi katika nchi ili vizazi vijavyo virithi matunda hayo.

Alisema katika miaka 54 ya Mapinduzi matufuku ya mwaka 1964, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika kufanya maendeleo katika sekta hizo ukilinganisha na miaka ya nyuma iliyopita.

Akizungumzia matukio rasmi ya shamrashamra hizo, alisema zitaanza rasmi Disemba 31 kwa shughuli za usafi wa mazingira katika wilaya zote za Unguja na Pemba.

Hivyo, aliwaomba viongozi wote wa serikali, wilaya, halmashauri, mabaraza ya Manispaa, mabaraza ya miji na masheha kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio makubwa katika maeneo yao.

Aidha, alisema Januari 11 mwaka 2018 sherehe mbalimbali zitafanyika katika viwanja vya Maisara ikiwemo upigaji wa fashfash, upigaji wa mizinga, honi za meli na gari ambapo pia upigaji wa fashifashi utafanyika katika uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.

Hata hivyo, waziri Aboud, alisema kilele cha maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi Januari 12 kitafanyika katika Uwanja wa Amani kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi 5:30 asubuhi ambapo mgeni Rasmi atakuwa ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.

Zanzibarleo

Tagsslider
Share: