Habari

Tatizo la umeme ni baharini na sio transfoma

Na Salma Said, Zanzibar

NAIBU waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Haji Makame Mwadini amesema kuwa tatizo la uhaba wa umeme katika baadhi ya maeneo linatokana na laini kubwa ya umeme iliyopo baharini na sio transfoma.

Katika suali lake la nyongeza Mwakilishi wa Jimbo la Bububu Hussein Ibrahim Makungu (CCM) alitaka kujua sababu zinazosababisha kuzorota kwa umeme ambapo katika jimbo lake kumekuwepo na usumbufu mkubwa wa wananchi kutokana na kukosekana huduma hiyo mara kwa mara.

Akijibu suali la nyongeza la Naibu waziri huyo alisema kwamba laini hiyo ya umeme iliyopo baharini ina uwezo wa kuchukuwa umeme megawati 45 ambazo hazitoshelezi kwa umeme wa Zanzibar.

Hata hivyo alisema kuwa tatizo hilo litaweza kuondoka muda mfupi kuanzia sasa mara baada ya kukamilika kwa ulazaji wa laini mpya ya umeme ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukuwa umeme megawati 100.

Aidha Mwakilishi wa jimbo la Wawi, Nassor Saleh Juma (CUF) alitaka kujua ni lini Serikali itawapunguzia wananchi gharama za uungaji wa umeme ili wapate huduma hiyo na hatimae waende samabamba na utandawaji.

Akijibu suali hilo msingi alisema kuwa Serikali inaendelea na mpango wake wa kuwaungia umeme wananchi kwa njia ya mkopo ili kuwapunguzia mzigo wananchi wa kulipa gharama zote kwa pamoja.

Mwadini alisema kuwa Shirika la umeme linaendelea kujenga umeme wa mbali kwa wale wananchi wanaounda vikundi katika vijiji kwa gharama za Shirika na wananchi kulipia gharama ndogo ya kuungiwa umeme ndani ya nyumba zao.

Share: