Habari

Shein: Kinachosubiriwa Zanzibar ni tarehe ya uchaguzi

Vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mjini Magharibi wakiwa na mabango wakipita mbele ya viongozi walikuwepo jukwaa kuu kwenye sherehe za kilele cha miaka 52 ya Mapinduzi Zanzibar zilizofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, mjini Unguja jana.

Uwanja wa Amani, Zanzibar
Wednesday, January 13, 2016

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema uchaguzi Zanzibar, utarudiwa na kinachongojewa ni tarehe itakayotangazwa baadaye na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Alitoa kauli hiyo jana wakati wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja wa Amaan na kuhudhuria na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Rais, John Magufuli, makamu wake, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.

Wengine ni marais wastaafu, Jakaya Kikwete na Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohamed Gharib Bilal, Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho na mabalozi mbalimbali.

Hata hivyo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad hakuhudhuria kutokana na mgogoro wa kisiasa unaoendelea visiwani humo.

Katika hotuba yake ya saa 1.05 ambayo imechapishwa yote katika gazeti hili, Dk Shein alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, Sheria ya Uchaguzi namba 11, ZEC ndiyo yenye jukumu la kuendesha uchaguzi wa Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani.

“Kwa mujibu wa Katiba na Sheria ya Zanzibar, uchaguzi utarudiwa,” alisema Dk Shein huku akishangiliwa.

Dk Shein alitoa kauli hiyo siku moja baada ya Maalim Seif aliyeshindana naye kuwania urais kusema CUF haiko tayari kurudia uchaguzi na suluhu ya mkwamo huo ni kutangazwa kwa mshindi ili iundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Dk Shein alisema mazungumzo ya kutafuta suluhu yanayowashirikisha wajumbe sita yanaendelea na taarifa rasmi itatolewa baada ya mazungumzo hayo kukamilika.

“Katika kipindi hiki, naomba wananchi muwe wavumilivu na wastahamilivu, mwendelee na shughuli zenu za maisha ya kila siku na ZEC itatimiza wajibu wake,” alisema Dk Shein.

Wakati Dk Shein akimtaja Rais mstaafu, Amani Abeid Karume wananchi walioshiriki sherehe hizo walipiga kelele na wakati kiongozi huyo aliyeasisi Serikali ya Umoja wa Kitaifa alipokuwa akiondoka, alisimama kidogo kusikiliza kelele za wananchi waliokuwapo katika uwanja huo.

Awali, akimkaribisha Dk Shein, Balozi Idd alisema Wazanzibari wana kila sababu na haki ya kuadhimisha mapinduzi hayo yaliyowakomboa kutoka kwenye dhuluma na umaskini huku akirusha vijembe kwa CUF waliosusa sherehe hizo.“

“Walifikiri kutoshiriki kwao tusingeweza kufanikisha, lakini tumeweza. Je, yamekuwa hayakuwa?, wananchi wakaitia “yamekuwaaa.”

Awali, Dk Shein alikagua gwaride la vikosi vya majeshi na baada ya shughuli hiyo askari hao walikwenda kukaa katika majukwaa.

Dk Magufuli awa kivutio
Katika sherehe hizo, Rais Magufuli alikuwa kivutio hasa pale alipokuwa akiingia uwanjani, hiyo ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu kushika wadhifa huo. Wananchi wengi walimshangilia huku wakisema ‘Hapa Kazi Tu’.

Kulikuwa na mabango mengi yaliobebwa na waandamanaji yakimsifu Dk Magufuli kwa kutumbua majipu huku baadhi ya wananchi wakimwambia kwamba Zanzibar, pia majipu yapo. “Na Zanzibar yapo majibu njoo uyatumbue haraka,” walisikika wakisema.

Burudani
Wimbo uliotawala katika uwanja huo ni ule unaopendwa kuimbwa na wana CCM ambao ni “Piga ua hatutoi nchi,” wimbo mwingine ambao uliongozwa na bendi za polisi ni, “Sisi sote tumegomboka,” ambao ulitumika baada ya Mapinduzi kuonyesha kwamba wale waliojitolea na kufa kwa ajili ya kupigania nchi na ule wa “Tunaye Dk Shein tunaye.”

Bango la ubaguzi latia nyongo
Wakati shamrashamra hizo zikiendelea, CCM imeomba radhi kutokana na ujumbe uliokuwa na maudhui ya kibaguzi kwenye moja ya mabango yaliyobebwa na wafuasi wake katika mkutano maalumu wa maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar, uliofanyika kwenye Viwanja vya Maisara Suleiman juzi.

Chama hicho kimeeleza kusikitishwa kwake kutokana na kitendo hicho na kukikemea vikali.

Katika mkutano huo, kundi la vijana waliokuwa wamevaa fulana na kofia za CCM, lilipita mbele ya Dk Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Zanzibar, likiwa bango lililokuwa limeandikwa “Machotara Hizbu Zanzibar ni nchi ya Waafrika.”

Picha hiyo ilisambaa jana kwenye mitandao ya kijamii huku baadhi ya watu wakionyesha hisia tofauti juu ya ujumbe huo.

Saa chache baadaye, Mkuu wa Mawasiliano kwa Umma wa CCM, Daniel Chongolo alitoa taarifa akisema: “Chama kimesikitishwa na ujumbe wenye maudhui ya ubaguzi ulioandikwa kwenye bango lililobebwa na mmoja wa wananchi waliojitokeza katika maadhimisho ya sherehe za miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.”

“Chama cha Mapinduzi kinaomba radhi kwa ujumbe huo, kinapinga na kinakemea kabisa fikra, hisia na mitazamo yoyote yenye maudhui ya kibaguzi,” ilisema taarifa ya Chongolo.

Alisema ujumbe huo si tu una maudhui ya kibaguzi, bali pia unakwenda kinyume kabisa na falsafa na shabaha ya waasisi wa Mapinduzi hayo ya mwaka 1964.

Kauli ya Chadema
Bango hilo lililaaniwa pia na chama cha upinzani, Chadema ambacho kupitia kwa Mkuu wake wa Idara ya Mawasiliano na Habari, Tumaini Makene kilisema kinalaani na kupinga mipango, mikakati, tabia na chembechembe za ubaguzi wa aina yoyote, ukiwamo ulioonyeshwa kwenye bango hilo.

“…Kupitia kwa Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete (CCM) kama hakiko nyuma ya ajenda hizo za kibaguzi na fikra hizo za kikaburu, kichukue hatua za haraka mara moja kuwawajibisha viongozi wake waliosimamia na kuachia jambo hilo,” alisema Makene.

Share: