Habari

SMZ yatoa onyo kali kwa wataomfuata Maalim Seif

SERIKALI ya Mapinduziya Zanzibar (SMZ) imesema haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wafanyabiashara wanaojipanga kugoma kulipa kodi kama kutekeleza kampeni ya Chama cha Wananchi (CUF) ya kutomtambua Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein na serikali yake.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud, mjini hapa jana baada ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuwataka wanachama na wafuasi wake kutomtambua Rais Dk. Shein na viongozi wake pamoja na kutolipa kodi na kufanya migomo.

“Serikali haitasita kufunga biashara kwa kumnyang’anya leseni na kupigwa faini mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutolipa kodi kwa sababu kitendo hicho kinyume na mashariti ya leseni yake ya biashara,” alionya Waziri Aboud.

Alisema SMZ haitavumilia mgomo wa aina yoyote katika utoaji wa huduma kwa jamii na watu watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria na vyombo vya dola.

Alisema uchaguzi wa Zanzibar umemalizika kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na Rais wa Zanzibar Dk. Shein ni Rais halali.

Waziri Aboud alisema Rais wa Zanzibar amechaguliwa na wananchi na ataendelea kuwapo madarakani kwa miaka mitano kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.

Alisema serikali imeanza kufuatilia kwa karibu nyendo za wafanyabiashara wanaotoa huduma kwa ubaguzi wa itikadi za kisiasa katika maduka au huduma nyingine kabla ya kwa kushirikiana na wakuu wa wilaya, mkoa na watendaji wa serikali kabla ya kuwafutia leseni zao.

Waziri Aboud alisema Zanzibar ni nchi inayoongozwa kwa kufuata misingi ya utawala wa sheria na haiwezekani wananchi kubaguliwa wakati vitendo hivyo ni kinyume cha misingi ya haki za binadamu.

Katika hatua nyingine, Chama Cha Mapinduzi Zanzibar (CCM), kimesema hakuna mabadiliko ya utawala yatakayotokea Zanzibar mpaka mwaka 2020 kinyume cha inavyodaiwa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif. Kauli hiyo imetolewa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.

Aliyasema hayo akijibu kauli ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, aliyesema Serikali ya Rais Dk. Shein haitafika mbali kutokana na vikwazo vya kiuchumi vinavyoendelea kuwekwa na wahisani pamoja na msimamo wa chama chake wa kuwataka wananchi kutoitambua pamoja na kuwataka kugoma kulipa kodi na kufanya migomo ya kutoa huduma.

Vuai alisema kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, uchaguzi mMkuuwa Zanzibar umemalizika na serikali tayari imeundwa na hakuna mamlaka yoyote yenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kiutawala kabla ya Rais wa Zanzibar kumaliza muda wake wa uongozi wa miaka mitano.

“Hakuna mabadiliko ya utawala yanayoweza kutokea Zanzibar mpaka mwaka 2020, serikali imeundwa na viongozi wa serikali wamepatikana yanayozungumzwa mbwembwe za kisiasa na siyo mambo mageni kwa Maalim Seif,” alisema Vuai.

Alisema kuwa msimamo wa CUF wa kutomtabua Rais wa Zanzibar pamoja na viongozi wake, sawa na kupoteza muda wakati huduma zote za jamii kwa wananchi zikitolewa na serikali bila ya kujali itikadi ya vyama vya siasa.

Alisema msimamo wa CUF wa kutoitambua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wabunge wake wakiendelea kushirikiana na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, inaitambua Zanzibar sawa na kuwadanganya wananchi Zanzibar.

Alisema Maalim Seif haikuwa sahihi kumuita Rais wa Zanzibar Rais wa majeshi na dikteta wakati amechaguliwa na wananchi kwa njia halali za kidemokrasia.

Hata hivyo, alisema CCM itaendelea kulinda na kutetea misingi ya umoja wa kitaifa kwa madhumuni ya kuimarisha amani, lakini alieleza kuwa mamlaka yenye dhamana za kusimamia amani na umoja wa kitaifa zinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa vitendo

Nipashe

Share: