Habari

TAMWA washirikiana na mitandao ya kijamii kupinga udhalilishaji

July 3, 2018

Imeandikwa na Salmin Juma.

Chama cha waandishi wa habari wanawake TAMWA –Zanzibar kimewataka waandishi wa habari kutumia mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe wa kupinga vitendi vya udhalilishaji na ukatili kwa wanawake na watoto ambao unaonekana kutuama nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mafunzo maalum ya siku moja ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kuripoti habari za usawa wa kijinsia katika mitandao ya kijamii mratibu wa TAMWA , Bi Asha Abdi amesema, mitandao ya kijamii inaonekana ndio njia rahisi ya kuwafikishia watu ujumbe kwakua waliyowengi wanaitembelea.

Amesema, hali ya vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto nchini Zanzibar si ya kuridhisha kwani matukio mbalimbali yangali yanaendelea kuripotiwa hivyo ni vyema kwa kwaandishi wa habari kuzidisha juhudi kuvitripoti vitendo hivyo kupitia mitandao ya kijamii kama vile ,blogi, website facebook nk.

“hali ya udhalilishaji sio nzuri, na TAMWA kupitia mradi wake wa Media Platform to fight GBV unaofadhiliwa na DANIDA tumeona kuna umuhimu wa kuwashirikisha waandishi wa habari wanaoposti habari mitandaoni kwa lengo la kufikisha ujumbe wa kupinga matendo ya udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto “amesema Bi Asha.

Akichangia mada ya “dhana ya kijinsia” Salma Said mwandishi wa habari wa Zanzibar Yetu amesema udhalilishaji upo nchini na miongoni mwa sababu zinazopelekea matukio hayo ni uwasili wa maisha ya watu tokea walipoanza kukulia hivyo upande mmoja hasa wanawake imezoelekea kuonekana upo chini katika kila eneo.

Nae Muhammed Khamis mwandishi wa habari kutoka gazeti la mwananchi ambae pia ni mwanahabari mtandaoni amesema, kitendo kilichofanywa na TAMWA ni kitendo kizuri kwani watu wengi hivi sasa wanafuatilia mitandao hivyo kuwapa mafunzo wanahabari kuandika mitandaoni kutasaidia vikubwa kuondosha matendo hayo thakili.

“nawapongeza sana TAMWA dunia hivi sasa imeahamia mtandaoni na naamini ujumbe utawafikia watu kiurahisi sana na mabadiliko yataonekana” amesema Khamis.

Mafunzo hayo ya siku moja yaliwashirikisha waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mtandaoni kama vile Zaima Tv, PembaToday na Mazrui Media na kwa pamoja wameondoka na azma ya kwenda kuripoti habari za matukio hayo zitakazoleta mabadiliko ya haraka.

Pemba Today

Share: