Habari

Taarifa ya Maalim Seif kujiunga na chama cha ACT

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI:

Mahakama Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Masjala Kuu ya Dar es Salaam) leo imetoa uamuzi wa Kesi Na. 23 ya 2016 ambayo tuliifungua kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia maamuzi ya ndani ya Chama pale alipotangaza kumtambua Prof. Ibrahim Lipumba kuwa Mwenyekiti wa CUF licha ya kujiuzulu na Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama kuridhia kujiuzulu kwake. Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu imesema kwamba Msajili alikuwa na mamlaka ya kufanya alivyofanya. Si nia ya mkutano wetu huu leo kuendeleza mabishano kuhusu suala hilo. Itoshe tu kusema kwamba kwa tafsiri yetu huu ni mwendelezo wa mpango uliosukwa na Dola kwa lengo la kuihujumu na kuidhoofisha CUF ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuhujumu demokrasia nchini.

Tumeshuhudia Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (RITA), lakini pia Polisi, Bunge na Mahakama vyote vikiwa sehemu ya mkakati huu. Dalili ya mwisho tulisema kwamba kuahirishwa kusomwa uamuzi wa kesi hii kutoka tarehe 22 Februari hadi leo tarehe 18 Machi ulikuwa na lengo la kutoa nafasi kwa upande unaobebwa na Dola kuandikisha tena Bodi yao ya Wadhamini na kufanya Mkutano Mkuu feki ili wakati uamuzi unatolewa iwe wametuingiza katika mgogoro mwengine. Labda lengo ni kutufanya tuendelee kupanda na kushuka Mahakamani huku tukishindwa kufanya shughuli za kisiasa. Sasa imetosha. Mapambano ya kisiasa lazima yaendelee.
Kwa msingi huo, mimi na wenzangu katika uongozi tumetafakari kwa kina juu ya upi uwe mwelekeo wetu iwapo maamuzi ya kesi yangekwenda hivi yalivyokwenda. Tumeona njia sahihi ni kutafuta jukwaa jengine la kuendeleza mapambano ya kisiasa tuliyokuwa tukiyasimamia kupitia CUF. Jukwaa tuliloamua kulitumia kwa kuelekeza nguvu zetu zote ni Chama cha ALLIANCE FOR CHANGE AND TRANSPARENCY (ACT – WAZALENDO).

Hivyo, nawatangazia Watanzania wote na hasa wanachama wa CUF walio wengi waliokuwa wakituunga mkono kutoka kila pembe ya nchi, Tanzania Bara na Zanzibar, kwamba mimi na wenzangu tunajiunga na Chama cha ACT – WAZALENDO. Tunawaomba na wao wote waungane nasi kujiunga na jukwaa hili jipya ili kuendeleza kazi kubwa tuliyokuwa tukiifanya kupitia CUF.

Nichukue fursa hii kwa niaba ya wenzangu kuwashukuru wananchi wote waliojitolea kwa kutuazima nyumba na sehemu zao kutumika kama ofisi za Chama za ngazi mbali mbali katika kipindi chote tulipokuwa CUF. Nawaomba waendelee kutuunga mkono huko tunakokwenda kwa kuendelea kutuazima nyumba na sehemu hizo sasa zitumike kwa jukwaa jipya tunaloekea la ACT-WAZALENDO.
Nimalizie kwa kuwaambia Watanzania kuwa mapambano ya kujenga demokrasia na kusimamisha utawala wa haki unaoheshimu utawala wa sheria si kazi ya lelemama. Tumefanya kazi kubwa mpaka hapa tulipofikia. Ni jukumu letu na wajibu wetu sasa kuikamilisha kazi hiyo.

Tunahitaji JAHAZI la kutufikisha kwenye TANZANIA MPYA inayoheshimu utu, ubinadamu, haki na yenye neema inayofikia wananchi wote. Jahazi hilo ni ACT-WAZALENDO. Pamoja na kuamua kulitumia jukwaa la ACT-WAZALENDO, niwahakikishie kwamba bado tunaamini katika USHIRIKIANO WA VYAMA VYOTE MAKINI VYA SIASA na makundi mengine ya kijamii katika mapambano yetu ya kuleta demokrasia na haki nchini.

Hatua tunayochukua leo ni kuandika historia mpya ya mabadiliko ya kisiasa Tanzania, kote Zanzibar na Bara. Umma haujawahi kushindwa popote duniani. Ndivyo historia inavyoonesha kote. Hatuna wasiwasi kwamba Umma wa Watanzania nao utashinda.

Kauli yangu kwa wana-CUF wote wanaotuunga mkono na Watanzania wote kwa jumla ni kwamba WAKATI NI HUU, WAKATI NI SASA.
SHUSHA TANGA, PANDISHA TANGA! SAFARI IENDELEE!

SEIF SHARIF HAMAD
18 MACHI, 2019

Share: