Habari

TAMKO KUHUSU MASHEKHE WA UAMSHO NA WAISLAMU WENGINE WENGI WANADHALILISHWA KATIKA MAGEREZA BILA KUWA NA HATIA, LILILO TOLEWA JANA NA SHEIKH KHALIFA KHAMIS MWENYEKITI WA TAASISI YA IMAMU BUKHARI

Mashekhe wanaokwenda kupekuliwa wanavuliwa nguo uchi wa mnyama kama walivyo zaliwa mbele ya watoto wadogo huu ni udhalilishaji wa hali ya juu sana. tungeomba serekali iyasikie haya na iliondoe hili tatizo. Halikadhalika tunaomba serekali iweke wazi kwa nini hairuhusiwi kwa shekhe au muislamu mwengine yoyote aliyeko gerezani kuonekana na zaidi ya mtu mmoja ila baada ya siku kumi na nne.

Akija mke wake au ndugu yake kuonana nae leo, mtu huyu ahesabu siku 14 zipite yaani siku ya kumi na tano ndio atakuwa na ruhusa tena ya kumuona mtu wake. “Haya mambo hayapo katika sheria” yamewekwa maalumu kwa kuwadhalilisha waislamu. Huu ni unyanyasaji na udhalilishaji, kwahiyo mimi nichukue fursa hii kwa niaba ya waislamu wote kumpongeza sana Mh Edward Lowassa kwa kuona kwamba jamii miongoni kwa watanzania inadhalilika/inadhalilishwa na haitendewi haki.

Kama yeye aliyasema maneno haya kwa kutafuta faida za kisiasa hayo ni yake yeye. Lakini aliyoyasema ni maneno ya haki na ukweli kwamba waislamu wale wanadhulumiwa, wamekaa siku nyingi jela. Kama alivyosema yeye na kama lilivyosema baraza kuu la waislamu Tanzania ambalo sisi tunalitii tunaunga na wote wale wanaosema kwamba watu hawa wamekwisha kaa jela sana wapelekwe mahakamani.

Sheikh Farid na Sheikh Msellem wamekamatwa mwaka 2012 mauwaji ya kibiti yalikuwa hakuna kwa nini leo tunaambiwa wanahusika na mauwaji yanayofanyika huko na wao wapo jela?

Kuna mtu mmoja kule Zanzibar anaitwa balozi Seif Ali Iddi ambae ni makamo wa rais ndio aliwakamata kina Sheikh Farid Zanzibar wakawaleta huku (Tanganyika). Na wao walieleza sababu za kuwakamata “walisema wanaichezea serekali na tumeshawapeleka Bara waende wakanye ndani ya ndoo.

Mtu mzima tena ni makamo wa rais mbele ya mkutano wa hadhara anazungumza maneno ya kuwasimanga watu ambao wapo katika mikono ya sheria?
Lakini imekuwaje leo tunaambiwa kwamba hawa wanahusika na mauwaji? Tufanye na iwe kweli wanahusika na hayo mauwaji labda kuna kipindi huwa wanatoroka jela wanaenda kuuwa halafu wanarudi jela.

Yote haya tunawaachia vyombo vya usalama na upelelezi ambavyo vina mamlaka mkubwa na uwezo wa kupeleleza. Lakini tunasikitika na tunaona vibaya sana katika nafsi zetu kwa namna ndugu zetu wanavyodhulumiwa, kunyanyaswa, kuteswa, kupigwa, kulawitiwa yote haya wanafanyiwa.

Miongoni mwa hukumu na adhabu anazostahili muhalifu ni pamoja na kulawitiwa? Pamoja na kuingizwa machupa sehemu za siri? Pamoja na kuvunjwa miguu? Wakati tumesoma hapa vifungu vya katiba vinasema ni makosa na inakatazwa kumpiga mtu wala kumtazama kama mfungwa au muhalifu kama hajathibitishwa na mahakama.

Vipi munawachukulia watu ni wakosaji, wahalifu ilhali mahakama haijathibitisha? hamuwezi kuwapeleka mahakamani?

Mwisho naomba niseme kwamba rai yetu na wito wetu kwa waislamu wote nchini Mashekhe, Maimamu, Waalimu wa madrasa nchi nzima wawafahamishe waislamu wenzao katika mihadhara na katika mimbar/misikitini za siku ya Ijumaa kwamba jela kuna waislamu waliokamatwa kwa kudhaniwa kuwa ni magaidi.

Vivile baada ya waislamu kueleweshwa jambo hili tunaomba wajitokeze kuchangia fedha kwaajili ya kuwalipa mawakili pia kusaidia kuendesha familia za ndugu zetu ambao wapo magerezani. Wasione woga kufanya hivo na wafanye hivo mchana kweupe. Waende mbele ya viongozi wa kiserekali wakawaulize kuhusu ndugu zao kisha wafate taratibu zinazokubalika kisheria.

Taarifa hii muhimu wawe nayo kwamba kule kuna wenzetu. kwa msingi huo wasilale wasinywe, wasile, wasishibe wala wasistarehe mpaka wajue wamewasaidiaje ndugu zao. Hili ni jambo kwanza.

Jambo la pili; katika kila mkoa ziundwe kamati za waislamu zenye wajibu wa kuhakikisha zinatambua uwepo wa Waislamu wanao tuhumiwa ugaidi katika magereza ya eneo lao, kwa shabaha ya kwenda kuonana na maofisa wanaohusika na magereza ili kupewa haki wanazostahili kapewa kama wenzao.

Nendeni katika ofisi za magereza za mkoa mukutane na kamanda mumuulize kuna waislamu wenzetu huku vipi haki zao za msingi je tunaweza kuwasaidia dawa, chakula nguo nk.

Jambo la kushangaza ukonga hairuhusiwi kwa mahabusu wa kiislamu kuwa na nguo zaidi ya mbili. Haya ni masharti ya unyanyasaji tu. Na kwa nini unyanyase wakati kuna mahakama?

Ugaidi si jambo ambalo mtu anaweza kulificha mfukoni. Ugaidi ni matendo ya kutisha yanayowafanya watu waishi kwa ghofu, ugaidi huleta hasara ya mali na vifo.

Sasa watu ambao wanashitakiwa kwa kuleta vitisho katika nchi, kwa kufanya vitendo ambavyo vimeiweka nchi katika hali ya hatari mpaka leo ushahidi wao haujapatikana miaka sita saba sasa. Je ushahidi huu wakutunga? Ushahidi huu wa namna gani ambao miaka saba haujapatikana?

Kwa sababu sisi hatujajua ni mahala gani walipokwenda kufanya hayo makosa Hatupajui ni mahala gani waliporipua. Labda serekali unajuwa na kama inajuwa sababu ya kutokwenda mahakamani ni nini?

Mwisho niungane na baraza kuu la waislamu Tanzania kuiomba serekali hususan Rais John Pombe Magufuli ambae sisi tulimchagua (mimi Sheikh Khalifa nilimchagua)

Basi tunaitaka serekali iharakishe upepelezi pia tunamtaka Rais Magufuli afahamu ndani ya Magereza kuna waislamu wengi wamebambikwa kesi. Kesi za kubambikwa ni nyingi katika hao waliokamatwa. Kwa nini waendelee kuteseka kisha ipokewe kwa kila anaeambiwa ni gaidi iwe ni mtu mbaya na kutengwa?

Kina Sheikh Farid walichokamatiwa kwa mujibu wa serekali ya Zanzibar walikuwa wanapinga Muungano wanataka Zanzibar huru. Haya ni mawazo yao. Kuna watu wanataka serekali tatu alizopendekeza Warioba, kuna watu wanataka serekali mbili kama ilivyo sasa, kuna watu hawataki huu Muungano wenyewe wanasema ni ukoloni sio Muungano.

Haya yote ni mawazo ya watu na hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kuzuia mtu kufikiri. Kina Sheikh Msellem na wenzake wao walisema kuwe na serekali tatu hayo ndio mawazo yao. Serekali ya Zanzibar wakasema hawa wanachezea serekali.

Na majuzi wamekariri maneno ya Dr Salmin Amour wanasema unaweza kuchezea ndevu lakini huwezi kuchezea serekali ndio maana tumewapeleka wakanye ndani ya debe. Huyu balozi Seif Ali Iddi ni mtu wa hatari manaake katika uongozi kiongozi hawezi kuropoka-ropoka tu namna kama hii kumbe anafurahia mateso kwa raia wake?
Kwa sababu tu raia wapo tofauti na mawazo yake?

Hii inatuudhi na inatuuma na tunaishitakia serekali kwamba waislamu wote tuko pamoja na yeyote ambae anasema watu wale wapelekwe mahakamani wakashitakiwe na wapewe fursa ya kujitetea kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi.

Na ikiwa hawana mashtaka waachiwe huru. Lakini kwa kusema tu kama hawa wanamakosa wacheni vyombo vifanye kazi ilhali tunajua kwamba kuna watu walikamatwa kwa kesi za kubambikwa hata Rais akitaka tutamuonesha kwa sababu tunawajua. Lakini unafikaje kwa Rais utamuonaje? Kuna watu wanamuambia na wanataka yale wanayomwambia ndio Rais ayatekeleze.

Kwa hiyo ndugu waandishi nisipoteze muda mrefu sana kitu cha msingi hapa ni kwamba “tunasema masheikh wamekaa ndani sana” na sio watu 23 pekee aliowasema Mh Lowassa ni zaidi ya watu 200 kwa hapa dar es Salaam. Arusha kuna watu 68 tazameni karatasi za majina hakuna hata mmoja ambae sio muislamu. Hii sheria inamakengeza ya kutokuona watu wengine inaona waislamu tu?

Je! Hii ni sheria ya kibaguzi au utekelezaji wake unaleta athari na taswira ya ubaguzi?

Asanteni sana kwa kunisikiliza

Tagsslider
Share: