Habari

SMZ yabomoa nyumba 16 Tunguu bila kuwafidia wananchi

Chanzo: ZanziNews
Jumanne, Agosti 28, 2018

Jumla ya nyumba 16 za wananchi wa kawaida katika eneo la Tunguu, Unguja zimebomolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kufuatia amri iliyotolewa na Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Kusini.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ni kwamba nyumba hizo za makazi ya wananchi, zimejengwa kinyume na utaratibu.

Taarifa imesema eneo hilo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa shughuli za maendeleo na miradi ya serikali pamoja upanuzi wa majengo ya chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA).

Akizungumza Jumanne, Agosti 28, 2018 alipokuwa akisimamia kuvunjwa kwa nyumba hizo Mkuu wa Mkoa huo, Hassan Khatib Hassan amesema ofisi yake ya serikali mkoa imeamua kuchukua hatua hiyo kutokana na wananchi wanaomiliki nyumba hizo kushindwa kutii maelekezo ya serikali waliyopewa miezi mitatu iliyopita.

Mkuu wa Mkoa amesema serikali yake iliwataka wananchi na wakazi wa eneo hilo kuzivunja nyumba zao na kuhama katika eneo hilo ili kupisha serikali kuendelea na zoezi la usafishaji kwa ajili ya matumizi yaliokusudiwa.

Lakini, baadhi ya wananchi na wakazi wa nyumba hizo ambao wamekumbwa na janga hilo, wamelalamika na kusikitishwa na hatua hiyo, kwamba wamekuwa wakiishi kwenye eneo hilo kwa muda wa takriban miaka 45.

Wamesema hatua hiyo iliyochukuliwa na serikali ya kubomolewa kwa nyumba zao imewapa wakati mgumu kwa kuwa, kwa sasa hawana sehemu nyengine ya kwenda kuishi na watoto wao.

Wakazi hao, pia wamelalamika kuwa, kwa sasa hawana uwezo wa kumudu gharama ya ujenzi wa makazi mapya kutokana na kukabiliwa na hali ngumu ya maisha na umasikini.

Hata hivyo, wakizungumza kwa huzuni na masikitiko, wananchi hao wameiomba serikali kuu ya SMZ kuangalia uwezakano kwa jicho la huruma na utu kuweza kuwapatia fidia itakayowezesha kuanza maisha mapya pamoja na kupata shehemu nyingine ya kujihifadhi na watoto wao.

Naye, Kaimu Makamu Mkuu wa SUZA, Haji Mwevura amesema ni vyema kwa wananchi kuhakikisha kwamba wanafuata taratibu za uhaulishaji wa ardhi kabla ya kuuziwa/kununua maeneo ili kuepuka matatizo yanayoweza kuwakumba.

Tagsslider
Share: