Habari

Siasa za Magufuli hazipo popote duniani labda Burundi, Ruwanda na Uganda

Mwandishi wetu
Alhamisi, Agusti 10, 2017

ASTAAGH’AFIRU-LLAH, Ewe Molla wetu mtukufu, tunakuomba utusamehe makose yetu kwa kauli na kwa vitendo vyetu. Lakini, imenibidi kusema kwamba, Waafrika wapo duniani kwa bahati mbaya. Hawakustahiki kuwepo.

Watu wa mabara yote matano ya dunia: Africa, Australia, America, Asia na Europe. Afrika ndilo Bara pekee linalozungumzwa kwa mifano mibaya. Likitajwa, lazima watu wagune.

Hata kwa Muafrika mwenyewe, huona bara lake ni kituko, huona si eneo sahihi binadamu kuishi. Baadhi ya watu hufika kutoa kauli za kukufuru na kusema: “Bora kama ningezaliwa mbwa Ulaya, kuliko binadamu Afrika.”

Mtu analazimika kusema hivyo, kutokana na ubaya wa viongozi wa Afrika. Viongozi wa Kiafrika, hawajali kuwatesa hata kuwauwa raia wao kwa sababu ya madaraka.

Kwa mfano, Watanzania wakiwa nje ya nchi yao, kuna wakati mwingine wanasikika wakisema: “Vipi wewe unakuwa kama Mwafrika au ama kweli wewe Mwafrika.” Ilhali mwenyewe ni Mwafrika, pengine baba yake au jamaa yake ndiyo Rais wa Tanzania.

Waafrika wanadharaulika, wanaonekana kama wanyama kutokana na hulka za watawala wa nchi zao kuwa mbaya. Dharau hii haitaondoka iwapo watawala wenyewe ni namna ya Magufuli!.

Hili imesababishwa na viongozi (watawala) wake, kutokana na kuwa na tabia za ovyo wanapokuwa ndani ya madaraka. Raia wa kawaida, hawalaumiki kwa sababu wao ni sawa na ng’ombe waliyovishwa ujamu, jukumu lao nikufuata tu.

Kiongozi wa Kiafrika, anapoingia katika madaraka badala ya kutumia sheria na katiba ya nchi, huona hazimsaidii wala hazina maana katika utawala wake, badala yake hutumia amri na vitisho. Kinywa chake ndiyo kila kitu, ndiyo sheria,ndiyo katiba, ndiyo kanuni.

Baadhi ya viongozi wengine wa Afrika, huingia madarakani kwa kasi ya kutaka kujitajirisha kwa kujilimbikiza mali na rasilimali za Wananchi kutaka zote ziwe zake na familia yake.

Tuangalie mfano wa kichekesho huu. Unapokutana na kiongozi wa Afrika nje ya nchi yake, tuseme kama Japan, China au Ujerumani, mkazungumza kirafiki kuhusu Afrika, ataguna na kuzidharau nchi za Afrika, utadhani yeye hakutoka huko au si kiongozi wa moja ya nchi za Afrika.

Kiongozi wa Afrika, anaingia katika madaraka anazitupilia mbali katiba na sheria za nchi. Na papo hapo, anaanza kuimarisha mifumo ya utawala kwa misingi ya kidikteta.

Tatizo, viongozi wengi wa Afrika, hawapendi kuiga mifumo mizuri ya kiutawala iliyopo katika nchi zilizoendelea, kwa kuwa hawatafanikiwa kupata matlaba yao.

Kufanya hivyo, wanahisi hawatafaidi utamu wa mdaraka. Viongozi wa Afrika, madaraka wameyaweka mbele kuliko maendeleo kwa raia wao. Wanadhani watazikwa na madaraka yao.

Na hilo, ndilo linalodumaza katika maendeleo ya demokrasia, utawala bora unaofuata sheria na maadili kwa mihimili yote mikubwa ya nchi. Kiongozi wa nchi anafanya mambo ya ovyo. Bunge linafanya mambo ya ovyo. Mahakama zinafanya mambo ya ovyo na kushangaza.

Taasisi za umma katika baadhi ya nchi za Afrika, hata zile zinazotakiwa kulinda sheria za nchi, hazifanyi hivyo, zinakiuka sheria. Taasisi za utawala na ulinzi, zinafuata amri na kuvunja sheria na katiba ya nchi. Zinawaonea raia, bila makosa au sababu za msingi.

Nanukuu: Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara ya 3(1) ambayo inatamka wazi wazi kuwa Tanzania, itakuwa na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Rais Magufuli, anaivunja ibara hiyo.

Kifungu hicho hicho, kinaeleza kuwa vyama hivyo vinatakiwa kufanya shughuli zake za siasa vikiwa huru bila kuingiliwa na chombo chochote. Rais Magufuli, anatumia Jeshi la Polisi, kuzuia upinzani kufanya shughuli za siasa.

Sasa kama katiba ya nchi inatamka hivyo, ni kwa nini Rais Magufuli anazua vyama vya siasa visifanye shughuli zake, ikiwamo mikutano ya hadhara na ya ndani na shughuli nyingine zinazoashiria kuwa za kisiasa.

Katiba ya nchi inaposema vyama vya siasa, maana yake inakusudia kuwepo kwa upinzani wa kisiasa. Katiba inasema wazi juu ya uwepo wa vyama vya siasa na shughuli zake. Kwa Serikali ya Rais John Magufuli, upinzani wa kisiasa ni kama uasi na uadui.

Nanukuu tena: Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 18(1) ambayo inatamka kuwa kila raia atakuwa huru kutoa maoni yake nje, bila kubugudhiwa na chombo chochote.

Katiba ya nchi inafafanua hivyo. Je, Jeshi la Polisi linapata wapi mamlaka ya kuwakamata watu mara kwa mara kwa madai ya tuhuma za uchochezi. Ki-uhalisia raia wanatekeleza kikatiba, haki yao ya kutoa maoni.

Lakini, wakati huo huo, Rais Magufuli na chama chake cha CCM wanaendelea kufanya mikutano nchi nzima bila kubugudhiwa. Polisi, wanailinda mikutano ya CCM.

Rais Magufuli kwa makusudi kabisa anavunja katiba na sheria za nchi na Watanzania wanaoguswa na uonevu huu wajitokeze hadharani kuonyesha hisia zao. Wasisubiri kuomba huruma ya mtu asiyewasikiliza kwani ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa.

Nadhani, Watanzania tu hawajaamua kutafuta njia mbadala ya kudai haki zao zinazovurugwa na watawala kwa maslahi yao na familia zao. ‘We have to stop this brutality by facing the reality.’ Wakili Fatma Karume kasema: “Kinyago unakichonga mwenyewe iweje kikutishe.”

Kiongozi Dikteta, au kwa msemo wa Tundu Lissu: “Dikteta Uchwara” asiechwe kuendeleza ukorofi na ukatili ndani ya nchi ambayo tayari ilishajielekeza katika kujenga demokrasia ya kweli na utawala wa sheria. Japo kwa mwendo wa kusuasua.

Haijawahi kutokea tangu kuundwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 udikteta kama huu unao jichomoza sasa.

Hakuna mantiki yoyote, kuzuia shughuli za kisiasa au kuwadhibiti wapinzani, iwe ndiyo njia ya kujenga maendeleo ya viwanda. Ni unafiki uliyokubuhu na kutafuta sifa kwa wananchi.

Kwa ufupi niseme kwamba, tatizo la Magufuli, hawezi siasa za upinzani, anaziogopa, anachukia sana upinzani. Haiwezekani nchi tangu kujitawala miaka zaidi ya 50, unawarundika magerezani wapinzania bila sababu wala makosa. Anasahau kuwa wapinzani, kazi yao ni siasa.

Magufuli kuna wakati mmoja aliwahi kusema kwamba:  “Nanatamani malaika engeshuka akaifunga mitandao ya kijamii yote angalau kwa miaka mitatu.” Ni kauli yenye taswira za Kidikteta.

Kauli hii aliitowa kwa sababu watu wanaandika maoni yao kuhusu yeyey (Magufuli) na serikali yake, mambo ambayo hataki kuyasikia, hataki kuyaona, akiashiria kuwa hataki kukosolewa.

Maskini, hata hajui kwamba ulimwengu huu wa leo unaendeshwa zaidi na mitandao ya kijamii kuliko hata media. Magufuli, labda anataka Watanzania wote wanaotumia mitandao ya kijamii wamsifu yeye tu. ‘This is 21st Century.’ Hapa kazi tu!!.

Magufuli, hotuba zake hazina mpangilio zinatia hasira/zinaudhi wala si dhani kuwa zinawasaidia wananchi labda wale wenye akili zinazofanana na zake, ‘kutumbua majipu.’

Siku ile alipokuwa anamwapisha Anna Mughwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, alimwambia amempa uwezo (power) ya kumweka mtu ndani kwa saa 48.

Akimuelekeza Mkuu wa Mkoa huyo kwa kutoa mfano, kutumia power hiyo kwa wale watu wanaomsema katika maneno yanayoitwa ya uchochezi.

Kauli hii ilidhihirisha wazi kwamba inawalenga wapinzani moja kwa moja. Huku, lengo la matumizi ya kuwekwa kwa power hiyo ni kwa ajili ya masuala ya usalama wa jamii tu. Si kuhusu masuala ya kisiasa wala wanasiasa.

Mimi nadhani, wanasheria na wanasiasa nchi nzima waanze utaratibu wa kuendesha makongamano ya kisiasa ili kumuelewesha Magufuli, kuwa upinzani upo nchini kwa mujibu wa sheria.

Hii itasaidia kumpunguzia munkari katika akili yake kufikiri kuwa alitakalo yeye ndiyo sheria au yeye ndiyo sheria. Hata kama ni kinyume cha kanuni, katiba na sheria za nchi.

Aidha, nataka niseme tena kitu kimoja, CCM ni kati ya vyama vichache vikongwe vya ukombozi vilivyosalia Barani Afrika, hivyo 2020, ndiyo iwe kikomo kuendelea kutawala watu kibabe.

Gazeti la Mwananchi la juzi Jumanne, tarehe 8/8/2017 liliandika kuhusu Magufuli, jinsi anavyo wafitinisha wabunge wa upinzani kwenye mikutano yake ya hadhara katika mikoa mbali mbali nchini.

MAONI YA WACHAMBUZI
Walipotakiwa kutoa maoni yao kuhusu staili hiyo ya Rais Magufuli, wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini walikuwa na maoni mbalimbali.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, George Shumbusho alisema, “Nilichokiona hapo ni kuwaambia ‘next time’ wasijisahau, japokuwa alitoa nafasi kwa upinzani kuwachukua wanaCCM wanaotaka kwenda huko, lakini sidhani kama watakwenda kwani ukiangalia kwa sasa, upinzani wameshikwa, hawana uwezo wa kufanya siasa kama yeye (Rais Magufuli).”

Mwananchi linaripoti kuwa Rais John Magufuli amewaweka katika mtego wabunge watano wa vyama vya upinzani katika majimbo yao kutokana na kauli za mafumbo alizotumia katika ziara mbalimbali ambazo amekuwa akizifanya.

Mtego unaowakabili ni ama wachague kuhamia CCM au wabakie upinzani lakini wananchi wasiwakubali tena katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2020.

Rais Magufuli ambaye alifanya kazi hiyo ya kichama kupitia ziara za uzinduzi wa miradi mbalimbali ya kiserikali mikoani, alitumia kauli kama “Huyu ingawa ni upinzani lakini damu yake ni CCM.”

Mbali ya kauli hiyo ambayo imewafanya baadhi yao kuonekana kama ni ‘CCM B’, akiwa katika majimbo yanayoshikiliwa na upinzani, kila alipopokea kero kutoka kwa wananchi, Rais Magufuli alichomekea kauli za kuwabeza au kuwataka wananchi wasifanye tena makosa.

Lakini, pamoja na kuchomekea maneno hayo katika ziara zake Rais Magufuli, amekuwa akisisitiza  kuwa yeye ni Rais wa Watanzania wote bila kubagua vyama, dini au makabila yao, akisema maendeleo hayana vyama.

Wabunge walioingizwa mtegoni kwenye majimbo yao ni: Magdalena Sakaya (Kaliua – CUF Lipumba), Kasuku Bilago (Buyungu – CHADEMA), Mussa Mbarouk (Tanga Mjini – CUF) Vedasto Ngombale (Kilwa Kaskazini – CUF) na Saed Kubenea Ubungo – CHADEMA).

Nadhani hadi hapo limefahamika lengo la Magufuli, dhidi ya upinzani. Habari hii iliyojaa fitina za Magufuli, ipo yote katika records zangu, nitairudia tena ikiwa kamili, siku zijazo.

Wakati huo huo, siku hiyo hiyo ya Jumanne, Agusti 8, 2017 Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe aliwaomba Watanzania wamuombee Rais John Magufuli kwa Mungu, ili apunguze ukali wa maneno yake kwani analigawa na kulitia hofu Taifa.

Mbowe, ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mikutano ya hadhara maeneo ya Masama, Mailisita na Bomang’ombe.

“Nimeongea Bomang’ombe nikampelekea Rais salamu na wasaidizi wake wakanipigia wakaniambia tunakusikia Mbowe… Tumia ulimi laini. Acha ulimi wa maneno makali makali tu kila siku,” alisema Mbowe.

“Wanadamu saa nyingine wanahitaji wapewe mapenzi ya viongozi. Sio kila siku kiongozi amekaza tu misuli. Kuna mahali anatakiwa awaambie maneno ya kuwatia faraja.”

“Unajenga taifa lenye upendo sio kujenga taifa la kutishana tu kila saa. Namuomba Rais aelewe unapokuwa Rais, unakuwa mfariji mkuu. Kauli zako zinaweza kulijenga taifa au kuliogofya taifa.”

“Rais wetu tumuombee Mungu ampe uungwana wa kujua kuwa anaowaongoza ni binadamu wenye damu wenye nyama, walio maskini na tajiri. Kauli za mkuu wetu wa nchi zinatukwaza.”

“Yapo mambo mazuri anayofanya lakini yapo mambo mengine anayofanya na kauli ambazo haziashirii kuwa kiongozi mkuu wa taifa ni mfariji. Wewe Rais wa nchi, sawa lakini ruhusu tukukosoe,” alisema Mbowe.

“Sisi tunaamini huwezi kwenda kwenye wahanga (waathirika)  wa tetemeko la ardhi Bukoba, ukawasimanga badala ya kuwapelekea chakula. Huwezi kutoa kauli kuwa wasio na chakula, serikali haigawi chakula wafe. Hizo sio kauli.”

Mbowe alisema: “Tumuombe Mungu amjaze neema amlegeze ulimi. Ulimi unakaza sana nafikiri mnanielewa.”

Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa muungano wa vyama vinne vya upinzani chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) alisema yako mambo mabaya yanayofanyika katika nchi ambayo alisema, wataendelea kuyasema bila ya kuogopa.

“Kwenye nchi zilizoendelea na zinazoheshimu demokrasia, wanaona upinzani kama nyenzo muhimu ya kujenga mshikamano na nguvu ya pamoja ya taifa. Kwa serikali yetu ya CCM wapinzani ni maadui.”

“Kwa mataifa makubwa yaliyoendelea kama Marekani, Uingereza na Ujerumani, wana vyama vingi vya siasa. Ukienda Marekani wana mtu anaitwa (Donald) Trump na Democrat wana (Hilary) Clinton.

“Wamepambana kwenye uchaguzi na uchaguzi umemalizika hakuna anayempiga mwenzie ngumi. Hapa uchaguzi umeisha miaka miwili lakini bado ni visasi tu. Kamata viongozi, wabunge weka ndani,” alisema Mbowe.

Tangu Rais Magufuli apige marufuku mikutano ya vyama vya siasa na maandamano hadi mwaka 2020, viongozi wa upinzani wakiwamo wabunge, wamejikuta katika msuguano na Jeshi la Polisi.

Ingawa Rais aliruhusu wabunge na madiwani kufanya mikutano katika maeneo yao ya uchaguzi, lakini bado baadhi ya viongozi hao wamejikuta matatani wanapofanya mikutano baadhi wakidaiwa kutoa maneno ya uchochezi au kutopata kibali..

 

 

 

Tagsslider
Share: