Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kinatoa pole kwa wananchi wote waliopatwa na maafa yaliyotokana na upepo mkali uliotokea mapema leo katika maeneo mbali mbali ya visiwa vya Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa tulizozipokea katika ofisi zetu za Makao Makuu, upepo huo umeathiri zaidi maeneo ya kisiwa cha Unguja katika mitaa ya Nyarugusu na Kinuni kwa kisiwa cha Unguja.

Taarifa hizo tulizozikusanya zinaonesha kuwa zaidi ya nyumba mia tatu (300), zinazotumiwa kwa makaazi ya wananchi, zimeathiriwa vibaya kwa kuangukiwa na miti na kubomoka kuta zake na nyengine kuezuliwa mapaa yake.

Aidha, miundo mbinu ya umeme hasa nguzo na nyaya za umeme zinazotumika kwa ajili ya kusafirishia na kusambazia nishati hiyo zimeharibika kwa nguzo kuanguka na nyaya zenye moto kusambaa ovyo katika maeneo yaliyokumbwa na kadhia hiyo.

Ili kukabiliana na hali iliyopo, The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kinatamka yafuatayo:

1. Viongozi wote wa CUF katika maeneo yote yaliyofikwa na maafa waongoze wanachama wa maeneo yao kwa lengo la kuratibu mpango wa kutoa usaidizi wa dharura na wa haraka, bila ya kujali tafauti yoyote baina ya wananchi, kwa wahanga wote wa maafa ya upepo kama ilivyo kawaida ya Chama chetu kila tunapokabiliwa na hali kama hii.

2. Kwa kuwa nchi yetu imekosa uongozi halali wa serikali, na kile kikundi kidogo kilichojiweka madarakani bila ya ridhaa ya wananchi kuonekana kwamba hakina nia ya kuwasaidia wananchi kutokana na maafa yanayowakumba, CUF inazitaka Mamlaka zenye jukumu la kuhakikisha usalama wa raia, kutekeleza wajibu wake kikamilifu. Ni wajibu wa Mamlaka hizo, hasa Shirika la Umeme Zanzibar, ZECO kuhakikisha kuwa miundo mbinu ya shirika hilo, hasa nguzo na nyaya za umeme zenye moto zilizoathirika kwa upepo zinadhibitiwa kitaalamu ili kuepusha athari zaidi kwa wananchi wa maeneo yaliyokumbwa na maafa.

Baada ya kukamilika kwa ukusanyaji wa taarifa kamili, The Civic United Front (CUF-Chama Cha Wananchi) kitatoa tamko rasmi kwa kubainisha athari zote na hasara iliyotokana na maafa yaliyoikumba nchi yetu.

HAKI SAWA KWA WOTE

HAMAD MASOUD HAMAD
MSEMAJI WA CUF-OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS

FB

Share: