Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI ILIYOTOLEWA NA CHAMA CHA WANANCHI CUF PEMBA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI ILIYOTOLEWA NA CHAMA CHA WANANCHI CUF PEMBA LEO TAREHE 26/02/2018 KATIKA OFISI YA CUF JIMBO LA ZIWANI CHAKE CHAKE PEMBA.

Waheshimiwa wana habari,

Kama tujuavyo kwamba Lipumba alijiuzulu mwenyewe uenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF toka mwaka 2015 na kutangazia uma kupitia vyombo kadhaa vya habari na wala hakujiuzulu siri na hivyo kuanzia kipindi hicho Lipumba hakuwa Mwenyekiti tena wa CUF.

Waheshimiwa wana habari,

Lipumba alikaa nje ya chama kama Mwenyekiti kwa kipindi cha miezi kumi (10) na Chama kikaweka Kaimu Mwenyekiti ambaye ni Mh. Taslima ili atekeleze majukumu ya chama kama katiba ya CUF inavyoelekeza. Wakati chama kinajipanga kufanya Mkutano Mkuu wa dharura ili kufanya uchaguzi wa kumpata mwenyekiti, Lipumba alijitangaza kwamba yeye eti amerudi kwenye nafasi yake ya uenyekiti jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya Chama. Na hapo aliamua kufanya vurugu kwenye mikutano kadhaa ya chama hasa iliyofanyika Dar-es-Salaam kwa kushirikiana na makundi ya wahuni na dola na hatimae chama kupitia vikao vya Baraza Kuu tukamfukuza uanachama.

Waheshimiwa wana habari,

Hivyo kwa sasa Lipumba sio tu kwamba si mwenyekiti bali pia si mwanachama wa CUF.

KWANINI LIPUMBA KAJA PEMBA.

Waheshimiwa wana habari,

Pia ikumbukwe kwamba wapo viongozi walioasi hapa Pemba baada ya wananchi kupitia majimbo yao kuwakataa katika nafasi za Ubunge na baada ya kufanya uasi chama kiliamua kuwafukuza na ni hasa baada ya kushirikiana na Lipumba kukihujumu chama.

Viongozi walioasi ni:-
1. Mussa haji Kombo
2. Haroub
3. Khalifa Suleiman Khalifa
4. Rukia Kassim Ahmed

Hivyo waasi hawa kwa kushirikiana na CCM na Serikali yake na Dola ndio waliamua kumleta lipumba Pemba ili iwe muendelezo wa kuhujumu CUF. Sisi viongozi wa chama Wilaya na Majimbo ya Pemba, Wabunge wote wa CUF, Wawakilishi na Madiwani tunasema, CUF ipo imara sana na ipo ngangari na itaendelea kuwa ngangari na tunawahakikishia wana CUF na wananchi wote kwamba CUF haitoyumbishwa na Vibwetere na wasaliti hawa wachache sana. Na tunawaambai wasaliti hawa kwamba wasishindane na Katibu Mkuu Maalim Seif, hawamuwezi na hawatomuweza kabisa. Pia watambue stahiki anazopatiwa Maalim Seif zipo kwa mujibu wa katiba. Hivyo tunamuambia Mussa Haji atafute hoja na propaganda nyengine hii haina nafasi tena.

MKUTANO WA LIPUMBA

Waheshimiwa wana habari,

Mkutano wa Lipumba ulifanyika kwenye ukumbi wa serikali makonyo, ulihudhuriwa na watu 169 na kati ya waliohudhuria watu 9 tuliwatuma sisi CUF ili kurikodi kila kitakachofanyika, watu waliobaki wote ni wana CCM walioandaliwa na viongozi wa CCM hasa kutoka Mkoa wa Kusini Pemba. Na pia mna paswa kujua kwamba magari yaliyowabeba wafuasi hao wa CCM yalikuwa ya wana CCM hasa ya Gerei Mwakilishi haramu asiyekuwa na ridhaa ya wananchi wa Jimbo la Wawi.

Waheshimiwa wana habari,

Munapaswa kujua kwamba mkutano wa Lipumba licha ya kufanyika kwenye ukumbi wa CCM pia ulirushwa live na Idara ya Habari Maelezo inayomilikiwa na CCM na serikali yake. Hii inadhihirisha wazi kwamba Lipumba ni CCM na ni wakala wa CCM.

Waheshimiwa wana nhabari,

Hivyo Lipumba ni CCM na ni sehemu ya CCM, ni wakala wa CCM na anatumiwa na kuitumikia CCM. Na ziara yake ya Pemba pia imedhaminiwa na kuratibiwa na CCM. Tunamwambia Lipumba amechelewa CUF iko imara na itaendelea kuwa imara.

JESHI LA POLISI:

Waheshimiwa wana habari,

Ni wazi kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likitumika kwa muda mrefu, juzi jeshi hilo lilidai kupata barua kutoka CUF Makao Makuu Zanzibar, jambo ambalo sio la kweli, ni jambo la uongo kabisa hakuna barua iliyotoka ya kuijulisha ujio huo. Tunalinasihi na kulitaka Jeshi la Polisi kuacha mara moja mtindo wa kulitumikia CCM na makundi ya uasi ya vyama vya siasa. Hali hii inaweza kusababisha uvunjifu wa amani. Wana CUF hatutokubali kabisa kuona mtu yoyote anatuvurugia chama.

ULINZI WA OFISI ZA CHAMA:

Kwa sasa chama kinaendelea kuimarisha ulinzi kwenye ofisi zake zote ili kujikinga na hujuma za wahalifu na uhalifu wowote ule. Na ndio Lipumba na wenzake hawakuthubutu kabisa kukanyaga Ofisi yoyote ya chama hapa Pemba na ziara yake iliishia kwenye majengo ya CCM. Tunawahakikishia wananchi kwamba Blue guard wetu na vijana wetu wapo imara na wanafanya kazi zao vizuri na chama kinawapongeza sana.

MWISHO.

Sisi CUF tunawaambia na kuwahakikishia wana CUF na Wananchi wote kwamba ujio wa Lipumba Pemba haukuwa na madhara yeyote kwa Chama na zaidi uliwaongezea ari wana CUF kisiwani Pemba. Hivyo Lipumba na CCM wenziwe walikuja kupoteza muda wao na kujifedhehesha kutokana na dhambi zao za usaliti. CUF ipo imara na wana CUF wapo imara.

Ahsante sana.
HAKI SAWA KWA WOTE.
fb

Share: