Habari

Tibaijuka, Jussa na sheria mpya ya ubaguzi‏

Tibaijuka, Jussa na sheria mpya ya ubaguzi

Ahmed Rajab
WATANZANIA ni watu wa ajabu kwelikweli. Angalia namna wanavyomtukuza na wakati huohuo kumtweza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Sina dhamiri ya kumpa Nyerere cheo cha uungu. Alikuwa binadamu na kama tulivyo wana wa Adamu alikuwa na makosa yake; makubwa na madogodogo. Mengine hayawezi kusameheka, mengine hayawezi kusahaulika.

Hata hivyo, hadi sasa Taifa hili halijapata kiongozi mithili ya Kambarage. Mithili yake kwa namna alivyoweza kulidhibiti Taifa, kwa kipaji chake cha kufikiri, kwa ulimi wake, kwa nadhari yake, kwa busara zake, kwa haiba yake na hata kwa ujanja wake.

Simpambi bure. Miongoni mwa viongozi walioliendesha Taifa hili ni Nyerere pekee aliyekuwa na nyingi ya sifa za uongozi zinazohitajika. Waliomfuatia hawamfikii hata ukucha, seuze udole. Naweza kula amini kuwa hakuna hata mmojawao anayethubutu kujigamba kwamba ana uwezo wa kumpiku Kambarage. Si kwa hili si kwa lile.

Pamoja na kuwa kiongozi wa chama, wa watu na wa Taifa Nyerere alikuwa hali kadhalika kiongozi wa viongozi. Hivyo, si ajabu kwamba aliwaweza Watanzania.

Takriban kila siku utaisikia sauti ya Nyerere walau kwa muda wa sekunde kadhaa kutoka Redio Taifa ya TBC. Tepu zake zinachezwa kwa sababu moja tu: kwa sababu amekuwa kama moyo wa Taifa na matamshi yake yanachukuliwa na Watanzania wengi kuwa ni mwongozo au dira ya Taifa.

Ndiyo maana miaka 13 baada ya mwili wake kulazwa kaburini bado tunamsikia kila siku akiukaripia ukabila, udini na ulaji rushwa.

Kwa bahati mbaya, nadhani matamshi hayo yanawaingia Watanzania sikio moja na kutoka sikio jingine bila ya kuwatwanga na kuwafanya wayatafakari na kuyafuata.

Ndiyo maana mafisadi wanaendelea na ufisadi wao, walaji rushwa wanaendelea kula rushwa, na wahongaji mirungura wanaendelea vivyo hivyo na amali yao bukheri wa mustarehe. Wanaochochea ukabila na udini nao hali kadhalika wanaendelea na chokochoko zao.

Labda wenye kusikitisha zaidi ni hawa Watanzania wa karne hii ya 21 — hasa vijana — wenye mawazo ya ubaguzi wa kikabila. Wao wamekwishazoea kuyatoa mawazo hayo bila ya kuona haya au aibu kana kwamba jambo la kawaida.

Nilishtuka na kuhuzunishwa niliposoma maoni yaliyotolewa kwenye mablogi mbalimbali ya Watanzania yaliyokuwa yakiuponda msimamo aliouchukuwa wiki iliyopita Ismail Jussa Ladhu, mwakilishi wa Mji Mkongwe, katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Jussa aliongoza upinzani wa wajumbe wa Baraza hilo kutoka vyama vya CCM na CUF kupinga hatua iliyochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya kupeleka andiko lake makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, kudai mipaka ya eneo la kiuchumi la bahari ya Tanzania itanuliwe.

Ombi hilo liliwasilishwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka. Yeye alisema kwamba mpango wa Tanzania wa kuomba iongozewe maili 150 (kilometa 241.5) kutoka mwambao wake utaliwezesha Taifa kulifanyia utafiti zaidi eneo hilo kuhusu rasilmali zilizoko chini ya bahari kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi.

Wazanzibari wengi wanaamini kuwa lengo hasa la hatua hiyo ni kuziingiza kwa ghiliba maliasili za Zanzibar, hasa mafuta na gesi, katika orodha ya mambo ya Muungano. Ndipo mablogi ya Wabara yalipoanza kumuandama Jussa.

Bila ya shaka, wanaompinga Jussa wana haki ya kumpinga. Ndivyo demokrasia ilivyo. Lakini wampinge kwa hoja si kwa kuwa ana asili ya Kihindi. Mmoja aliandika kwamba angekuwa yeye rais angemrudisha ‘kwao’.

Lakini jama, ninauliza tena, hivyo ni dhambi mtu kuwa na asili ya Kihindi au ya Kiarabu? Uzalendo uko wapi? Haki na usawa wa uraia upo wapi? Au ndo tuseme unafuatwa ule usemi wa ‘Baniani mbaya kiatu chake dawa’? Yaani Baniani aonekane mbaya na abaguliwe ila pale anapokuwa wa maslahi kwa haohao wenye kumbagua?

Tuna wajibu na dhamana ya kukumbushana kwamba ubaguzi kama huu na chuki zake ndio uliopelekea mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994. Ajali ya ndege iliyomuua Rais Juvénal Habyarimana mwezi Aprili mwaka huo ilikuwa kichocheo tu.

Wanamgambo wa Interahamwe na wa Impuzamugambi ndio waliokuwa safu ya mbele kushika mapanga na kuwaua Watutsi lakini mbegu za chuki zilikuwa tayari zishamea katika nyoyo za Wahutu.

Halaiki ya watu waliuliwa Kenya baada ya kutangazwa kuwa Mwai Kibaki ndiye aliyeshinda uchaguzi wa urais wa mwaka 2007. Kwa vile Kibaki ni Mkikuyu na wengi wa wafuasi wa Raila Odinga, mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo, walikuwa Wajaluo na Wakalenjini watu wa makabila hayo mawili wakaanza kuwaingilia Wakikuyu na kuwashambulia.

Wakikuyu nao wakalipiza kisasi kwa kuwashambulia Wajaluo na Wakalenjini. Roho za watu wasiopungua 1,500 zilipotea bure, maelfu wakajeruhiwa na maelfu wakawa hawana makazi ya kuishi. Ingawa siasa zilikuwa kichocheo lakini mzizi wa fitina ulikuwa chuki za kikabila.

Lazima baadhi ya walioandika mitandaoni na magazetini kumshambulia Jussa kwa kutumia uhuru wake tena ndani ya chombo cha kisheria — Baraza la Wawakilishi — ama ni kizazi kipya au ni watu wasioijuwa historia yao.

Lau wangeidurusu historia ya mapambano ya uhuru wangekutana na michango ya wazalendo wasiokuwa na asili ya Kiafrika. Wangekumbana na majina ya Watanzania kama akina Amir Jamal (Mhindi), Derek Bryecson (Mzungu) na Alnoor Kassum (Mhindi) ambaye bado yu hai.

Hao ndio waliokuwa kwenye mstari wa mbele lakini walikuwepo wengi wengine kama wao wasio na asili ya Kiafrika waliokuwa na hisia za kizalendo zilizo sawa au pingine hata zaidi ya zile za Watanzania wengine. Sema tu hawakuwa na umaarufu wa kujulikana kitaifa.

Bado tunaikumbuka aibu iliyolivaa Taifa pale baadhi ya vigogo ndani ya chama cha CCM walivyoutumia ukabila kumuangusha waziri mkuu (mstaafu) Dakta Salim Ahmed Salim wakati wa kumtafuta mgombea urais kutoka chama hicho kwa uchaguzi wa mwaka 2005.

Waliompinga Salim walisema kwamba hafai kwa sababu ana asili ya Kiarabu. Matamshi hayo yalikuwa ya fedheha na ya kashfa tupu. Tena ni matamshi ya kinafiki.

Ni matamshi ya kinafiki kwa sababu mbili. Ya awali ni kuwa mtu yuleyule waliyesema hafai kuwa Rais kwa sababu zao za kijinga hawakumpinga alipolitumikia Taifa katika nyadhifa nyingine.

Pili, haohao waliokuwa wakimpinga Salim kwa ‘uarabu’ wake hii leo ndio wenye kumuenzi na kumuengaenga. Hao mahasimu wake wa mwaka 2005 ndio wanaomtaja kama kiongozi mwenye kustahika si kwa kingine ila kwa moyo wake wa kizalendo. Wakikutana naye wanathubutu kumpa shikamoo na kutabasamu naye huku wakiutafuta ushauri wake kuhusu masuala ya uongozi wa Taifa.

Mara tu baada ya kupatikana mgombea urais wa CCM kwa uchaguzi wa 2005 kwa ghafla mahasimu wa Salim wakamvua gamba la uarabu na wakamvisha joho la uzalendo. Ndio wao ambao sasa wanamtukuza kuwa ni mzalendo mwenye hekima na maarifa ya uongozi.

Baadhi ya wabaguzi wa Bara wana tabia ya kumhujumu kila Mzanzibari mwenye kuukosoa Muungano kwa fimbo ya ukabila. Husingiziwa kuwa ama anaupinga Muungano kwa sababu anataka usultani urudi au pawepo utawala wa Waarabu au kwa sababu mtu huyo ni Mwarabu (hata ikiwa si Mwarabu) au kama si Mwarabu basi ni mtumwa wa Waarabu.

Wabaguzi aina hiyo haiwaingii akilini kwamba kunaweza kuwepo uzalendo Wakizanzibari uliokiuka tofauti za kikabila au hata imani za kidini.

Katika Zanzibar ya leo wananchi wameshikamana kuzizika tofauti zao za kisiasa na za kikabila. Lakini bado ziko chokochoko za kikabila kwani vigogo vya Kizanzibari navyo si vidogo katika mambo haya. Wengi wao wamo kwenye CCM na wanaupalilia ukabila kwa maslahi yao ya kibinafsi.

Ithibati ya haya tuliishuhudia wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea wa CCM katika uchaguzi mdogo wa kumchagua mwakilishi wa jimbo la Uzini huko Unguja. Mara baada ya kujitokeza mfanyabiashara maarufu Mohamed Raza Dharamsi akitaka awe mgombea wa CCM vikazuka vitimbakwiri vilivyompinga kwa sababu babu zake walikuwa Wahindi.

Tuna habari kuwa kigogo mmoja wa CCM ndiye aliyeuandika ule uitwao Waraka wa Wazee wa Uzini uliojaa chuki za kikabila na uliojaribu kumuangusha Raza.

Jengine lililopo Zanzibar ni madharau na matusi dhidi ya wenzetu wa Bara. Hizo pia ni hisia za kibaguzi.

Labda umefika wakati wa Tanzania kufikiria kuweka sheria itayoharamisha na kuwa ni kosa la jinai kutoa matamshi ya kikabila au kuwabagua watu kwa sababu za kikabila, za kidini au hata za kijinsia.

Inafaa tulitie maanani onyo la Nyerere kuhusu dhambi ya ukabila. Aliwahi kuonya kwamba Wabara wakishawamaliza Waunguja na Wapemba wataanza kulana wenyewe kwa wenyewe. Wataanza kusema ‘hawa Wachaga, hawa Wasukuma.’

Hatari kubwa iliyopo ni kuwa matamshi ya ubaguzi wa kikabila aghalabu hupaliliwa na baadhi ya viongozi kwa ajenda zao maalumu. Lakini viongozi hao wasisahau kwamba kiongozi anapopiga zumari la ukabila na wafuasi wake wakacheza yeye ndiye chanzo cha midenguo ya wachezaji.

Chanzo: Raia Mwema

Share: