Habari

Sura mbili ziara za Lissu nje

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu

Chanzo Gazeti la Mwananchi
Jumapili, Februari 10, 2019

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameibua gumzo kwa takriban wiki mbili kutokana na mahojiano anayofanya na vyombo vya habari vya mataifa makubwa, na sasa wasomi wanasema ziara zake zinaweza kuibua sura mbili kiuchumi na Uchaguzi Mkuu ujao.

Katika muda wa takriban mwezi mmoja, mnadhimu huyo wa kambi ya upinzani bungeni ameshatembelea nchi za Uingereza, Ujerumani na Marekani.

Lissu, akifanya mahojiano na vituo vikubwa vya habari vya Deutsche Welle (DW), Shirika la Habari la Uingereza (BBC) na Sauti ya Amerika (Voa) lakini pia na Chuo Kikuu cha Mambo ya Kimataifa cha Elliot nchini Marekani.

Katika mahojiano yote, Lissu amejikita katika kujenga hoja kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu akitumia matukio kama shambulio la risasi dhidi yake lililofanyika Dodoma Septemba 7, 2017 kwa madai kuwa serikali haijajishughulisha ipasavyo kuwakamata waliomshambulia au kuwahoji walioondoa kamera za usalama au walinzi eneo hilo kabla ya tukio.

Pia amekuwa akizungumzia kuminywa kwa demokrasia kama uhuru wa kujieleza kutokana na vyama vya siasa kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara na wakati mwingine hata ya ndani, kutoweka kwa baadhi ya watu akiwemo mwandishi wa habari, vyombo vya habari kufungiwa na kwamba wanaonekana kuikosoa serikali kufunguliwa kesi.

Hoja zake zimewafanya viongozi wa Serikali kujitokeza kukanusha, wakiwemo mabalozi wawili (Ujerumani na Marekani), huku kauli zake kuhusu bunge zikimlazimisha Spika Job Ndugai kutolea ufafanuzi.

Wasomi waliohojiwa na Gazeti la Mwananchi wanaona ziara na mahojiano hayo yatakuwa na athari katika siasa za Tanzania, hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020 na uwezekano wa mataifa makubwa kufanya uamuzi mgumu dhidi ya Tanzania.

“Mpaka sasa athari za ziara ya Lissu zimeshaanza kuonekana, kwa kuwa mjadala ni mkubwa. Ndani ya CCM kwenyewe wanajadiliana na wa wapinzani pia kuna mjadala. Hiyo ni impact,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Paul Luisulie alipoulizwa kuhusu ziara hizo.

“Kwa upande wa CCM tunajua Rais Magufuli yupo, lakini kwa upinzani Lissu alishasema atagombea, Hata kama hawakuwa na mpango wa kumpitisha, lazima atakuwa na ushawishi mkubwa.”

Hata hivyo, Lissu amesema uamuzi wa kugombea urais uko mikononi mwa chama chake cha Chadema, akisema atagombea iwapo wataona anafaa.

Na Dk Luisulie anasema Lissu ndiye aliye na nafasi kubwa. “Lissu ameshapata huruma kubwa ya wananchi. Matusi mengi anayotukanwa yanamjenga.”

“Tumesikia Spika akisema watakatisha mshahara wake, huko nako ni kumjenga maana watu wanajadili mshahara huo. Yaani hatapata taabu kupigiwa kura kwa kuwa ameshajijenga wakati huu,” alisema Dk Luisulie.

Dk Luisulie alisema tayari mitaani watu, hasa vijana wameshaanza kuvutiwa na ujasiri wa Lissu wa kutokata tamaa.

“Wengine wanataka kujenga brand (chapa) kama Lissu. Wengine watataka kuongea Kiingereza kama Lissu, wengine watatamani kusoma sheria na wengine watataka kuwa na ujasiri kama huo,” alisema Luisulie.

Msomi mwingine kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mohamed Bakari ameangalia zaidi kauli zake.

“Maneno yake yameshaanza kuwapata hata waliomshambulia. Huko waliko wanaweza kuyajutia. Watu wanajiuliza inakuwaje mtu ashambuliwe akiwa karibu na Bunge Dodoma? Ni suala lililolitia doa Taifa na hasa ikizingatiwa hakuna uchunguzi uliofanyika,” alisema Profesa Bakari.

Profesa Bakari alisema Serikali inapata wakati mgumu, “kwa kuwa utawala bora umeyumba. Ni kipindi ambacho wapinzani watapata sympathy (huruma)”.

Alisema kuwa ziara hizo zinaliweka Taifa katika wakati mgumu kiuchumi kwa kuwa zinafanyika katika nchi zinazotoa misaada kwa Taifa.

Kati ya nchi alizotembelea, Uingereza ndiyo nchi pekee kati ya wafadhili wakubwa wa Tanzania. Nchi nyingine zinazoisaidia Tanzania ni za Scandinavia, Uholanzi na Japan.

Hata hivyo, Marekani na Ujerumani zinasaidia shughuli nyingine za maendeleo zilizo nje ya bajeti.

“Kwa hiyo nchi inaweza kukosa misaada kwa kuwa wanatumia kigezo cha utawala bora,” alisema Profesa Bakari.

Mtu mwingine aliyehojiwa na Gazeti la Mwananchi, Njelu Kasaka alimtetea Lissu kuwa hachafui nchi.

“Sijui woga wa viongozi wa Tanzania unatoka wapi? Mambo mengine wangekaa kimya tu, yaishe. Kama ameongea ukweli itajulikana kama ni uongo pia itajulikana. Huu woga ni dalili kwamba anayosema ni ya kweli,” alisema Kasaka.

Pamoja na ziara hizo, Lissu yuko nchini Ubelgiji ambako alipelekwa kumalizia matibabu akitokea Hospitali ya Nairobi nchini Kenya.

Lissu alishambuliwa kwa takriban risasi 30 akiwa ndani ya gari, nje ya nyumba yake Area D mjini Dodoma. Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyo usiku akahamishiwa Nairobi ambako alifanyiwa operesheni kadhaa.

Mahojiano ya DW yalisababisha balozi wa Tanzania, Dk Abdallah Possi kutoa taarifa ya kurasa mbili kujibu tuhuma zake na baadaye, akiwa Marekani, Balozi Willson Masilingi alipambana naye katika kipindi cha Straight Talk Afrika cha VOA.

Akiwa katika ziara hizo, pia aliwahi kumtuhumu Spika Ndugai kuwa alikuwa na mpango wa kumvua ubunge na kwamba Bunge halijagharimia matibabu yake, jambo lililomfanya kiongozi huyo wa mhimili wa nchi kutoa taarifa ya malipo ambayo ofisi yake imekuwa ikimlipa tangu ajeruhiwe.

Share: