Habari-Picha

Picha:Eid El Hadj – Zanzibar

9009JPG ////// Baadhi ya askari wa Kikosi cha Polisi cha FFU wakitoa salamu ya heshma ya Gwaride kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein,alipowasili katika viwanja vya Salama Bwawani Hotel,akiwa mgeni rasmi kulihutubia Baraza la EID EL HAJJ Leo.

Salma Said, Zanzibar (Octoba 26-2012)

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein ametoa ametangaza vita dhidi ya watu wenye kuchagua hali ya amani na utulivu akisema serikali yake imefikia ukomo wa uvumilivu.

Kauli hiyo imetolewa jana katika baraza la Eid El Hajj katika ukumbi wa Salama kwenye Hoteli ya Bwawani muda mfupi baada ya kumaliza sala ya Eid iliyosaliwa kitaifa katika msikiti wa Muembeshauri Mjini Unguja.

Akionesha kukerwa na vitendo vya fujo na vurugu vinavyojirudia mara kwa mara katika visiwa vya Zanzibar, Rais alisema polisi pamoja na vyombo vya usalama vimejipanga kukabiliana na hali hiyo pamoja na kuwachukulia hatua kali watu wanaochochea fujo hizo.

“Napenda kukuhakikisheieni nyote kwamba serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti dhidi ya watakaotishia amani ya nchi yetu…jeshi letu la polisi na vyombo vya ulinzi na usalama vipo imara kudhibiti vitendo vya vurugu na fujo” alisema huku akipigiwa makofi katika hafla hiyo.

Alisema serikali yake itatumia sheria na taratibu zilizopo ili kuvishughulikia vitendo vya uvunjaji wa amani vitakavyofanywa au kuchochewa na kikundi chochote visiwani Zanzibar.

Kauli ya Dk Shein imefuatia vurugu za hivi karibuni zilizotokea baada ya kutoweka kwa kiongozi wa taasisi za kiislamu, Sheikh Farid Hadi Ahmed ambaye baadae aliibuka na kusema kwamba alitekwa na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi.

Hata hivyo polisi walikanusha kuhusika na kadhia hiyo na Rais Dk Shein jana alirudia kusema kuwa Sheikh Farid hakutekwa na kuwataka vijana kutojishirikisha katika vitendo vya uvunjifu wa amani.

Tayari Sheikh Farid na wenzake saba wanashitakiwa katika mahakama za wilzaya na mkoa kwa makosa mbali mbali ya uchochezi na uvunjifu wa amani pamoja na kuharibu mali za serikali na watu binafsi. Kesi hiyo inatearajiwa kuendelea Novemba 7 mwaka huu.

Rais alisema ili kufikia malengo ya serikali pamoja na watu binafsi katika katika maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi suala la amani na utulivu linahitaji kupewa kipaumbele hasa wakati huu ambapo serikali inategemea sekta ya utalii.

Akizungumzia kuhusu muelekeo wa uchumi na hali za maisha ya watu, Dk Shein alisisitiza juu ya kufanya kazi kwa bidii na hasa akitoa wito kwa wakulima kujitayarisha kwa ajili ya msimu wa kilimo unaotarajia kuanza mwezi huu.

Alisema serikali imejipanga kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo pamoja na matrekta ya kulimia mapema kabla ya mvua kubwa hazijaanza.

Aidha Rais aliwataka wananchi kutunza mazingira ikiwemo suala la kuacha tabia ya kuchimba mchanga kiholela, kukata miti na kuharibu vianzio vya maji kwani kufanya hivyo ni kuharibu mazingira.

Picha zote kwa hisani ya Salma Said

Tagsslider
Share: