historiaNyaraka/Vitabu

MJUE SHEIKH HASSAN BIN AMEIR.

MJUE SHEIKH HASSAN BIN AMEIR

(Na HAMZAH Z. RIJAAL)

Katika mfululizo wa makala za wanavyuoni wetu hii leo tutamuangalia alimu mkubwa wa Zanzibar na Afrika Mashariki kwa jina ni  Shekh Hassan Bin Ameir Bin Mazi Bin Haji Bin Khatib Al-Shirazy aliyezaliwa mwaka wa 1300 AH (1880 CE).

Sheikh Hassan Bin Ameir amezaliwa Mkoa wa Kusini Unguja katika kijiji cha Mtegani, Makunduchi. Sheikh Hassan alianza masomo yake ya Quraan hapo kwao Mtegani, ambapo hakudumu kipindi kirefu na kuhamia Dunga amabapo nako huko alikuwa akisoma chuwoni, baada ya hapo akelekea Upenja ambapo alikuwa ni mmoja kati ya wanafunzi waliokuwa wakimudu fani ya tajwidi.

Sheikh Hassan hakusitia hapo, kwani baada ya kuondoka Upenja aliingia mjini na hapo alipata fursa ya kusoma kwa Maulamaa wa nyakati hizo ambao kwa leo utawaita kama ni Ma-Professa, kwani walimu hao waliomiminia elimu walikuwa kila mmoja wao akimwambia mwenzake nipishe. Kati ya hao walimu wake alikuwa ni Sheikh Hamdani Bin Abdulkadir Al-Qahtan, Sheikh Said Bin Dahman, Sheikh Muhammed Bin Abdaulla Bin Wazir, Sheikh Ali Bin Mandhry huyu alisoma kwake huko Pemba, Sheikh Abdulrahman Bin Mahmoud, Sheikh Abdulrahman Bin Hassan, Sheikh Muhammad Bin Ali Khamis Al-Barwany, Sheikh Abdaullah Bin Amour bin Muhammed al-Mendhry na Sheikh Abdulla Bin Amour al-Azzi. Mbele ya mashekhe hao alisoma ilimu zote ikiwa pamoja na Fiqh, tafsiri ya Quraan, fani zote za lugha, sayansi ya hadithi za Bwana Mtume Muhammad S.A.W na maulamaa wote hao ! walimkubali kuwa mwanafunzi wao ataweza kuendeleza kile walichomfunza.

Sheikh Hassan Bin Ameir alianza na kazi ya kusomesha kabla ya kujiunga na mahkama ya kadhi, na alipokuwa anasomesha aliweka madrsa yake hapo mtaa wa Misufini madrasa iliyokuwa ikijulikana kwa jina la “Madrasa el-Shirazi”, watu wengi walinufaika na madrasa hiyo, ingawa kwanza ilikuwa na wanafunzi wengi kutoka sehemu za kwao Makunduchi lakini kipindi kisichokuwa kirefu  wanafunzi walikuwa wakifurika kutoka sehemu mbali mbali za Unguja, Pemba, Mrima na baadhi ya sehemu nyenginezo za maeneo ya Afrika Mashariki na kati kwenda kusoma kwa alimu huyu.

Ingawa Sheikh Hassan alikuwa ameshapea na kuwa mwalimu lakini alikuwa hajasita na kusoma sio kwa kujisomesha mwenyewe tu lakini ilikuwa kwa kupiga goto na kwenda popote pale panapotolewa elimu ndipo alipokuja Unguja Sheikh Abdulbari Al-Aziy kutoka Misri, Sheikh Hassan Bin Ameir  alikuwa mmmoja katika wanafunzi waliojiunga kwa kupata taaluma kwa mwalimu huyo, na kati ya mengi aliyoyasoma hapo ilikuwa pamoja na uandikaji wa khati, na inasemekana Sheikh Hassan alikuwa na khati nzuri sana za kiarabu kwa maandishi ya “nusha” na “rika”, vile vile alisoma masomo ya hesabu ambayo ni muhimu katika fani ya mirathi na kuna mmoja aliyowahi kusoma kwake alifika kueleza kuwa “ulipokuwa ukiingia mlango wa mirathi kila mmoja akisikia raha kutokana na namna Shekhe alivyokuwa akimudu mada ya mirathi”. Sheikh Hassan alijifunza kis! wahili cha skuli kwa mwalimu wa kiengereza Mr. River Smith, na alipomaliza msomo hayo akapatiwa cheti kilichomruhusu kusomesha katika skuli za serekali na kuweza kufanya kazi popote pale anapotakiwa mtu wa elimu ya dini.

Sheikh Hasasan alisomesha skuli nyingi tu humu visiwani zikiwemo skuli za Makunduchi, Muyuni, Kiembe Samaki, Chake Chake Pemba na kwengineko.

Wengi wa wanafunzi wake walishika nyadhifa mbali mbali katika sehemu zao akiwemo Mufti wa Ngazija Muhammed b Abdulrahman, Sheikh Fatawi Bin Issa aliyekuwa kadhi baada ya kuwacha Sheikh Abdaalh Farsy, Sheikh Ameir Tajo Al-Shirazi naye pia alikuwa kadhi mkuu wa Zanzibar, Sheikh Rashid Bin Haji Al-Shirazi wa Tabora, Sheikh Abdaalh Iddi Chaurembo wa Mrima, Sheikh Ramadhan Abass wa Mrima, Sheikh Masoud Bin Khatib wa Rufiji, Sheikh Abdulmuhsin Bin Kitumba wa Ujiji-Kigoma, na wengi wengineo ambao nao wameweza kutoa mchango mkubwa wa kuelimisha watu elimu ya dini ya kislamu.

Sheikh Hassan Bin Ameir aliwacha kazi ya ualimu na kujiunga na mahkama akiwa kama karani, na nyakati hizo zilikuwa sio elimu yako tu ndio inakubalika lakini shakhsia yako nayo ilikuwa ni kiegezo cha kuweza kupata kazi, aliifanya kazi vilivyo na kwa uadilifu kabisa na hakuna yeyote yule aliyewahi kumtia ila juu ya kazi yake.

Sheikh Hassan alielekea bara kwa kustakimu na kufanya kazi kubwa ya tabligh, kuna wengine wanaosema kuwa kule bara aliitwa kwenda okoa jahazi, kuna wengine wanasema alikwenda kwa hiari yake, itavyokuwa Sheikh Hassan Bin Ameir alifanya kazi kubwa sana ya kusomesha na hata pale ilipoundwa jumuia ya “The East African Muslim Welfare Society” iliyokuwa chini ya ulezi wa Kiongozi Mohammed El Husaini Aga Khan iliyoasisiwa katika mwaka wa 1945, Sheikh Hassan b Ameir alikuwa katika washauri wakuu na hata pale msafara wakwenda Misri,Lebnon na nchi nyengine za kislamu kwa kutafuta msada wa kujenga Chuo Kikuu Cha KIislamu Sheikh Hassan Bin Ameir alichaguliwa kuwa ndio kiongozi wa msafara huo ukijumuisha watu wengine akiwemo Sheikh Tewa Said, Mwinyi Baraka na wengineo maelezo zaidi ya msafara huo na kazi zake za Mrima pitia kitabu cha Ndugu Muhamed Said “The Life and ! Times of Abdulwahid Sykes”.

Sheikh Hassan alipokwenda Hijja marejeo yake alipitia chuo kikuu na kikongwe duniani chuo cha Al-Azhar huko aliweza kupatiwa fursa ya kutoa mhadhara mdogo ambao wengi walishtuka kuona mtu ambaye amesoma Unguja tu na Pemba yake kuweza  kuwa na umahiri na umilikaji mkubwa wa lugha ya kiarabu hata Sheikh Mahmoud  Zuttuti kumkubali na kusema kuwa “Afrika masahariki imepata lulu”.

Dunia mdawari hilo mja ulijue, Shekhe alirejeshwa Zanzibar katika mwaka wa 1968 kutoka bara, naye alirudi nyumbani bila ya ukaidi, kurudishwa kwake ni kitandawili  kikubwa hakitatuliwa humu, hata hivyo alipokewa na kupewa kazi katika Mahakama ya Rahaleo, Mahakama ya suluhu .

Sheikh Hassan alibarikiwa kupata fursa ya kuandika vitabu na kati ya vitabu alivyoviandika ni:

-Wasialatul Rraja (Shrerehe ya Safinatul Najaa)

-Fathul Kabir (Sherhe ya Mukhtasarul Kabir)

-Idhanil Maani Fi-Asamail Husana (Sherehe ya Taibatil Asmai

-Musliku Karib Fi mughnil Muhtaj (Sherehe ya Maslaqul Qarib)

-Madarijul Ulaa (Sherehe ya Tabaraka Dhul Ulaa

Na baadhi ya vitabu alivyoviandika na kutochapishwa ni pamoja na :

-Tuhfatul Zinjibariya( Sherehe ya Robol Ibada)

-Maulidi barzanji (Sherehe ya Maulidi ya Barzanji)

-Anwaru Saniyyat (Sherehe ya Addurarul Bahiya)

Sheikh hassan Bin Ameir alifunga macho tarehe  8 Oktoba mwaka wa 1979 katika mtaa wa Michenzani na kuzikwa kijijini mwao Mtegani Makunduchi. Maziko yake yalikuwa makubwa mno, kwa wale wanayakumbuka, kwani mbali ya wakazi wa Zanzibar watu wengine walitoka nje ya Zanzibar kwa  kuja kumlaza kigogo hichi.

Nuru yake ipo na inangara hadi leo, lakini bado kazi nzito inahitajika kufanyika kuanzia Makunduchi hadi mjini Unguja na Pemba ili Zanzibar iwe katika makamo ya mashekhe zetu hawo  waliopita ambao Maarifa wamewavalia njuga kuwaeleza japo kwa mukhtasari.

Mola tupe kila yalio mema, na utupe satwa ya kufwata nyayo za watangulizi wetu “AMIN”

(Maelezo haya mafupi nimeyapata kwa Sheikh Salmin Bin Hafidh ambaye naye amepokea kwa Sheikh Ameir Tajo, Haji Bin Hafidh, Hamid Bin Hafidh)

Share: