Habari

Shein ‘Apigilia Msumari’ Kwenye Muungano

2nd March 2014

Na Romana Mallya

Asema ni tumaini la kuziunganisha nchi za Afrika

Wakati hofu kuhusu hatma ya Muungano wa Tanzania ikizidi kuongezeka, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Muungano huo ni moja ya tunu zinazopaswa kulindwa kutokana na umuhimu kwake kwa bara la Afrika.

Amesema wakati Tanzania ikiadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Afrika haikufanikiwa kwa sababu baadhi ya viongozi wake hawakuwa na nia ya dhati kama walizokuwa nazo waasisi wetu marehemu, Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Aman Karume.

Dk. Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, sherehe ambazo zilifanyika Salama Bwawani, Zanzibar.

Maadhimisho hayo ambayo kilele chake ni Aprili 26, mwaka huu, yamebebwa na kauli mbinu isemayo, ‘Utanzania Wetu ni Muungano Wetu; Tuulinde, Tuuimarishe na Kuudumisha’.

Katika hotuba yake, Rais Shein alisema Muungano ambao unaadhimishwa ndio tumaini pekee la bara la Afrika katika azma ya kuwa na muungano kwa nchi za Afrika.

“Muungano huu ni fahari ya Afrika na unatumika kama mfano na kigezo kwa nchi nyingine za bara hili katika kuleta umoja na muungano wa kweli,” alisema.

Aliongeza kuwa ni dhahiri kwamba kama Afrika ingekuwa na viongozi waliojidhatiti na wa kweli kama marehemu Karume na Mwalimu Nyerere, hivi sasa wangezungumzia Shirikisho la Nchi za Afrika kutoka miaka ya 60.

“Lakini ndio kwanza nchi za Afrika Mashariki hivi sasa zimeanza mchakato wa kutaka kuwa na shirikisho kamili la kisiasa la Afrika Mashariki,” alisema.

Alitaja baadhi ya nchi za Afrika ambazo ni Gambia, Misri, Senegal, Libya nazo kwa nyakati tofauti zilijaribu kuungana lakini mwisho wa siku hazikufanikiwa kudumu.

Pia alisema baadhi ya nchi zilizopo kwenye mataifa makubwa duniani zinatamani kuungana kama ilivyo hapa nchini lakini imeshindikana.

Alisema muungano wa Tanganyika na Zanzibar umedumu kutokana kwa sababu ulikuwa muungano wa watu ambao ni wamoja kiasilia, kimila, kilugha, kiutamaduni na kisiasa.

Pia alisema utamaduni wa kukaa pamoja na kuzungumzia changamoto zinazojitokeza na kuzifanyia kazi kwa kuzingatia amani na mshikamano, umeongeza ufanisi katika hilo.

Kuhusu changamoto ya suala kuchangia shughuli za muungano pamoja na mafuta na gesi, Dk Shein alisema anaamini ifumbuzi wake utapatiakana.

Alitaja baadhi ya mafanikio kuwa utekelezaji wa sheria ya haki za binadamu Zanzibar, uwezo wa kukopa ndani na nje ya nchi na misamaha ya mikopo ya fedha kutoka IMF.

Katika suala zima la kuimarisha Muungano, Shein alisema mabadiliko kadhaa yamefanyika na kubwa ni hili linaloendelea hivi sasa la kuandikwa kwa katiba mpya.

“Naamini wabunge watatimiza wajibu wao kwa kuifanya kazi ya kutunga Katiba mpya kwa uadilifu na kuongeza umakini wao na hatimae kutoa Katiba ambayo itazingatia maslahi ya nchi na wananchi wa pande zote mbili,” alisema.

Alisema muungano umedumu hadi sasa kutokana na hoja na sera sahihi za kuanzishwa kwake huku jitihada za kuziendeleza kufanywa na viongozi watawala.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Tanzania bara na visiwani, akiwamo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi pamoja na William Lukuvi ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Tagsslider
Share: