Habari

SMZ ITAENDELEA KUTHAMINI MISAADA YA MAENDELEO

Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi amesema Zanzibar ni miongoni mwa nchi chache Duniani zinazoendelea kutoa Elimu bila malipo tokea kuasisiwa Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.

Akizungumza katika ufunguzi wa Skuli mpya ya Sekondari ya Mapinduzi, Chaani katika maadhimisho ya sherehe za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Mwinyi amesema mafanikio hayo yanatokana na viongozi shupavu wa Mapinduzi na wale waliofuatia kuongoza Zanzibar.

Amewapongeza viongozi na wananchi wa Zanzibar kwa jumla kwa kuendeleza malengo ya Mapinduzi ya 1964 ya kuimarisha maendeleo katika nyanja mbali mbali.

Rais mstaafu amewahimiza wananchi kuendeleza Umoja kwani bila umoja na mshikamano hakuna maendeleo yatakayopatikana.

Amewashukuru wahisani wanaosaidia maendeleo ya Zanzibar hasa katika nyanja ya elimu na afya na amesema misaada yao itaendelea kuthaminiwa .

Amewataka wazee wa Chaani kuendelea kuwasimamia watoto wao na kuhakikisha wanaitumia skuli hiyo katika kubadilisha uwezo wao wa kusoma kuwa bora zaidi.

Akizungumza katika sherehe hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna amesema baada ya kupata msaada wa skuli mpya 19 za sekondari na Benki ya Dunia na skuli mbili msaada wa BADEA, Wizara yake inatilia mkazo katika kuondosha tatizo la walimu wa sayansi linalokabili Skuli nyingi za Zanzibar.

Amesema Nigeria imewapatia msaada wa walimu 13 wa sayansi na tayari wamefanya mazungumzo na nchi ya Marekani, Uingereza, Ghana, India, Palestina, Misri na Oman na wote wameonyesha azma ya kusaidia kupunguza tatizo hilo.

Ameongeza kuwa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) kwa kuliona tatizo la walimu wa sayansi, kimeanzisha Skuli ya Sekondari ya sayansi na Chuo cha Ufundi Karume kimeimarisha somo la hesabu na ameeleza matarajio yake kwamba baada ya miaka mitatu tatizo hilo litapungua.

Waziri Shamhuna ameahidi Wizara yake itawaajiri wahitimu wote wa digrii ya sayansi na kuwapa mafunzo ya ziada walimu wa sayansi ambao wameajiriwa ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Skuli ya Sekondari ya Mapinduzi, Chaani imegharimu shilingi bilioni 1.32 na imejengwa na kampuni ya China Railway Jian Chang Engineering Co. LTD ya China

Share: