Habari

Sheikh Ponda: Bora tuchelewe uchaguzi tupate katiba mpya

Ibrahim Yamola – Mwananchi
Jumapili, Novemba 25, 2018

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema kufanya Uchaguzi Mkuu ujao mwaka 2020 kwa Katiba ya sasa na Tume ya Uchaguzi ya sasa ni hatari na ameshauri kwamba ni bora kuuahirisha.

Sheikh Ponda amesema hayo kipindi ambacho kumekuwa na mjadala wa Katiba Mpya na tume huru ya uchaguzi hasa baada ya Rais John Magufuli kusema serikali haitatenga fedha sasa kwa ajili ya katiba.

Baada ya kauli hiyo ya Rais Magufuli, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku walisisitiza umuhimu wa Katiba Mpya.

Mchakato wa Katiba Mpya ambao uliasisiwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete mwishoni mwa mwaka 2011, uliishia kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambalo licha ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ambayo imekwama, haijapigiwa kura ya maoni.

Akizungumza katika mahojiano maalumu alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) zilizopo Tabata Relini, Dar es Salaam, Sheikh Ponda alisema kunahitajika mkutano wa kitaifa ili kufanikisha masuala hayo.

“Hili suala la fedha, anachokizungumza (Rais) hakiwezi kuwa kikwazo. Fedha zinatafutwa. Tukiitisha mkutano wa kitaifa wa katiba utakaokuwa umeshirikisha watu mbalimbali, suala la fedha litazungumzwa.”

“Kutazungumzwa tunaanzia wapi na tunaamini haya si mambo makubwa kama tutakaa meza moja na kuzungumza,” alisema Sheikh Ponda

Kiongozi huyo wa Taasisi za Kiislam alisema chaguzi ambazo zimefanyika huko nyuma na mazingira ya sasa ya wananchi kutokuwa na imani ya Tume ya Uchaguzi (NEC), ni bora mambo hayo yakashughulikiwa kwanza kabla ya kuingia kwenye uchaguzi wowote.

“Sisi tunashauri wakati mwingine bora tuchelewe kuingia kwenye uchaguzi kuliko kuingia na katiba hii, hali halisi ya chaguzi zetu na yale yaliyojitokeza yana nafuu zaidi kuliko wakati ujao.”

“Kuingia kwenye uchaguzi mwingine bila kuwa na katiba na ukiangalia hali ya wananchi, wamechoka, wamekata tamaa, wanafikiri wasishiriki chaguzi kwa hiyo suluhisho ni katiba mpya na tume huru,” alisema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda alisema, “Tukiingia kwenye uchaguzi hakuna katiba hakuna tume huru halafu jamii imechoka zaidi unaingia katika jambo la kubahatisha zaidi. Tunapendekeza hili jambo lifanyike kabla ya uchaguzi wa mwaka 2020.”

“Tume tuliyonayo sasa haiwezi kukidhi haja, tatizo kubwa ile tume inaundwa na washiriki wa kisiasa na kuna methali inasema yule anayemtunza mpiga zumari ndiye anayechagua wimbo.”

Katika kusisitiza hilo, Sheikh Ponda alisema, “Iwe tume huru, iwe na maofisa wake kuanzia ngazi za kata na ithibitishe kuwa chombo hicho kimeundwa na watu huru.”

Novemba Mosi, Rais Magufuli akizungumza katika kongamano la uchumi na siasa lililofanyikia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema hawezi kutenga fedha kwa ajili ya mchakato wa katiba licha ya kutambua kiu ya wananchi kupata Katiba Mpya.

Rais Magufuli alisema wanaotaka kusaidia kutoa fedha kwa ajili ya mchakato huo wazilete zikatumike katika miradi ya maji na barabara.

“Sasa sifahamu baada ya rasimu ya Jaji Joseph Warioba miaka minne iliyopita tunaendelea na hiyo rasimu au tunakwenda kuanza upya. Badala ya kulumbana kwa hayo ya katiba bora tufanye kazi sasa,” alisema Magufuli.

Alisema kuna nchi zenye katiba za miaka mingi ambazo zimezifanyiwa marekebisho.

“Lakini watu wameng’ang’ania katiba mpya utadhani ndiyo suluhisho la matatizo yote,” alisema Magufuli na kusisitiza kuwa hawazuii wanaotoa maoni yao, lakini mtazamo wake ni Tanzania kwanza.

Katika mahojiano hayo, Sheikh Ponda ambaye ni mzaliwa wa Kigoma alizungumzia hali ya kisiasa nchini akisema, “Sio nzuri kwa sababu hakuna mwafaka wa pamoja wa kisiasa. Kuna mitazamo mingi ya kisiasa na usawa haupo.”

Alisema siasa zina mambo yake kama watu kusimama kueleza sera, kushauri serikali lakini sasa hairuhusiwi kupanda majukwaani.

Kiongozi huyo ambaye aliwahi kukamatwa na kuhojiwa uraia wake na paspoti yake kushikiliwa alisema, amekuwa akiingia katika mvutano mara kadhaa na serikali.

Share: