Habari

SUK yaombwa kutonyanyasa wafanya biashara

Salma Said, Mwananchi

ZANZIBAR: Wajumbe wabaraza la Wawakili Zanzibar wameiomba serikali na viongozi wake kutowanyanyasa wafanyabiashara kwa kuwanyanganya mali zao kupitia baraza la manispaa katika maeneo ya Darajani.

Ushauri huo umetolewa jana na baadhi ya wajumbe waliokuwa wakichangia Mswada wa kuanzishwa Mahakama ya biashara Zanzibar uliowasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari katika kikao cha baraza hilo kinachoendelea Chukwani Mjini Zanzibar.

Akichangia mswada huo Mwakilishi wa Jimbo la Micheweni (CUF) Subeti Khamisi Faki alisema ni jambo la kushangaza baadhi ya viongozi wanavyochukua sheria mikononi mwao na kuwanyanganya wafanyabiashara mali zao pamoja na kuwanyanyasa hasa katika maeneo ya Darajani ambapo wafanyabiashara hao wahawa maeneo mengine ya kwenda kuwa kuwa serikali imeshindwa kuwatengena maeneo maalumu ya kufanyia biashara.

Alisema kwa kuanzisha mahakama hiyo itasaidia kwa kuweka usawa baina ya viongozi na mwananchi wa kawaida katika usawa na wafanyabiashara wataweza kufanya biashara zao bila ya kubughudhiwa katika maeneo wanayopangiwa kufanya shughuli zao.

“Sisi viongozi ndio tunaoanza kuchukua sheria mkononi kwa wafanyabiashara wanajiondolea umasikini lakini wanapouza biashara zao sisi viongozi ndio tunaokwenda pale wananyanganya vitu vyao sasa kuanzisha kwa Mahakama hiyo itasaidia tuwe na utaratibu wa kutowanyanganya raia mali zao” Alisema Faki

Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni (CCM) Salmin Awadh Salmin alisema dhana ya kuanzishwa Mahama ya biashara ni zuri lakini tatizo liliopo kunakuwa na msongamano mkubwa wa kuzisikiliza kesi kama inavyojionesha katika Mahakama ya Ardhi.

Alisema Mahakama hiyo iwe muda wa kuzisikiliza kesi kwani katika Mahakama zilizopo zimezoea kuziweka kesi kwa uda mrefu, hali ambayo inakata matumaini kwa mlalamikaji kupata haki yake na hivgo wananchi wanakata tamaa na wanapofikwa na matatizo wanashindwa kwenda mahakamani.

Mwakilishi wa nafasi za wanawake (CCM) Asha Bakari makame yeye alipendeleza kwamba vyombo vya habari vishirikishwe kutoa elimu kwa wananchi ili wananyabiashara wazijue sheria kwanza kaba ya kutungwa sheria kwani kufanya hivyo kutasaidia wananchi kujua haki zao na wajibu.

Alisema katika kifungu No 17 kinasema kesi zote zitashughulikiwa ndani ya miezi kumi hazitozidi mwaka na bila ya kutumia vyombo vya habari kuwaelimisha wananchi bado kutakuwa na msongamo wa kesi kama Mahakima ya Ardhi ambayo imekuwa ikirundika kesi nyingi bila ya kuzipatia ufumbuzi.

Mwakilishi huyo alisema katika Mahakama ya Ardhi kuna kesi 300 na baadhi ya walalamikaji wameshafariki bila ya kupata haki zao jambo ambalo linatokana na wananchi kutofahamu sheria hivyo ipo haja ya kuwapa mwamko wakuijua sharia inayohusiana na shughuli anayoifanya.

Aidha baadhi ya wajumbe waliochangia mswada huo walipendekeza baadhi ya vifungo vingi kufanyiwa marekebisho kwa kuwa havijafahamika kutona na lugha iliondikwa haipo katika Kiswahili chepesi ambacho wawakilishi ni vigumu kuvifahamu.

Walipendekeza mswada huo kuandikwa katika lugha nyepesi ili wawakilishi wate waufahamu ndipo wataweza kuupitisha na kuwa Sheria itayoweza kuwasaidia wafanyabiashara wa Zanzibar.

Pia wajumbe hao walitaka kueleweshwa biashara gani itakayohusika na Mahakama hiyo kwani pia kuna biashara ya kuuza nyumba, kuwekeana ubia na mambo mengi lazima Mswada huo ufafanuliwe kwa kuanisha wazi bidhaa zitakazo husika na Mahakama hiyo.

Tagsslider
Share: