Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSIANA NA MWENDELEZO WA HUJUMA ZA DOLA DHIDI YA THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI)

Taarifa ya Maalim mchana wa leo.

Date: 27 Julai, 2017

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSIANA NA MWENDELEZO WA HUJUMA ZA DOLA DHIDI YA
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – CHAMA CHA WANANCHI)

UTANGULIZI:

Jana, tarehe 26 Julai, 2017, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Yustino Ndugai, alitoa taarifa kwa Watanzania akieleza kwamba eti amejiridhisha kuwa Wabunge wanane wa Chama Cha Wananchi (CUF) ‘wamefukuzwa Uanachama kulingana na taratibu za Chama hicho na hivyo wamekosa sifa za kuendelea na Ubunge”. Wabunge hao ni:-

1. Mhe. Severina Silvanus Mwijage, (MB);
2. Mhe. Saumu Heri Sakala, (MB);
3. Mhe. Salma Mohamed Mwassa, (MB);
4. Mhe. Riziki Shahari Mngwali, (MB);
5. Mhe. Raisa Abdallah Mussa, (MB);
6. Mhe. Miza Bakari Haji, (MB);
7. Mhe. Khadija Salum Ally Al-Qassmy, (MB); na
8. Mhe. Halima Ali Mohamed, (MB).
Taarifa yake hiyo ikamalizia kwa kusema kwamba, “Mheshimiwa Spika ametangaza nafasi hizo kuwa wazi na pia kumuandikia Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ili aendelee na hatua zinazostahili kujaza nafasi hizo kwa Mujibu wa Sheria na Taratibu zilizopo”.

Hatua hii imekuja ndani ya saa 24 tokea alipotoa taarifa nyengine juzi, tarehe 25 Julai, 2017 ambapo alisema kwamba amepokea barua kutoka kwa Ibrahim Lipumba na Magdalena Sakaya ambapo wamemuarifu kuhusu uamuzi wa kile alichokiita “Baraza Kuu la Chama hicho kuwafukuza Wabunge wanane (8) na Madiwani wawili kwa makosa kadhaa ya kinidhamu”. Alisema anaendelea kutafakari barua hiyo; na taarifa rasmi kuhusu maamuzi ya Spika ataitoa hapo baadaye.

Taarifa hiyo yenyewe nayo ilitolewa siku moja tu baada ya mtu anayeitwa Ibrahim Lipumba kutangaza kwamba eti aliitisha kitu alichokiita “Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi (CUF)” na kwamba eti hilo aliloliita “Baraza Kuu” limewafukuza uanachama Wabunge hao wanane (8) na Madiwani wawili (2) na kwamba tayari wameshamuandikia Spika wa Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu uamuzi huo.

YALIYOTEKELEZWA HADI SASA:

Matukio haya bila shaka yoyote hayawastaajabishi tena Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwa sababu ni muendelezo tu wa hujuma kubwa zinazoandaliwa, kuratibiwa, kuendeshwa na kusimamiwa na Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumtumia kibaraka Ibrahim Lipumba na genge lake waliloliweka Buguruni na kulilinda kwa nguvu zote.

Mpaka sasa taasisi za kidola zifuatazo zimeonekana waziwazi zikishiriki kwenye hujuma hizi dhidi ya CUF kwa njia na namna tofauti:

1. Polisi ambao ndiyo waliyomuingiza kwa nguvu na kumlinda kibaraka Ibrahim Lipumba katika Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CUF uliokuwa ukifanyika katika Ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo Plaza siku ya tarehe 21 Agosti, 2016 kwa lengo la kuuvuruga Mkutano Mkuu huo. Polisi pia wakamuongoza na kumlinda Lipumba na genge lake kwenda kuvamia na kuvunja Ofisi Kuu ya Chama iliopo Buguruni, Dar es Salaam, siku ya tarehe 23 Septemba, 2016. Hata matukio kadhaa ya uhalifu yanayofanywa na genge hilo na kuripotiwa Polisi likiwemo lile la kuvamia, kupiga na kujeruhi watu wakiwemo waandishi wa habari waliokuwemo kwenye mkutano wa waandishi wa habari uliokuwa ukifanyika katika Hoteli ya Vina, Mabibo nayo hayakuchukuliwa hatua zozote. Polisi pia mara kadhaa wamemzuia Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, asitekeleze shughuli zake kwa upande wa Tanzania Bara kwa kuzuia ziara zake Wilayani.

2. Baadhi ya Wakuu wa Wilaya ambao walisimamia kuzuia ziara za Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, na viongozi wengine halali wa Chama upande wa Tanzania Bara; na wakati huo kuambatana na kumlinda kibaraka Lipumba aweze kufanya shughuli za CUF ambazo baada ya kufukuzwa hana uhalali tena wa kuzifanya.

3. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo ilijitwisha uwezo na madaraka (ambao Mahakama Kuu ya Tanzania ilishawahi kutamka kwamba haina) ya kutengua maamuzi ya vikao halali vya Chama ambavyo ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Taifa uliokubali barua ya Ibrahim Lipumba kujiuzulu Uenyekiti wa Chama; na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa ambalo lilimfukuza uanachama Ibrahim Lipumba na kuwasimamisha uanachama waliokuwa viongozi wengine kadhaa wa Chama. Ofisi hiyo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, inayoongozwa na Jaji ambaye ungetegemea ni mtu anayejiheshimu, baadaye ikashirikiana na genge hilo kuiba Shilingi 369 milioni, fedha za ruzuku halali ya CUF na kuzigawa namna wanavyojua wao. Ofisi hii pia ndiyo inayoratibu hujuma hizi kwa kuziandikia taasisi nyengine za dola ikihalalisha maamuzi mbali mbali haramu kama ilivyofanya kwa kuwasiliana na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), na pia Bunge wakati wa kupitisha wagombea wa Ubunge wa Afrika Mashariki.

4. Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambaye amekubali kuvunja Sheria ya Wadhamini (The Trustees’ Incorporation Act Cap. 318) huku akijua na akiwa na taarifa zote ambazo tulimpatia kwa maandishi kupitia barua mbali mbali za Chama, na tarehe 17 Juni, 2017, kuamua kusajili wajumbe feki wa Bodi ya Wadhamini ya CUF ili waweze kutumika kufuta kesi ambazo Chama kimezifungua katika Mahakama Kuu kupinga hujuma hizi zinazoendelea na pia kuweza kufanikisha kuchota fedha za ruzuku ya Chama zilizobakia ambazo zimezuiwa kutolewa kupitia zuio la Mahakama Kuu.

5. Ofisi ya Spika wa Bunge ambayo katika uchaguzi wa Wabunge wa Afrika Mashariki ilipuuza barua rasmi iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, kumtambulisha mgombea wa CUF aliyepitishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama na badala yake ikasimamia barua ya anayejiita “Kaimu Katibu Mkuu” wa CUF, nafasi ambayo haipo ndani ya Katiba ya CUF. Spika wa Bunge baadaye akaliongoza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linapaswa kuwa alama ya heshima na haiba ya Taifa katika kusimamia sheria za nchi na mikataba ya kimataifa ambayo Jamhuri ya Muungano imeiridhia kuvunja sheria hizo na mikataba hiyo kwa kupitisha na kuchagua Mbunge ambaye ameshafukuzwa kwenye CUF.

YALIYOFANYIKA WIKI HII:

Pamoja na hujuma hizo zote zilizofanikishwa na Ofisi zote tulizoziorodhesha hapo juu, lengo kuu (ambalo nitalieleza baadaye kidogo) bado halijafanikiwa. Ndipo ukasukwa huu mpango mpya wa kutengeneza Baraza Kuu feki ili kukamilisha mpango wao huo.

Hatua iliyoanza Jumapili, tarehe 23 Julai, 2017 na kutekelezwa kwa mwendokasi kufikia jana ya eti kuwafukuza uanachama Wabunge na Madiwani na hatimaye kuwavua Ubunge na Udiwani na kuteua wapya inalenga kudhoofisha Kambi ya Wabunge wa CUF na UKAWA ambayo imekuwa mwiba mkali dhidi ya kibaraka Lipumba na genge lake pamoja na Dola inayowatumia vibaraka hao dhidi ya njama zao za kuhujumu vyama vikuuu na makini vya upinzani na kuua demokrasia hapa nchini.

Watanzania wanapaswa wajikumbushe kwamba hata kama hicho kinachoitwa “kuwafukuza uanachama” Wabunge halali wa CUF kingekuwa kiko sawa, hatua kama hiyo hufuata taratibu zote za kisheria na kikanuni za Bunge kujiridhisha kwanza. Hilo limefanyika mara nyingi tu tokea mfumo wa vyama vingi vya siasa uliporejeshwa nchini mwaka 1992. Kwa nini mara hii kumekuwa na KASI YA AJABU katika kuridhia maamuzi hayo, kila hatua ikiwa haizidi SIKU MOJA?

Hivyo, Spika Job Ndugai anadhani Watanzania ni vichaa wamuamini kuwa alishachukua hatua ya kujiridhisha kuwa kuwa Wabunge wanane wa Chama Cha Wananchi (CUF) ‘wamefukuzwa Uanachama kulingana na taratibu za Chama hicho na hivyo wamekosa sifa za kuendelea na Ubunge” ndani ya SIKU MOJA TU? Na amejiridhisha vipi ikiwa hata hakuwasiliana na Katibu Mkuu wa Chama ambaye kwa mujibu wa Katiba ya CUF ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za Chama na pia kwa nafasi hiyo ndiye Katibu wa vikao vya Mkutano Mkuu wa Taifa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama? Lakini kama hiyo haitoshi, Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif Sharif Hamad, alimuandikia Spika Ndugai barua rasmi, Jumanne, tarehe 25 Julai, 2017 akimueleza kwamba hilo lililoitwa Baraza Kuu la Uongozi la CUF halikuundwa na wajumbe halali wa Baraza Kuu. Angekuwa na nia ya kweli ya kutaka kujiridhisha si hapo ndipo pangekuwa pa kuanzia kwa kuwepo kile wanasheria wanachokiita shaka inayoweza kuingia akilini yaani ‘reasonable doubt’? Hoja hiyo ni mbali na ukweli ambao hakuna Mtanzania asiyeujua kwamba uhalali wa kibaraka Lipumba na genge lake unapingwa kwa kesi ambazo ziko Mahakamani. Spika Ndugai aliyapuuza yote hayo kwa sababu ni kinyume na mkakati wa Dola wa kuihujumu CUF na kuua demokrasia Tanzania. Hapo ndipo Spika Job Ndugai alipolifikisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

KIKAO CHA DODOMA:

Kwa kifupi, yanayofanyika ni mchezo wa kuigiza tu lakini maamuzi yameshafanywa na Dola na waliobaki wanatekeleza tu maagizo.

Watanzania na Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa wajue kwamba hujuma hizi zote ambazo lengo lake kuu ni kuisambaratisha CUF na UKAWA zinasimamiwa na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) wakiwemo baadhi ya maofisa wake walioko Ikulu Dar es Salaam, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na pia kama tulivyoeleza awali Polisi, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), na Ofisi ya Spika wa Bunge.

Hapo jana tu, Jumatano, tarehe 26 Julai, 2017, majira ya saa 1.30 asubuhi huko DODOMA kulifanyika kikao cha wanasheria wa serikali wapatao 12 kutoka Bungeni, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambapo walitakiwa kumshauri Spika wa Bunge kwa kumuandikia maoni ya kisheria (legal opinion) kuhusiana na hatua hii ya kuwafukuza Wabunge hawa.

Wanasheria hao kwanza walitakiwa kutoa maoni ya kitaalamu bila ya kuzingatia maelekezo ya MABOSI wao na kwa pamoja walieleza kwamba kitendo cha chama chenye mgogoro na uko Mahakamani na kisha upande mmoja unafukuza Wabunge na Dola inasimamia hilo kitashusha hadhi ya Bunge, kitaifedhehesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi mbele ya jumuiya ya kimataifa, na kuitia aibu ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) ambayo ina jukumu la kuishauri Serikali.

Walipoambiwa waeleze maelekezo ya mabosi wao, wote walieleza kuwa wametakiwa kufuata MSIMAMO WA KUTOKA JUU kwamba Wabunge wa CUF wafukuzwe, isipokuwa wanasheria wa Bunge tu ndiyo ambao hawakuwa na maelekezo haya.

Hatimaye Spika Ndugai amefanya aliyoyafanya ambayo yamemuweka yeye na Bunge analoliongoza katika FEDHEHA NA AIBU KUBWA SANA!

Baada ya hatua ya jana ya Spika Ndugai, na kwa utaratibu huo huo wa mwendokasi, tayari Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshapewa maelekezo na leo au kesho watatekeleza maelekezo hayo kwa kutangaza majina ya watakaowaita “Wabunge wapya” wa kujaza nafasi hizo.

Bila shaka ilivyokuwa DOLA imeshaamua hivyo basi taasisi zote hizo zitaendelea kutekeleza mpango huo.

HATUA TUTAKAZOCHUKUA KWA SASA:

Wabunge wenyewe wameamua kufungua kesi Mahakama Kuu kupinga maamuzi haya feki ya Baraza Kuu feki na kutaka Mahakama Kuu itamke kwamba wao bado ni wanachama halali wa CUF na hivyo bado ni Wabunge halali wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CUF.

Hatua nyengine tutakazochukua kama Chama zitaamuliwa na Baraza Kuu la Uongozi halali la Chama ambalo linakutana katika kikao cha dharura kesho Ijumaa, tarehe 28 Julai, 2017.

WITO WETU KWA WANACHAMA:

Tunawaomba na kuwasihi wanachama na wapenzi wote wa THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) waendelee kuwa watulivu na kufuata maelekezo wanayopewa na Chama kupitia viongozi halali na vikao halali vya Chama. CUF kimepita katika dhoruba na misukosuko mingi katika historia yake tokea kilipoasisiwa mwaka 1992. Tulishinda dhoruba na misukosuko hiyo na tutaushinda huu uliopo na hatimaye kuibuka tukiwa IMARA ZAIDI.

HAKI SAWA KWA WOTE

SEIF SHARIF HAMAD
KATIBU MKUU

Tagsslider
Share: