Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUTOKA MAKAO MAKUU YA CUF ZANZIBAR

Tarehe: 24 Septemba, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) kimepokea kutoka
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kile kinachoitwa “Msimamo na
Ushauri wa Vyama vya Siasa kuhusu Mgogoro wa Uongozi wa Kitaifa wa
Chama cha Civic United Front (CUF)” ambao uliwasilishwa Ofisi Kuu ya
Chama, Buguruni, jana usiku.

Baada ya kupokea Ushauri huo, The Civic United Front (CUF – Chama Cha
Wananchi) kinapenda kueleza yafuatayo:

1. Sheria ya Vyama vya Siasa (Political Parties Act, No. 5 of 1992)
haimpi mamlaka wala uwezo wowote Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa
ushauri, msimamo au mwongozo kwa vyama vya siasa kuhusiana na maamuzi
ya vikao vya Chama.

2. Msimamo huo wa kisheria wa nchi hii umetiliwa nguvu na
kuthibitishwa na Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kupitia UAMUZI wa tarehe 9/5/2005 wa Jaji T.B. Mihayo katika kesi ya
Emmanuel Nyenyemela na Magnus Msambila v/s Registrar of Political
Parties & Others (Civil Case No. 6 of 2003) ambapo Jaji Mihayo aliamua
kwamba:

“… I do not see anywhere in the Political Parties Act where the
Registrar has power to bless or condemn meetings of political parties
or decisions that they make.”

Tafsiri ya uamuzi huo ni kwamba, “… Sioni popote katika Sheria ya
Vyama vya Siasa ambapo Msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga
vikao vya vyama vya siasa ay maamuzi ambayo vikao hivyo vinafanya.”

3. Kwa msingi huo, CUF hatukuomba ushauri kwa Msajili na hivyo
tunamwambia ushauri wake abaki nao mwenyewe.

4. Kwa msingi huo huo, tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote
kutambua kwamba Msajili hana uwezo kisheria wa kusikiliza mashauri
yanayohusiana na malalamiko dhidi ya maamuzi ya vikao vya vyama vya
siasa na na kuyatolea uamuzi. Uwezo huo ni wa Mahakama. Hivyo
tunawataka wanachama wa CUF na wananchi wote kupuuza ushauri huo wa
Msajili na wamwachie mwenyewe ndoto zake na propaganda za kitoto.

5. Ni fedheha na aibu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa mwenye hadhi ya
Ujaji kukubali kutumiwa kiasi hicho na kushindwa hata kufanya rejea
kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu tulioutaja hapo juu ambao umeweka bayana
kwamba hana madaraka na uwezo aliojifanya anao. Itakumbukwa kwamba
Wabunge wa CUF walifanya mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma
tarehe 15 Septemba, 2016 na kumtahadharisha Msajili asikubali kutumiwa
kufanya alichokuwa anatakiwa kukifanya. Ni bahati mbaya sana kwamba
amefanya kile kile ambacho Wabunge wa CUF walieleza kwamba walikuwa na
taarifa kuwa ameagizwa kukifanya.

6. Tunajua kwamba baada ya hatua hiyo ya Msajili kufanya kazi asiyo na
uwezo wala mamalaka nayo na katika kutimiza malengo ya wanaotuma,
mchana wa leo Prof. Ibrahim Lipumba na kikundi chake cha wahuni
kimevamia Ofisi Kuu ya CUF, Buguruni, Dar es Salaam na kupiga watu na
kufanya uharibifu wa mali. Tunamwambia Msajili wa Vyama vya Siasa
atabeba dhamana kwa yote yaliyofanywa na yatakayofanywa na kikundi
hicho ikiwemo watu watakaoumizwa na uharibifu wa mali utakaofanywa
kutokana na tamko lake hilo ambalo halina msingi wa kisheria.

7. Tunatambua yote haya yanafanywa kwa sababu watawala wameingiwa
kiwewe kutokana na hatua kubwa ambazo zimefikiwa na CUF katika
kupigania haki yake ya ushindi ulioporwa katika uchaguzi mkuu wa
Zanzibar wa tarehe 25 Oktoba, 2015. CCM haijakaa sawa tokea
iliposhindwa vibaya na CUF katika uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na
Madiwani mwaka 2015 na sasa imepata mfadhaiko kutokana na jinsi
jumuiya ya kimataifa ilivyosimama kidete kutetea maamuzi hayo ya
kidemokrasia na haki za binadamu za Wazanzibari na Watanzania kwa
ujumla. Ni vyema watawala na kibaraka wao Prof. Ibrahim Lipumba na
kikundi chake pamoja Msajili anayewatumikia wakatambua kwamba CUF
haiyumbishwi na michezo yao ya kitoto na itaendelea kusimamia malengo
yake ya kupigania haki za kidemokrasia za wananchi wa Zanzibar na
Tanzania kikamilifu.

8. Chama kinasisitiza tena kwamba maamuzi ya Mkutano Mkuu Maalum wa
Taifa wa tarehe 21 Agosti, 2016 na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la
tarehe 28 Agosti, 2016 ni halali na yako pale pale na kwamba Prof.
Ibrahim Lipumba si Mwenyekiti wa CUF na wanachama waliosimamishwa au
kufukuzwa wataendelea kubakia wamesimamishwa au kufukuzwa isipokuwa tu
iwapo vikao vya Chama vitakapofanya maamuzi mengine.

9. Chama kinawataka viongozi wake wote na wanachama wake katika ngazi
zote kuanzia Taifa hadi Tawi kuendelea na kazi zao za ujenzi wa Chama
kama kawaida na kuendelea kufuatilia harakati za Chama chao kupigania
ushindi wetu wa tarehe 25 Oktoba, 2015.

HAKI SAWA KWA WOTE

NASSOR AHMED MAZRUI
NAIBU KATIBU MKUU – CUF

Tagsslider
Share: