Habari

TANZANIA TUKAE TAYARI KWA RAIS WA MILELE.

Tanzania/Tanganyika imepitia wakati mgumu sana huko nyuma wakati wa Hayati Mwalimu Nyerere, kweli tulikuwa na amani ya kutosha muda wake wote ukiondoa wakati ule alipotutia vitani na Uganda. Lakini kiuchumi na kisiasa tulikuwa na tumebaki nyuma sana, kiasi kwamba mpaka sasa matatizo tuliyonayo mengi chanzo au kiini chake hasa ni siasa za kubahatisha alizokuwa akiziunda, akizihakiki na kuzitekeleza huku akitawala kama vile mkemia mkuu afanyavyo tafiti zake akiwa katika maabara. Siasa za ujamaa na kujitegemea, (vijiji vya ujamaa nk), azimio la arusha, muungano pamoja na kulazimisha kiswahili, kitu ambacho ni jambo jema katika kuondoa ukabila, lakini madhara yake kielimu kwa vizazi vyetu imekuwa msiba wa kudumu, hasa kwa kuwa lugha yetu bado ilikuwa changa na haijitoshelezi.

Tanzania bado ni uwanja wa kufanya majaribio yote ya kisiasa, kwasababu bado nchi yetu haiongozwi na sheria au katiba. Hivyo vitu tunavyo siku zote, lakini  sisi  huogozwa kwa kutegemea nani “rais” wa wakati huo, na ana uwezo gani katika kuifanya kazi hiyo. Ndio maana  hivi karibuni rais mstaafu Kikwete, alikiri wazi kuwa hakuna chuo chochote nchini cha kujifunza kazi hiyo. Hivyo ni wajibu wetu kumuomba Mola mara zote, wakati wa kumchagua mtu huyo tuombe awe na akili timamu. Pia kauli  hiyo inaonekana kuungwa mkono kila siku  na rais Magufuli, kwa sababu yeye pia hutukumbusha tumuombee siku zote. Kitu ambacho ni kizuri, tatizo maombi peke yake hayatoshi, hasa ikiwa mtu au watu tunao wachagua hawamuamini wala hawampendi Mungu wetu sisi. Kwasababu ikiwa wana imani na muumba wetu sote, wala wasinge thubutu kuteka watu, kuuwa, kuiba au kudhulumu haki ya walio wengi na kujipa wao wachache. Wanafanya hivyo kwa kuwa wanaziabudu na wanaziamini zaidi silaha za moto walizowakabidhi wananchi waliowatia umasikini usio wa lazima na kuwakabidhi silaha hizo kama sehemu ya ajira ili wapate mkate wao (riziki).

Tanzania au watawala wetu kwa sasa wako katika mikakati ya kubadilisha katiba ili rais wa Tanzania au ‘Tanga’ na ‘nyika’ aweze kutawala kwa miaka saba badala ya mitano. Pia kusiwe na kikomo, kama vile ilivyo Uganda kwa Museveni na Rwanda ya Kagame. Wote hawa viongozi wawili waliapa miungu yote, kuwa hawatotawala zaidi ya katiba za nchi zao zinavyotaka. Lakini wote hawa wamezigeuza katiba hizo katika vipindi muafaka ulipofika na sasa ndio watawala wa milele au miungu watu wa kudumu.

Naomba niwape mifano kidogo kwa kuwa muda sina wa kutosha. Hili jaribio la kutaka kumuuwa mbunge wa Singida ya Mashariki, mheshimiwa Tundu Lissu ni sehemu ya kuwaondoa bungeni wabunge wote walio kufa wadudu au wale wanaojiamini mapema, ili wakati wa kubadili katiba ya kusimika rais wa milele ikifika wawe wote marehemu au hawapo bungeni. Mpango unaoendelea hivi sasa nchini kote wa kuwanunua wabunge wa upinzani kwa mamillioni na  ghafla wanajiuzulu na kujiunga na chama tawala, ni sehemu pia ya mpango huu kabambe. Kwa wale wasionunulika wote wako magerezani wana kesi za kujibu na watatumikia vifungo tofauti zaidi ya miezi sita, ili wakitiwa hatiani basi ubunge nao huwa umefikia kikomo, kwa kuwa mbunge akifugwa miezi sita na kuendelea huwa hafai tena na jimbo lake linakuwa wazi.

Mpango wa kuwanunua madiwani wa upinzani wa kata za nchi nzima, pia ni sehemu kubwa ya kuweka serekali za mitaa katika wilaya zote muhimu ili wakati ukifika itakuwa ni maoni na kura za NDIO TUPU.

Ni vema Watanzania tukajua mapema kuwa chama cha Mapinduzi wanabadili mfumo mzima wa siasa nchini. Tunaondoka kwenye siasa za vyama vingi, uliokuwa ukihubiri kwa maneno matupu, haki za binaadamu na haki ya kuwa huru kuchagua chama unachokipenda na kiongozi unaemtaka, sasa tunaelekea kwenye siasa za kumpenda “KIONGOZI MMOJA TU TENA LAZIMA AWE WA CCM”.

Haya yote yamekuja baada baada ya tafakuri kubwa iliyofanywa na vyombo vya usalama na  chama tawala na kugundua kuwa upinzani umepanda kasi vibaya Tanganyika. Zanzibar inaeleweka na bila kudhibitiwa mapema ccm itaondoka na Tanzania iko hatarini kufa. Sasa inapokuja katika kuulinda Muungano, kuuwa, kuteka au kubadili mfumo mzima wa kiutawala, ccm haitaki kufanya makosa. Sisi hatuna tofauti na nchi yoyote ya bara hili, ‘take your pick’ Zimbabwe, Uganda, Gambia, Rwanda, Burundi, Congo, Equtorial Guinea, Ethiopia, Egypt nk, vyama tawala vikiona viko hatarini basi Udikteta ndio solution{jawabu} sasa ni kuuwa, kuwekana mahabusu watu ovyo kwa kila mwenye kutaka mabadiliko au anae jaribu kufikiri tofauti.

Dalili za mvua hata siku moja haiwi jua kali mno. Sasa sijui wananchi mnataka dalili gani tena au ushahidi wa msukuma gani? Maana Wamakonde hatunao tena, ili mjuwe kuwa nchi hii sasa imejiunga rasmi na makoloni mengine ya waaafrika weusi. Nilisema zamani kuwa Zanzibar haiwezi kujitawala ikiwa Tanganyika upinzani hautokomaa. Sasa hilo limetokea na hatari hiyo imeonekana ndio maana wanafanya mageuzi haya. Vibaraka wa Zanzibar wao hawana tatizo, ndio maana Balozi Seif anajua na ameshatamka kuwa kuongezewa muda rais miaka saba hilo jambo linazungumzika na wanasingizia uchumi, kuwa tutaweza kubana matumizi ikiwa tutafanya uchaguzi kwa kipindi hicho. Hiyo sio sababu na wanajua, uchumi utaanguka na unaanguka kila sekunde, wala hauji juu tena kwa mfumo huu wa siasa tunaojitafutia.

Katiba ya Warioba ilikuwa dawa nzuri ya kupata suluhisho kwa taifa hili lakini ccm kama vilivyo vyama tawala vya Kiafrika waliikataa, juu ya kusimamiwa na kada wetu wenyewe. Tatizo kubwa kwa mtawala wetu ccm Tanganyika ilikuwa suala la Zanzibar kuwa serekali yake iliyo huru, kwani katiba ya serekali tatu ingelituweka pazuri kiuchumi, na hilo ni kosa kwa Tanganyika. Nani anakubali kirahisi kuligawa koloni lake kwa karatasi? Sasa hawa mnao waita ndugu zetu, mimi nina mashaka nao. Kweli nafahamu sio siku zote ndugu kutendeana wema, lakini ikiwa huyu ni ndugu, adui unamtafuta wa nini?

Nirudi kwa masheikh wa uamsho hawa sijawasahau wala Mola asinijaalie nikawasahau. Hawa waungwana wanateswa kwa sasa pia ni sehemu ya mpango huu wa ccm. Kwa sababu huwezi kuwaaachia waumini hawa huru halafu waje kukaa kimya au wakuachie ubadili katiba na kuimaliza Zanzibar, kwani kumezwa tayari. Kama mnakumbuka kesi waliyobambikiwa ni ya ugaidi, sasa nchi hii haina sheria kiasi hichi hadi kufika watu kuwekwa ndani miaka tunaelekea mitano sasa bila dhamana, hawajatiwa hatiani wala hawajafungwa, wako ndani muda wote huu kwa dhana peke yake?

Hii ni ‘injustice” ya pekee, dunia nzima inajua na wamekaa kimya, kwa kuwa ugaidi ndio sare ya msikitini siku hizi. Mola hachezewi na yeye pekee ndie anaewalinda waumini hawa. Kosa lao sote tunajua ni kuitetea Zanzibar na kutuamsha kutoka katika usingizi mrefu na mnono. Sasa hata ikiwa hilo ni kosa, nchi hii si ina sheria dhidi ya uhaini au ugaidi? Sijapata kuona uchunguzi wa miaka kama hii ulimwenguni, ama una kesi au huna. Yote hii ni mikakati ya  kufikia lengo kuu la kumtafuta rais wa milele wa Tanzania.

 

Nimetoa indhari tu, na huu ni wajibu wangu kama raia/mkaazi wa Zanzibar. Nina mawazo tofauti siku zote, na ni haki au wajibu wangu kutoa mawazo yasiopendeza baadhi, iwe siku zote au leo tu, muhimu kila mmoja aseme au atoe ya kwake aliyo nayo moyoni. Sio lazima tukubaliane leo au kesho, historia itatuhukumia kwa wakati wake, muhimu tusikae kimya, huo itakuwa ni udhaifu wa kutovitumia vichwa vyetu ipasavyo, kazi ya kichwa sio kuitunza akili peke yake, ITUMIE.

Zanzibar ni visiwa na nchi, hili hamtoweza kulibadili.

Sikupata muda wa masahihisho, naomba tahfif kwa hilo.

 

MOLA TUSTIRI.

Share: