Habari

SIASA YA ZANZIBAR NA KIDONDA KISICHOPOA

Kwa kawaida binaadamu yeyote yule hupenda lile analolihitaji alipate. Liwe na madhara au faida, kwake si chochote si lolote. Apate tu analolihitaji aridhishe nafsi yake. Naam aridhishe hata kama lina madhara atajua mbele kwa mbele. Kwani si wapo wanaosema potelea mbali nzi kufia kwenye kidonda si hasara. Yaani yeye ameshajifananizisha na nzi kutafuta hata kama lina madhara kwake apate tu kufa kupona.

Katika huko kufia kwenye kidonda ndipo atakaposhindana na mwenye kidonda kumkera kwa milio na sauti ili tu ang’ong’e ama harufu au utamu ule aupatao kwenye hicho kidonda. Ingawa mwenye kidonda huchukua juhudi kipoe lakini nzi kwa vile kidonda hicho kinamaslahi kwake hapendi kipoe ndipo utasikia kila kukicha ‘ziiiiii zziiii ng’oo’ apate hilo linalomnufaisha kwake.

Kuendelea kumuachia nzi anufaike na kidonda hicho ni kuendelea kuuguza jeraha ambalo litadumu na kuongeza idadi ya nzi. Unashangaa wataongezeka! Ndio wataongezeka tu maana wameshaona na wameshajithibitishia kuwa mwenye kidonda ‘bwege’ hivyo wamng’ong’e tu ‘uyakhe na uami’ umemjaa. Masikini hujitahidi nae kutia dawa na pia kukifungia bendeji likafunga ‘barabbara’ ila na nzi nae anajua kunukiliza. Eh! nzi anakera huyu. Kaipata harufu na sasa anakera tena sio anakera tu bali ameking’ang’ania maana huo ndio uhai wake.

Kukera huku kunatia khofu mbili moja usalama wa nzi ingawa ni mweledi wa kuruka, usalama wake unaweza kuwa hatarini. Mwenye kidonda anaweza kuchoshwa na akaamua kumtegea nzi akitua ampige kofi afie juu ya kidonda kama alivyokwishajiapiza. Kufa kwake pia kutaleta athari nyengine ya kuumiza kidonda kilichokwisha pata nafuu.

Mithili ya siasa hizi za nzi na mwenye kidonda ndio hasa siasa za Zanzibar. Kuna viongozi ambao wao ni kama nzi wasiopenda kuwaona Wazanzibar ambao kwa asilimia 75 koo zao zimeungana kama si kwa mjomba ni kwa shangazi. Wenyewao wana msemo husema ‘ndugu wa mwenzako ni wako’ lengo la msemo huu ni kukoleza huruma baina yao. Na pale wanapotaka kutambuana utasikia tu wao hujuana kwa vilemba. Sadakta hujuana kweli kwa vilemba; sura zao, sauti zao na mienendo yao ni mshabaha unaorindana.

Upishi na upalilizi wa moto kwa chuki hizi si kama haujuilikani, la hasha! Unajuilikana ila wenye kufaidika na donda hili la chuki ni kishungu kidogo cha nzi ambao wao hupasiana kijiti kutoka mmoja kwenda mwengine waselelee na harufu. Kidonda hiki unaweza ukipenda kukiita sugu kimekua kikipatiwa dawa dahari na dahari hakipoi maana kikipoa nzi hatokua na uhai. Mara ya mwisho mwenye kidonda na daktari walikutana November 2009 wakitibu (ushahidi wa vyeti vya hospitali upo) kutibu kwake ni lazima kifanyiwe uperesheni (upasuaji). Na kabla ya upasuaji ridhaa ya wanafamilia ilitakiwa na ikapatikana asilimia 68.7 iliokubali upasuaji ufanyike. Bahati mbaya mtaalamu wa upasuaji alistaafu kazi kabla ya kupoa kwa kidonda na kumuachia daktari mwengine afanye ukaguzi wa mara kwa mara.

Daktari ambaye aliachiwa akifanyie ukaguzi yawezekana aliacha kufanya ukaguzi wa kutosha au mwenye kidonda alibweteka na unafuu wa maumivu ingawaje athari ya kutoka toka maji au uchafu ulishaanza kuonekana. Athari ya kutoka maji ilionekana kwa nzi kuanza kuking’ong’a. Kidonda kilipelekwa kwa dakatari ila bahati mbaya kumbe si mweledi imebainika nzi anawaogopa. Nzi pia wamebaini kuwa huyu ni daktari muoga hivyo waacha tu wang’ong’e hadi bendeji lifunguliwe wacharukwe. Hapa ndipo penye hatari.
Kidonda kinanuka na uvundo wake unaathiri si pua tu ambapo utachukua kidole gumba na cha shahada kubana tundu za pua kuzuia harufu isiingie ubongoni na kuleta hisia ya kukirihisha kwake, bali unaathiri akili na maisha ya ujumla ya mwenye kidonda na wale waliomzungurukwa.

Tunasikia ati madaktari wanakutana lengo kuu ni kutibu donda. Sasa mbona kuna kelele nyingi huku nje. Huu ni uperesheni wa aina gani? Usiokuwa na hata makadirio ya kwisha kwake! Jopo hili la madaktari kubwa ambalo miongoni mwao ndio hao nzi au wenye kulea nzi wanufaike na donda hili. Jee wataridhia ipatikane dawa mjarrabu wa kuondosha kabisa kidonda na hata itakayofuta na kovu? Jibu linanipa mashaka kulitoa. Naogopa kutoa jibu nikaonekana mimi pia ni sehemu ya upaliliaji wa mzozo huu.

Kupaza sauti ndani ya mzozo huu ni sawa na kujifananizisha na aliekuwa Waziri wa Habari nchini Iraq Mohammed Saeed al-Sahhaf, wakati wa uvamizi wa Wamarekani (2003). Bw. huyu sauti yake ilikua chungu sana plae ilipoingia kwenye masikio ya wamarekani na hata wale waliokua wakiijua hali hali halisi nchini Iraq. Alikua akishangaza wengi kutokana na moyo aliokuwa nao wa kujikaza kiasi kile wakati ambapo serikali yote ilishasambaratika huku nchi ikimiminiwa mabomu kutoka angani mithili ya mvua. Mfano wa sauti yake ni hizi sauti za leo zilizozagaa si ndani ya Zanzibar tu bali hata kwa Wazanzibar waishio nje. Wenyewao wameshazigeuza jina na kuzipa hadhi ya ‘dripu’ maana wao ni wagonjwa wanaoishi kupitia matumaini ya hizo dripu zenywe. Kwa pande zote zilizoingizwa ndani ya mzozo huu kwa maslahi ya hicho kishungu cha nzi kinachopendelea harufu ya uvundo wa donda la siasa ya Zanzibar liendee.

Kama kuna mazungumzo ya kutibu na kueka sawa kwa nini basi kueko na majibizano yasiokuwa na msingi? Watu wa lugha moja, dini moja nchi moja wenye kuungana koo kushindwa kukaa sawa ni kujiingiza kwenye mzozo usiokuwa na tija isipokuwa hasara yake sio tu itaimaliza nyumba ya mwenye kidonda Zanzibar bali itaendelea kuenea hadi kwa jirani mkuu wa pua na mdomo ambae amepewa hadhi kubwa na hata wakakubali kuoleana ili udugu usiishie kuwa ni wa ujirani tu.

Kwa kumalizia ili nisikuchoshe msomaji na najua unamajukumu mengi tungeliwaomba wale wenye kujifananisha na Al-sahhaf, wawaache Wazanzibar wafanye shughuli zao hadi hapo ambapo pameahidiwa kutolewa tamko la pamoja la hao madaktari waliojifungia kutibu donda. Kuendelea kupayuka na kuleta majibizano ni kuendelea kuwauumiza na kuwanyong’onyesha kujihisi wanyonge na wapweke pasipo msingi wowote. Waachieni Wazanzibar wavute subra kwao ‘subira huvuta kheri’ ni waja wa subira ila subira ina mipaka yake.

Share: