Habari

SMZ: Zanzibar imegeuzwa njia ya kusafirishia ‘unga’

NA MWINYI SADALLAH
11th April 2013
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema Zanzibar imegeuzwa kituo cha kuingiza na kusafarisha dawa za kulevya nje ya nchi.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej, wakati akijibu maswali ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwenye kikao chake Chukwani mjini hapa.
Alisema badala ya dawa za kulevya kusafirishwa kutoka nje kuingizwa Zanzibar, badala yake zimekuwa zikitoka Zanzibar kwenda nje ya nchi.
Hata hivyo, alisema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwamo kuwakamata watu kadhaa na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria.
Aidha, Waziri Fatma Ferej, alifafanua kuwa biashara ya dawa za kulevya hufanyika kwa usiri mkubwa.
Alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuchukua juhudi mbalimbali za kupambana na tatizo hilo.
“Serikali inazo taarifa kuwa Zanzibar imegeuzwa kuwa kituo cha kupitisha na kusafirisha dawa za kulevya nje ya nchi, kuna watu wamekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar,” alisema Fatma Ferej.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa watumiaji wa dawa za kulevya ndiyo wanaongoza kwa maambukizi ya Ukimwi, hasa wanaotumia njia za kujidunga sindano.
Alisema idadi ya watu wanaoishi na VVU imekuwa ikiongezeka kutoka watu 5,935 hadi 6,793 mwaka 2012/2013.
“Mheshimiwa Spika, ni kweli dawa za kulevya ni chanzo za vijana wengi kuathirika na Virusi vya Ukimwi, na mpango wa kuwafichua wauza unga na wasafirishaji kutoka ndani na nje ya nchi, upo kisheria,” alisema.
Hata hivyo, alisema utaratibu wa kuitisha kura ya maoni ya wauza dawa za kulevya, unaweza kutumika ingawa utekelezaji wake si rahisi kwa kuwa zoezi hilo linahitaji gharama kubwa kabla wananchi wote kushiriki kupiga kura.
Alisema Sheria ya Kuzuia Usafirishaji na Matumizi ya Dawa za Kulevya namba 9 ya mwaka 2009, imeweka mpango mzuri wa kuwafichua watu wanaofanya biashara hiyo na mtu yeyote atakayetoa taarifa atazawadiwa.
Machi 16, mwaka huu, kitengo cha kuzuia dawa za kulevya Zanzibar, kilifanikiwa kumkamata Alex Vasileios (24), raia wa Ugiriki, akiwa na kilo tano za dawa za kulevya katika begi akisafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kwenda nchini Italia.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani pamoja na Yusuph Abeid, mkazi wa Zanzibar na kusomewa mashitaka ya kuingiza dawa za kulevya na kusafirisha kinyume na Sheria za Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE
Share: