Habari

‘Sitta ahadaa Watanzania’

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta

na Shehe Semtawa 17/07/2014

‘Sitta ahadaa Watanzania’IMEELEZWA kuwa kitendo cha Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta kuunda Kamati ya Maridhiano ni cha kuwahadaa Watanzania.

Hayo yameelezwa jana na Mwinjilisti wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Mbagala, Temeke jijini Dar es Salaam, Medadi Kyabashasa.

Alibainisha kuwa kitendo hicho ni kutaka kuwafanya wajumbe wanaopigania Katiba ya Wananchi (UKAWA), waonekane wakorofi.

Kyabashasa alisema mwenyekiti huyo anafahamu fika kuwa UKAWA hawataweza kuhudhuria kwenye kamati hiyo ya maridhiano, kutokana na yeye kuwa sehemu ya mgogoro huo unaoendelea.

Alisema wakati Bunge hilo lilipokuwa likiendelea mjini Dodoma, Sitta alishindwa kuwakemea wajumbe wa CCM wakati walipokuwa wakiwaporomoshea matusi wenzao wa UKAWA.

“Mbaya zaidi, Sitta alikuwa akiunga mkono matusi hayo kwa kusema ‘mheshimiwa muda wako unalindwa, wajumbe tutulie amalizie’,” alisema mwinjilisti huyo.

Alisema kutokana na hali hiyo ya sintofahamu, Sitta anafanya propaganda ili waje waitumie na chama chake kuupotosha umma kuwa UKAWA wamekataa maridhiano.

“Hivi tangu lini mporwaji na mporaji wakakaa pamoja kufikia maridhiano, huu ni ujanja wa CCM kukwepa hoja za msingi,” alisema Kyabashasa.

Alisema kote huko wanakopita CCM ni kutaka kuwapotezea muda Watanzania, kwa sababu chanzo cha mgogoro huo wanakijua.

Aliitaka CCM kuacha kujikita kupoteza muda na ubabaishaji, bali ni vema wakubali kujadili rasimu ya pili ya Jaji Warioba na siyo ile ya kutoka mifukoni mwao, ambayo haikubaliki kwa wananchi.

“Maridhiano hayo ni maridhiano gani? Ni UKAWA wakubali ukiukwaji wa sheria, kanuni na matusi, badala ya kujadili rasimu ya katiba, katika hili hakuna haja ya kupoteza muda wa kuunda Kamati ya Maridhiano, lazima CCM ikubali kujadili maoni ya wananchi,” alisema Kyabashasa.

Aliwatahadharisha wanasiasa, hususani wale wanaotoka CCM kuwa wasipende kuvuruga amani ya nchi kisha kumgeuza Mungu kikaragosi kwa kuwaambia viongozi wa dini waombee amani.

Hivi karibuni, Sitta aliunda Kamati ya Maridhiano yenye wajumbe 30 ili kunusuru mvutano huo, lakini UKAWA wamekaririwa wakidai hawatashiriki katika kamati hiyo.

Chanzo Tanzania Daima

Share: