Habari

Tanzania yatakiwa kutekeleza masharti ya Benki ya Dunia

Sources: VOA News Swahili na Mwananchi
Jumapili, Novemba 18, 2018

Benki ya Dunia (WB) Kanda ya Afrika, imesema kuwa serikali ya Tanzania imetakiwa kutekeleza masharti ya benki hiyo kabla haijapewa mkopo wa Dola 300 milioni za Marekani (Sh680.5 bilioni) kwa ajili ya kuboresha elimu nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumamosi, Novemba 17 Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Dk Hafez Ghanem alisema benki yake inatoa fedha kwa ajili ya wasichana wote bila kuwatenganisha kwa kigezo cha ujauzito .

Alisema kuwatenganisha kwa kigezo hicho ni kwenda kinyume na mkakati wa elimu jumuishi.

Gazeti la Mwananchi nchini Tanzania limemnukuu akisema: “Mradi wa Tanzania haujajadiliwa. Lakini kwa mazungumzo tuliyofanya, utajadiliwa baada ya serikali ya Tanzania itakapotimiza masharti tuliyokubaliana,” alisema Dk Ghanem.

Mkopo huo ilikuwa ujadiliwe na kuidhinishwa Oktoba 30, lakini kutokana na msimamo wa Serikali ya Tanzania kutotoa fursa ya kuendelea na masomo kwa wasichana wanaopata mimba, bodi ya benki hiyo ilisitisha kuujadili.

Kwa utaratibu wa benki hiyo, kabla mradi wowote haujaidhinishiwa fedha zinazohitajika, huujadili kwanza.

Baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Dar es Salaam, Rais John Magufuli alisema benki imekubali kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni, maabara, nyumba za walimu na vifaa vya kufundishia.

Awali chanzo ndani ya benki hiyo kiliiambia BBC Swahili kuwa sababu kuu mbili za zuio hilo zilikuwa – Mosi, uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuzuia wanafunzi wanaopata ujauzito kutokuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.

Pili, maboresho ya Sheria ya Takwimu yaliyopitishwa na Bunge la Tanzania Septemba 10 ambapo pamoja na mambo mengine, inakataza usambazaji wa takwimu zinazolenga kupinga, kupotosha au kukinzana na takwimu rasmi za serikali.

Kwa mujibu wa sheria hiyo kwa mtu atakayeivunja adhabu yake ni faini ya Dola 6,000 za Maerkani au kwenda jela miaka mitatu.

Aidha, Dk Ghanem alisema walizungumzia mabadiliko ya Sheria ya Takwimu na wameishauri serikali ya Tanzania kuhakikisha wadau wake wanakuwa huru kukusanya na kutumia takwimu, bila kuguswa na sheria hiyo.

Alisema WB haiwezi kufanyakazi bila takwimu ambazo zitakusanywa kwa uhuru, lakini masharti yaliyomo kwenye muswada, huenda yakazorotesha ufanisi wake.

Mabadiliko ya Muswada wa Takwimu yaliyofanyika mwaka huu na kuridhiwa na bunge, yanazuia mtu au taasisi yoyote kukusanya, kutafsiri au kutumia takwimu lazima zithibitishwe na Ofisi ya Takwimu Tanzania.

Siku ya Ijumaa, Novemba 16, Rais Magufuli alisema: “Fedha hizo hazijafyekelewa mbali kama baadhi ya watu “wasiotutakia mema wanavyosema.”

Rais Magufuli alinukuliwa akisema kuwa Dk Ghanem alikwenda Tanzania kuthibitisha kuwa Benki ya Dunia haitaiacha mkono nchi hiyo.

Share: