Habari

Tanzania/Zanzibar inalo la kujifunza kwa uchaguzi wa Kenya?.

Wafuasi wa upinzani (NASA) wamekusanyika katika barabara za kuelekea kwenye majengo ya Mahakama ya Rufaa ya Kenya, wakiwa na mabango kuhusu mitambo ya uchaguz kuwa ilidukuliwa kumsaidia Uhuru Kenyatta.

Mwandishi Maalum
Jumapili, Agosti 20, 2017

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) Ijumaa, Agosti 11 ilimtangaza Uhuru Kenyatta (55) kuwa mshindi katika uchaguzi wa Rais wa nchi hiyo uliofanyika Jumanne, Agosti 8 mwaka huu.

Wakenya wamemchagua tena Kenyatta kuwaongoza kwa muhula wa pili wa miaka mitano. Alichaguliwa kwa mara ya kwanza katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2013.

Kwa mujibu wa katiba, sheria na taratibu za uchaguzi za Kenya, Rais anatakiwa kuapishwa ndani ya siku 14 baada ya kutangazwa kuwa mshindi, endapo hakuna pingamizi la kisheria lililowasilishwa  mahakamani.

Lakini juzi Ijumaa, 18/8/2017 Muungano wa upinzani nchini Kenya, ‘National Super Alliance’ (NASA) uliwasilisha mahakamani kesi ya kupinga ushindi wa Uhuru Kenyatta.

Mawakili wa NASA, waliwasilisha nyaraka na stakabadhi 9,000 zilizokabidhiwa kwao kutoka kwa viongozi wa NASA katika kesi iliyofunguliwa Mahakama ya Rufaani mjini Nairobi, saa chache kabla ya muda uliyopangwa kumalizika.

Kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, ilihitajika kuwasilishwa mahakamani ndani ya wiki moja tangu kutangazwa rasmi kwa matokeo.

Mgombea urais wa NASA, Raila Odinga akiwa katika kampeni za uchaguzi pamoja na maelezo yake aliyotoa katika mdahalo mmoja, alisema kuwa hatopinga matokeo ya urais, endapo atashindwa.

Hata hivyo, alibadilisha uamuzi huo na kutangaza kwamba muungano wa NASA umefikia makubaliano kupinga mahakamani ushindi wa matokeo ya uchaguzi wa rais.

Odinga alisema kwamba, ingawa muungano huo ulikuwa umeapa kutokupeleka kesi Mahakama ya Rufaani, lakini waliamuawa kufanya hivyo kutokana na udukuzu wa kura wa computer, uliyolenga kumsaidia Kenyatta.

Odinga alisema: “Tumeamua kwenda kortini kufichua namna wizi wa computer ulivyofanikishwa. Hawa ni wataalamu wa computer. Computer ndiyo iliwataga, computer iliwaangua, computer ilitotoa vifaranga.”

Odinga alisema kuwa mitambo ya IEBC ilidukuliwa na matokeo kuvurugwa kwa maslahi ya Uhuru Kenyatta. Alisema kuwa kulikuwa na tofauti ya kura kiasi fulani kati yake na Kenyatta, wakati wa kutangazwa kwa matokeo.

Pia, Odinga aliitupia lawama tume ya uchaguzi akisema kwamba, ilikuwa ikitangaza matokeo ya uchaguzi bila kutumia ‘Fomu namba 34A na 34B’ ambazo huonyesha mpangilio wa matokeo kutoka kwenye vituo vya kupigia/kuhesabu kura.

Hata hivyo, Timu za kimataifa za waangalizi wa uchaguzi huo zilishauri upinzani, na wagombea wengine ambao hawakuwa wameridhishwa na matokeo ya uchaguzi, kufuata utaratibu uiliyowekwa kikatiba, kutafuta haki.

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na IEBC, Uhuru Kenyatta alipata kura 8,203,290 na mpinzani wake mkuu mgombea wa NASA, Raila Odinga alipata kura 6,762,224.

Kesi hiyo itasikilizwa na Majaji 7 wakiongozwa na Jaji Mkuu, David Maraga. Washtakiwa katika kesi hiyo ni Uhuru Kenyatta (Jubilee) na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC)). Mahakama ya Rufaani kuhusu kesi hiyo, uamuzi wake ni wa mwisho katika ngazi zote za kisheria.

Majaji wengine 6 watakaojumuika kusikiliza kesi hiyo, ni Jaji Mohamed Ibrahim, Profesa Jackton Ojwang, Dr Smokin Wanjala na Jaji Njoki Ndung’u ambaye amewahi kusikiliza kesi ya matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2013.

Majaji wengine ni Naibu Jaji Mkuu, Philomena Mwilu na Jaji Isaac Lenaola, ambao tayari wote wameshakula kiapo katika kusikiliza kesi hiyo. Inathibitishwa kuwa baada ya kiapo cha MAJAJI hao, ndipo utafuata uamuzi wa mahakama.

Msajili wa Mahakama ya Rufaani, Esther Nyaiyaki amenukulukiwa jana akisema: “Timu ya utetezi kutoka upande wa Rais Uhuru Kenyatta, wanapaswa kujibu mashtaka yote.”

Katiba ya Kenya inaeleza, iwapo Mahakama ya  Rufaani itaridhia ushindi uliyotangazwa na IEBC, Kenyatta ataapishwa kuongoza tena nchi hiyo ifikapo Septemba 12, siku 7 baada ya uamuzi wa mahakama.

Aidha, endapo Mahakama ya Rufaani, itakubali malalamiko ya upinzani na kubatilisha ushindi wa Kenyatta, itabidi kuitishwa kwa uchaguzi mpya kwa muda usiyozidi siku 60 tangu baada ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaani.

Iwapo upinzani utashinda kesi hiyo, uchaguzi mpya wa kumchagua Rais wa Kenya, utalazimika kufanyika Oktaba 31 au Novemba 1, mwaka huu.

Ratiba kamili: Agosti 18 ni siku ya mwisho ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya rais mahakamani. Agosti 20 ni siku ya mwisho ya kuwasilisha mahakamani ushahidi wote nyaraka/stakabadhi na kadhalika.

Ifikapo Agosti 24 ni siku ya mwisho kwa wanaohusika kujibu kesi kuwasilisha majibu. Na Septemba 1 ni siku ya mwisho kwa Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa kesi hiyo.

Taarifa zaidi zinasema kwamba, Jaji Maraga wakati alipokutana na wanasiasa wakubwa wa nchi hiyo (Uhuru na Raila), aliwahakikishia uwazi wa hukumu za kesi zote.

Raila Odinga, amenukuliwa kumsifu Jaji Maraga kwamba yuko kwenye mioyo ya Wakenya na amebeba heshima ya mhimili wa mahakama ya kutenda haki kwa imani ya Wakenya wote.

Narudia tena: Kwa mujibu wa sheria za Kenya, kupinga matokeo ya rais, mlalamikaji anatakiwa kuzishtaki pande mbili, ambazo kwa sasa ni Rais Kenyatta na Tume ya Ucaguzi (IEBC).

Katiba ya nchi hiyo inasema, kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi inatakiwa kufunguliwa siku saba baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi. Kwa mujibu wa Katiba, Mahakama ya Rufaani itasikiliza kesi hiyo ndani ya siku 14 tangu kufunguliwa.

JE, WATANZANIA/WAZANZIBAR KUNA CHA KUJIFUNZA KUTOKA KENYA:

Kuna msemo: “Sahau makosa yako, lakini jifunze kutokana na makosa yako.” Wamisonari wa Kilwa Kipatimu,  katika miaka 1960/70 walikuwa na msemo: “Mtenda haki hafikwi ni shari.”

Pamoja na kwamba madaraka na ulwa ni matamu na kila mtu anapenda kuwa katika ulwa na madaraka na hasa kwa viongozi wa nchi kupitia mfumo wa siasa wa vyama vingi.

Uchaguzi wa Kenya wa hivi karibuni, tumesikia ni kwa kiasi gani mamlaka za kusimamia uchaguzi huo zilivyofanya kazi yake kwa uhuru na uwazi. Hii ilitokana na makosa ya chaguzi zake za miaka ya nyuma zilizosababisha vurugu na mauaji ya raia wa Kenya.

Kenya kabla ya kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), mfumo wake wa uchaguzi kwa kiasi fulani ulikuwa unafanana na wa Tanzania, mfumo uliyojizatiti kutokubali kushindwa kwa CCM chama tawala/chama dola.

Sheria za uchaguzi za Tanzania, mfumo wa kuendesha uchaguzi, kuanzia kujiandikisha, utaratibu wa kupiga kura, kuhesabu kura na kutoa matokeo ya kura kwa nafasi zote lakini, hasa kura za rais, ni utata mtupu, ni kifo.

Utaratibu hauko wazi, bado ni giza tena giza nene. Uchaguzi wote unakuwa katika mzingira magumu na unatawaliwa na hali tete.

Baada ya uchaguzi wa Kenya kumalizika tumemsikia Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ametangazwa na IEBC, kuwa ameshinda katika uchaguzi mkuu wa Agosti 8. Kenyatta, aliwahi kunukuliwa kwamba akishindwa atakubali matokeo.

Lakini pia, Rais Kenyatta ameruhusu wanaopinga ushindi wake kuandamana na kuvitaka vikose vya ulinzi na usalama kutokuwabugudhi waandamaji na kuyalinda maandamano yao.

Rais Kenyatta, ameonesha kudhihirishia  dunia kuwa ni kiongozi wa Bara la Afrika mwenye upeo na ukomavu mkubwa wa kisiasa, demokrasia, mwenye kuthamini haki za binadamu pamoja na maamuzi ya raia katika utawala bora.

Tumesoma hapo juu uwazi wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC). Katiba na Sheria za Kenya kuhusu uchaguzi, inavyo ruhusu kupeleka mahakamani madai na malalamiko ya ngazi  zote, pamoja na urais.

Tanzania, matokeo ya kura za rais, KATIBA inazuia kuhojiwa mahakamani. Matokeo ya rais yamewekewa kinga ya kuto kuhojiwa popote, hata ikitokea kuna dosari na kasoro katika zoezi la kumchagua rais wa Muungano na wa Zanzibar.

Nadhani, Serikali ya Tanzania, inafaa kujitafakari kuhusu mfumo wake wa uchaguzi wa kisiasa kuungalia upya ili kuwapa matumaini wapiga kura wake kuchagua viongozi wanaowataka, kwa uwazi, bila hofu, bila vitisho.

Miaka zaidi ya 50 inatosha kujifunza na kuona yepi mazuri na yepi mabaya ndani ya nchi. Wakati wa kuufanyia mabadiliko na kuufumua mfumo mzima wa uchaguzi umewadia.

Serikali inafaa kujitathmini kutokana na chaguzi zake zilizopita. Niwakati wa kuwepo kwa tume ya uchaguzi, isiyofungamana kwa namna yoyoyte na mlengo wa kisiasa.

Maendeleo ya nchi yanakuja kutokana na siasa safi, uongozi bora na fikra za viongozi wa nchi kukubali mabadiliko kwa mujibu dunia inavyo badilika. Viongozi wafike mahala waache kukumbatia fikra mgando.

Kwa mfano kwa upande wa Zanzibar, kila kipindi cha uchaguzi ni shida. Kwa viongozi ni shida, kwa tume ya uchaguzi ni shida, kwa vikosi vya ulinzi na usalama ni shida kwa wananchi ni shida na kwa wageni wa kupita na wale wa kuishi ni shida.

Mfano, tukiuliza: Uchaguzi wa Zanzibar wa kila baada ya miaka mitano, uliyojaa adha na karaha, uliyojaa vituko na vioja, shida na visa vya wazi na vya siri. Uchaguzi wa aina hiyo hasa unawanufaisha nani na unawanufaisha vipi?.

Tangu kurejeshwa tena mfumo wa vyama vingi, tangu uchaguzi wa mwaka 1995 Zanzibar, wananchi wake hawanufaiki kutokana na uchaguzi. Kinyume chake wanavuna migogoro, kuwekeana visasi na chuki.

Ni aibu na fedhehe kwa Tume ya Uchaguzi, ambayo haijawahi hata mara moja kujikuta inasifiwa na wananchi, waangalizi wa uchaguzi na Jumuiya nyingiene za kimataifa, zaidi ya kukumbana na lawama, masimango na aibu.

Zanzibar kwa kupitia sanduku la kura imeshindikana kuwepo utulivu na  ustawi wa kisiasa kwa wananchi wake. Zanzibar, badala ya kupiga hatua za maendeleo mbele inazidi kurudi nyuma, siku baada ya siku.

Viongozi wa SMZ, wanapaswa ‘kutafuna jongoo kwa meno’, kuwapa utulivu wananchi kila kipindi cha kufanya uchaguzi. Ili hili liwezekane, kunahitajika kukinai kisiasa, kuaminiana miongoni mwa na viongozi na wananchi kuwa wote ni Wazanzibari.

Ubaya na utashi wa kisiasa uliyomjaa Rais wa sasa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein kuufuta mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), ambao ulionekana kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar, kuwa kitu kimoja.

Tukiuliza, katika hali ilivyo sasa, hivyo viongozi wa juu wanaraha gani katika hali ile inayokuwepo siku za uchaguzi, kuanzia uandikishaji wa wapiga kura, kipindi cha kampeni za uchaguzi, siku ya kupiga kura, siku ya kutangazwa kwa matokeo ya kura.

Kwa muda wa miezi 6 au zaidi watu ni roho mkononi, ‘hakuchi – kwacha’. Tunauliza hadi lini?. Hivyo, viongozi wa juu hasa Rais wa Zanzibar, ana raha gani, anajisikia vipi hali inapochafuka kwa chuki, kwa uonevu na ubaguzi dhidi ya wananchi, Rais wa SMZ, anapata raha gani, anapata faida gani?.

Dawa mjarabu itafutwe kuondoa siku za uchaguzi kuwa siku za kiwewe, hofu, wasiwasi na vitisho. Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ifumuliwe yote. Iundwe vingine, itengwe iwe mbali na wanasiasa.

Kadhalika, vikosi vya ulinzi na usalama visihusishwe hata kwa chembe ya tone moja kuwa sehemu ya kusimamia uchaguzi. Vitengwe mbali na mwingiliano na viongozi wa siasa na tume ya uchaguzi.

Kwa ufupi, Ikichunguzwa hasa, uchaguzi wa Zanzibar, unachangia sana kwa baadhi ya wananchi kupata maradhi ya ‘pressure’ na mengineyo. Matatizo ya uchaguzi wa Zanzibar, yapatiwe ufumbuzi yasiachwe kuwa donda ndugu.

Narudia tena: Kwa nini tatizo la uchaguzi linaachiwa kuendelea kila uchaguzi. Tujiulize, kwamba licha ya kuwanufaisha viongozi wachache wa juu waliyoko madarakani, lakini sidhani kuwa wananchi wa kawaida wananufaika na mfumo wa uchaguzi ulivyo sasa.

Tanzania wajifunze kutoka Kenya, kuona ni mambo gani ya msingi ambayo wanaweza wakajifunza katika kuendeleza demokrasia, utawala wa sheria na uwazi katika chaguzi zake.

Ushujaa wa kiongozi wa nchi ni kujiamini, kupendwa kwa dhati na wananchi, siyo kulazimisha kupendwa, siyo kutumia vitisho, siyo kutumia maneno ya dharau na kejeli. Huko ni kukosa hoja na maarifa ya kuongoza nchi..

 

 

Tagsslider
Share: