Habari

Sisi ndio wana sports, Hongerezeni Zanzibar Heroes

MCHEZA KWAO HUTUNZWA, MCHEZA UGENINI JEE?

Kwa niaba ya mzalendo.net sinabudi kutoa shukran zangu za dhati kwenu timu nzima ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) mumeonyesha U-Heroes wenu katika ulimwengu wa soka. Mumetoa funzo kwa kila mpenzi wa soka duniani.

Musidhani mulikuwa mukiangaliwa na Wazanzibar tu, bali dunia nzima ilikuwa iko pamoja nanyi na inakuangalieni. Nipo kazini nimewafungulia jamaa wa Kizungu, Wabrazil, Wahindi, Wa East Europe wote na nimewaonyesha namna munavyolisakata kabumbu. Wengi wamekuwa wakiniuliza hii nchi gani? Nimewambia hiyo ndio Zanzibar, Spice Island within Indian Ocean.

Ujumbe umefika kwa Chama cha Mpira wa Africa CAF kwamba “THIS IS ZANZIBAR, NEVER WALK ALONE”. Wakati umefika wafikirie tena uamuzi wao wa kuirudishia uanachama wake uliofutwa hapo kabla na huu uliofutwa 2017. Tukitumai pia na majirani zetu (aka ndugu zetu) wataunga mguu mara hii, kwa hili. CAF inaweza kutupa hata kwa masharti kwamba tucheze michezo ya ndani ya Bara la Africa tu na sio ya kombe la dunia, si haba.

Ujumbe umefika kwa FIFA nawo kwani kwa vile ni wadau wa michezo na kila nchi inakuwa na mawakala wao, kwamba hii ndio Zanzibar inahitaji hivyohivyo, jicho la huruma. Mimi niko tayari kwa hilo.

Kizuri zaidi ujumbe umefika kwa vijana na watoto wa Kizanzibar kujiona kuwa wao ni Wazazibar wenye vipaji na weledi mkubwa, hivyo ushiriki na ubunifu wa mambo mbalimbali. Vijana na watoto wa Kizanzibar watarithi kutoka kwenu juhudi na ushuja mkubwa muliouonyesha kwenye mashindano haya toka mwanzo hadi mwisho. Ikiwa mulisafiri kwa basi, mulikuwa mukila mikate haina siagi, hamuna matibabu, etc yote muliweza kuvumilia.

Ipi lugha ya kueleza ushujaa wenu zaidi ya kupeperusha bendera ya nchi yenu nje ya mipaka licha ya wachache kukupigeni vita kuwa hamuna mipaka yenu. Kupigiwa wimbo wa Taifa la nchi yenu licha ya wachache kudharau asilini yenu. Huu ndio ushujaa wa kupigania nchi yenu.

Mwisho furaha ndani ya nyoyo za Wazanzibar kwasababu yenu tu kitimu cha watu hata 30 hamuzidi, leo nyoyo za Wazanzibar zimesabilia mapenzi yao kwenu.

Hongera Zanzibar Heroes
Hongera Zanzibar
Hongera Wazanzibar

ZANZIBAR NDIO KWETU HATUNA PENGINE PAKWENDA

Tagsslider
Share: