Habari

Siri ya Dola dhidi ya CUF zavuja

Huku wafuatiliaji wa mambo ndani na nje ya Tanzania wakisubiri kwa hamu uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kwenye kesi zilizofunguliwa na Chama cha Wananchi (CUF) dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kwa upande mmoja, na Wakala wa Usajili na Ufilisi (RITA), kwa upande mwengine, kuhusiana na shutuma kadhaa zikiwemo za kughushi nyaraka, kula njama, kukiuka taratibu na hata wizi wa fedha, imefahamika kuwa kuna shinikizo kubwa kutoka serikalini likimtaka Mwanasheria Mkuu George Masaju kuingilia kati.

Kwa mujibu wa mpasha taarifa wetu, ambaye hakutaka kutajwa jina kwa sababu ya nafasi yake serikalini, uamuzi huo umefikiwa baada ya serikali kugunduwa kuwa nafasi halisi waliyonayo washitakiwa kwenye kesi hizo ni ngumu.

“Serikali ilitaka kujuwa ukweli wa mambo kuhusu kesi hizo na nafasi ya washitakiwa kutoka salama, lakini ilipoelezwa kuwa ni vigumu, ndipo AG Masaju akaambiwa achukuwe hatua,” kinasema chanzo hicho.

Ingawa kwa kusema “serikali” mtoa habari huyo hakutaka kuelezea anakusudia nini hasa, ila inafahamika kuwa katika jumla ya kesi zilizopo mahakamani, CUF inamshitaki Jaji Francis Mutungi kwenye Shauri Na. 21 la mwaka 2017 kwa kutowa kwake ruzuku ya chama hicho kwa watu wasiostahiki sambamba na lile la kuingilia kwake uhuru wa mahakama ambalo limesajiliwa kama Shauri Na. 50/2017.

Pia katika kesi nyengine dhidi ya RITA, CUF inamshitaki wakala huyo wa usajili kwa kuisajili bodi mpya ya wadhamini kinyume na sheria, huku ikitumia nyaraka za kughushi. Na pia kwenye Shauri Na. 51/2017, CUF inaitaka mahakama kuu kuizuwia bodi hiyo ya RITA.

“Kwenye kesi zote hizi, serikali imeambiwa ukweli kwamba Jaji Mutungi na RITA hawana njia ya kutoka. Hivyo itakuwa aibu kubwa kwa serikali. Ndio maana anatakiwa Masaju kufanya ushawishi wa hali ya juu kubadilisha sura ya mambo,” kinasema chanzo hicho cha habari.

Njia moja ambayo mpasha habari huyo alisema Mwanasheria Mkuu Masaju anatazamiwa kuitumia kwenye kubadili mwelekeo wa kesi hizi, ni kumshinikiza jaji mkuu kiongozi kuingilia kati.

Bado haijafahamika endapo ubadilishaji huo wa mambo utamaanisha kufutwa kwa kesi hizo kwa visingizio vya kiufundi au kuwapa washindi washitakiwa kwa kuwatoa hatiani, lakini inatajwa kuwa muhimili wa mahakama umeendelea kuwa pekee nchini Tanzania unaojaribu kujipambanua dhidi ya kutekwa na muhimili wa utawala.

Kwa kiasi gani muhimili huo utaendelea kudumisha uhuru wake baada ya shinikizo hili, ni jambo la kusubiri na kuona, lakini upinzani nchini Tanzania unaamini kuwa vurugu kubwa iliyomo ndani ya CUF hivi ina mkono wa moja kwa moja wa vyombo vya dola na taasisi nyengine za serikali.

Tangu aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, kujirejesha madarakani kwa msaada wa Jaji Mutungi, CUF, ambayo inadai kushinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 visiwani Zanzibar, imekuwa ikipitia kipindi kigumu sana kwenye historia yake.

Tagsslider
Share: