Habari

Tanzania ina mabalozi tisa kutoka Zanzibar

April 13, 2018

NA FATINA MATHIAS, DODOMA

WIZARA ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema Tanzania ina balozi 40 nje ya nchi na kwamba mabalozi wanaotoka Zanzibar ni tisa sawa na asilimia 22.5.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk.Suzan Kolimba alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Baraza la Wawakilishi(CCM) Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua balozi zote za nje ya Tanzania zipo ngapi na Zanzibar ina mabalozi wangapi.

Dk. Kolimba akijibu swali hilo, alisema Tanzania ina balozi 40 nje ya nchi huku mabalozi wanaotoka visiwani Zanzibar wakiwa tisa sawa na asilimia 22.5.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Wingwi(CUF), Juma Kombo Hamad alitaka kujua Zanzibar ina nafasi gani katika Jumuiya za Kimataifa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri wa Tanzania.

Naibu waziri huyo alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na mabadiliko yake, masuala ya mambo ya nje yapo chini ya mamlaka ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikihakikisha serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashiriki kikamilifu kwenye masuala yote ya kimataifa.

Alisema masuala hayo ni pamoja na ziara za viongozi wa nchi na mashirika mbalimbali ya kimataifa zinazofanyika nchini, ziara zinazofanywa na viongozi wa kitaifa na mikutano ya pande mbalimbali.

Aidha alisema mikutano ya mashirika na taasisi za kimataifa na kikanda na mikutano ya pande mbili na Zanzibar kuwa mwenyeji wa mikutano na makongamano ya Kimataifa.

Hata hivyo alisema viongozi wa Zanzibar wamekuwa wakiongoza ujumbe wa nchi kwenye mikutano mbalimbali ya kimataifa.

“Katika mwaka 2017/18 serikali ya Zanzibar imeshiriki katika mikutano ipatayo 11 ya mashirika na Taasisi mbalimbali za kimataifa, imeshiriki katika ziara nne za viongozi mbalimbali wa mashirika na taasisi waliofanya ziara nchini imekuwa mwenyeji wa mikutano na warsha zilizosimamiwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa,” alisema.

Zanzibarleo

Share: