Habari

Tarehe ya Kura ya Maoni yaibua mapya

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema. Picha na Maktaba
Wednesday, October 22, 2014

Na Fidelis Butahe, Mwananchi

Dar es Salaam. Kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema kwamba kura ya maoni kupitisha Katiba Inayopendekezwa itafanyika Machi 30 mwakani, imeelezwa na wanaharakati, wasomi, wanasiasa na viongozi wa dini kuwa ni mwendelezo wa kauli zinazokinzana zinazotolewa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Juzi, Jaji Werema aliliambia gazeti hili kuwa, Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba itapigiwa kura za maoni Machi 30, mwakani kwa sharti kwamba: “Lazima Daftari la Kudumu la Wapigakura liboreshwe kwanza ili kuwapa fursa wapigakura wapya ambao hawamo kwenye daftari hilo.”

Alisema upigaji kura utatanguliwa na kampeni ambazo zitafanyika kwa siku 30, kuanzia mwanzoni mwa Machi ili kushawishi Katiba Inayopendekezwa iungwe mkono au kinyume chake kwa makundi yanayoipinga.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi yao wamekwenda mbali zaidi ya kuifananisha kauli hiyo na samaki aina ya kambale ambao wote huwa na ndevu na kwamba kila mmoja anataka aonekane ana kauli thabiti.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema elimu ya uraia inatakiwa kutolewa miezi mitatu hadi sita kabla ya kufanyika kwa Kura ya Maoni na siyo siku 30 alizozitaja Jaji Werema.

“Huwezi kutoa elimu ya uraia kwa siku 30, mfano Zimbabwe walitumia miezi sita kutoa elimu ya uraia. Mchakato huu umeingiliwa na wajanja, si riziki tena,” alisema.

Kibamba alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilieleza kuwa hadi Mei ndipo itakuwa imemaliza kazi ya kuboresha Daftari la Wapigakura na kwamba kitendo cha Jaji Werema kueleza kuwa Kura ya Maoni itafanyika Machi mwakani ni ishara ya ‘ukambale’.

“Waziri Mkuu alisema Katiba ipatikane kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015, Rais Jakaya Kikwete akakubaliana na TCD kuwa ni 2016, jana (juzi) Jaji Werema anatueleza kuwa ni Machi mwakani, tumsikilize nani?”

Alisema tarehe ya kura ya maoni kwa mujibu wa Sheria inatakiwa kutangazwa na Rais, si Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kusisitiza kuwa Serikali bora ni ile inayojiendesha kwa uwajibikaji wa pamoja.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema: “Serikali ya CCM imegawanyika, kila mtu ni kambale. Nakumbuka Rais Kikwete aliwahi kusema uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika Februari mwakani, lakini Waziri Mkuu akatangaza kuwa utafanyika Desemba mwaka huu.

“Nchi inayokuwa na viongozi ambao kila mmoja anatoa kauli yake haiwezi kuwa na mshikamano. Wao hawana umoja halafu wanataka Watanzania kuwa na umoja, hilo litawezekana kweli!” alisema Dk Slaa.

Aliongeza: “Hata kura ya maoni ikifanyika leo, haina maana tena kwa sababu Katiba Inayopendekezwa imeondolewa mambo ya msingi yaliyotokana na maoni ya wananchi. Wanasema Katiba hii ni bora barani Afrika, sijui nani kawadanganya.”

Dk Slaa alisisitiza kuwa ili hali iwe shwari, ni lazima kura ya maoni ifanyike wakati ambao NEC itakuwa imeliboresha daftari la wapigakura … “Watambue kuwa safari ya kudai Katiba Mpya ndiyo inaanza sasa kwa sababu Katiba Inayopendekezwa ni mali ya CCM, si Watanzania.”

Aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Dk Charles Kitima alilalamikia Serikali kwa kupuuza mawazo na malalamiko ya watu… “Katiba Inayopendekezwa ina uhalali wa kisheria lakini inakosa uhalali wa kisiasa. Kuokoa mvutano maridhiano ni jambo la msingi.”

Alisema kitendo cha Serikali inayoongozwa na CCM kupuuza malalamiko ya wananchi kuhusu mchakato wa Katiba si jambo la kuchekesha, linatakiwa kupatiwa ufumbuzi.

Alisema endapo Katiba hiyo itapitishwa, haitadumu muda mrefu kwa sababu watawala wengine watakaokabidhiwa kijiti wataibadili.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Hivi unafuata sheria au makubaliano? Sheria inasema Rais atatangaza kura ya maoni baada ya siku fulani, hivyo huwezi kufuta sheria hiyo eti kwa sababu kuna maridhiano.”

Aliongeza, “Rais asipozingatia makubaliano ya TCD hatakuwa na tatizo lolote kwa sababu makubaliano hayo hayakuwa sheria. Mazungumzo ya TCD hayawezi kukinzana na sheria iliyotungwa na Bunge.”

Kauli hiyo iliungwa mkono na Wakili na Mwandamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold Sungusia ambaye alisema: “Hawa viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa kuwa makini. Makubaliano siku zote hayawezi kuwa sheria. Makubaliano yao yangekuwa na maana kama na sheria ingebadilishwa.”

Alisema nchi inaongozwa kwa utawala wa sheria, kutoa mfano jinsi makubaliano mengi kati ya rais na vyama vya siasa yanavyoshindwa kutekelezeka kutokana na makubaliano hayo kukinzana na sheria zilizopo.

“Viongozi wa kisiasa wanatakiwa kutambua nchi inaongozwa kwa utawala wa kisheria. Wahakikishe makubaliano yao na Serikali yanakwenda sambamba na kubadilishwa kwa sheria,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severini Niwemugizi alisema: “Mchakato wa Katiba ni suala la kisheria na kisiasa. Kama Rais alikutana na wanasiasa na kukubaliana, ingekuwa jambo jema kama makubaliano hayo yangezingatiwa … Kwa sasa kuna mvutano mkali, sijui nini kitatokea.”

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka alisema: “Kama tunaamini kuwa Katiba Inayopendekezwa siyo nzuri, umefikia wakati wa kuwaachia wananchi wapige kura. Kama ni nzuri wataipitisha na kama hawaikubali wataikataa.”

Mbali na kusisitiza kuboreshwa kwa daftari la wapigakura kabla ya kura ya maoni, Sheikh Mataka alisema tatizo ni kwamba kikao kati ya Rais na TCD kilitawaliwa na mapendekezo zaidi na si makubaliano.

Katibu Mkuu Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Dk Leonard Mtaita alisema: “Kazi yetu ni kuwahamasisha wananchi kupiga kura utakapofikia wakati wa kupiga kura ya maoni… wananchi watapigia kura kile wanachokiamini kwa sababu wao ndiyo waliotoa maoni na wanajua kilichoendelea.”

Alisisitiza pia kuboreshwa kwa daftari la wapigakura na kusema nakala za Katiba Inayopendekezwa hazijasambazwa ipasavyo kama ilivyokuwa nakala za Rasimu ya pili ya Katiba akisema mpaka sasa CCT haina nakala yoyote ya Katiba hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz

Share: