Habari

SMZ kuanzisha sheria kudhibiti madaktari wanaozamia

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed na Naibu wake, Harusi Said Suleiman (waliovaa ‘gowns’ za hospitali) wakikagua vifaa vya matibabu ya uti wa mgongo na kichwa katika Hospitali ya Mnazimmoja, Zanzibar. Wengine ni Wataalam wa kitengo hicho – Picha na Abdallah Omar wa Maelezo, Zanzibar.

Na Faki Mjaka – Maelezo Zanzibar
Jumanne, Machi 6, 2018

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Hamad Rashid Mohamed amesema serikali inaandaa sheria itakayowalazimisha wafanyakazi wanaopewa fursa za kusomea taaluma ya udaktari nje ya nchi kurudi Zanzibar ili kufanya kazi kizalendo.

Waziri Hamad aliyasema hayo siku ya Jumanne, Machi 6, 2018 kwa nyakati tofauti alipofanya ziara katika Kitengo cha Matibabu ya Uti wa Mgongo na Kichwa kilichopo Hospitali ya Mnazimmoja na Hosptali ya Kivunge, Kaskazini A, Unguja.

Alisema kuna tabia iliyojengeka muda mrefu ya wasomi kupewa nafasi za kusoma nje ya nchi lakini wanapomaliza masomo yao hukataa kurudi nyumbani kufanya kazi.

Alisema hali hiyo huchangia ongezeko la uhaba wa madaktari bingwa katika baadhi ya maradhi na hivyo, kupelekea serikali kupoteza fedha nyingi za kuwahudumia wagonjwa nje ya nchi.

Waziri Hamad alisema kuwa serikali ipo mbioni kuhakikisha kila anayepata fursa za masomo anarudi nyumbani kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Unguja na Pemba.

“Haiwezekani mtu anapewa fusrsa ya kusoma nje ya nchi lakini akimaliza tu anatafuta nchi ya kwenda kufanyakazi…Hiyo siyo haki tunaandaa sheria tuwashitaki wazazi wake au tukamate mali zake” alisema Waziri Hamad.

Aidha, waziri huyo alikemea lugha chafu zinazotolewa na baadhi ya madaktari na wauguzi kwa wagonjwa na kusema kuwa hana muhali kwa wafanyakazi wenye tabia hiyo.

Aliongeza kuwa miongoni mwa mambo yanayomchukiza ni kusikia wananchi wakilalamika kuhusu madaktari na wauguzi wenye tabia ya kutoa lugha chafu kwa wagonjwa huku wakitambua kwamba wagonjwa wanahitaji faraja kwa muda wote.

“Kazi yenu ni nyepesi kukuingizeni Peponi maana munapompa maneno mazuri mgonjwa mnapata thawabu na mnavyomtibu pia mnapata fungu mbele ya Mwenyezi Mungu na kinyume chake ni dhambi” alisema Waziri Hamad.

Aliwahakikishia wafanyakazi wa wizara hiyo mashirikiano ya karibu na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika kufanyakakazi zao.

Miongoni mwa mambo aliyoahidi ni kupigania bajeti ya wafayakazi kwa ajili ya mavazi ya kidaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wa sehemu za utabibu na huduma za hospitali ili waondokane na tabia ya kuvaa nguo za kienyeji wanapokuwa kazini.

“Kama askari wanapatiwa sare za kuvaa kazini kwa nini madaktari, wauguzi na wafanyjazi wengine wasipatiwe…wao wanunue kwa pesa zao?” alihoji na kuongeza. “Hili nawaahidini nitalisimamia na kupata ufumbuzi.”

Awali akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mratibu wa Kitengo cha Matibabu ya Uti wa Mgongo na Kichwa kilichopo Hospitali ya Mnazimmoja, Dk Mohamed Ally alisema tangu kuanzishwa kwa kitengo hicho mwaka 2014, wagonjwa zaidi ya 800 wamefanyiwa matibabu ya upasuaji yakiwemo ya mgongo na vichwa.

Pia, alifahamisha kuwa kutokana na kufanyika kwa matibabu hayo, wamefanikiwa kuokoa zaidi ya dola milioni 20 za Kimarekani, kama wagonjwa hao wangefanyiwa matibabu nje ya nchi.

Hata hivyo, Dk Mohamed aliomba serikali kukiangalia kitengo hicho kwa ukaribu na kukifanya kuwa taasisi kamili inayojitegema ili kwenda sambamba na mabadiliko ya wagonjwa na utaalamu.

Share: