Habari

TOBA

Mambo Yenye Kutuepusha na Uovu wa Maasiya

AlhamduliLlah Rabbil-Alamiin. Wassalatu Wa Salaam Ala Sayyidina Muhammad SAAW.
Ndugu zangu Waisilamu, Matatizo yote tuliyonayo sisi Waisilamu hayatakwisha, Ni lazima tukae tutafute suluhisho la matatizo. Suluhisho la kwanza kabisa ni Lazima kwanza turudi kwa Allah SWT. Tuombe toba, na tulete istighfaar, na tushikamane na hii dini inavyotakiwa. Kwani matatizo yote tunayo yaona hutokana na madhambi tunayo yatenda. (Dhahara alfasadi fil Barr wal Bahar bima kasabat Aidi Nnasi) Umeenea ufisadi na ukharibifu kaitka bara (ardhini) na baharini kwa sababu ya yale yanayochumwa na mikono ya watu. Haya matatizo hayatakwisha bila ya kuomba toba na kufanya istighfaar. Madhambi yetu ni mengi.
Ni wajibu wetu tujikumbushe kuhusu umma uliopita kwa nini uliangamizwa? Tulishawahi kujiuliza suala hili? Sababu ni nini umma huo uliangamizwa? Hebu kaa ufukirie ni nini kama si madhambi!! Jambo gani lilimfanya Baba yetu Adam atolewe Al Jannah? Jambo gani lilimfanya ibilisi atolewe katika Rehma ya Allah SWT? Jambo gani liliufanya Qaumu Aad waletewe na SWT kimbunga, upepo mkali uangamize wao na majumba yao? Jambo gani liliwafanya qaumu Thamud waletewe ukulele ambao uliwafanya kama vipande vya mitende vimelala katika ardhi? Jambo gani liliwaangamiza Firaun na Qaumu yake kwenye bahari, wote wakazama na kufilia mbali? Sababu ni moja tu. Allah SWT Anasema, wote Tumewaadhibu kwa sababu ya madhambi yao. Madhambi ndiyo yanayo sababisha watu waangamizwe Na Allah SWT Anajua kwa Hekima yake ni adhabu gani Awaletee kufuatana na hali zao zilivyo! Na sio kila umma ni adhabu aina moja. Ikiwa mtachunguza ulimwengu tunao ishi sasa na matatizo tuliyonayo ndugu zangu Waisilamu, yatosha kwa wenye akili waone kuwa hali tuliyo nayo leo, twaadhibiwa na Allah SWT. Na Adhabu hii haitaondoshwa hadi tutakapo tangaza toba na kurudi kwa Allah SWT.

Ni mambo gani yatayo tuepesha na maasiya?
Lazima ujiulize wewe ni mtenda dhambi yupi? Ili ibaki kwenye akili yako. Sababu utakuwa mmoja kati ya makundi mawili. Ama utakuwa mtenda dhambi na mwenye kufurahia, kuchekelea dhambi na kujisifu, ama utakuwa mtenda dhambi mwenye kuumia nafsi yake, akiudhika ndani ya nafsi yake akilia ndani ya moyo wake. Sasa wewe unajiweka katika kundi gani kati ya haya mawili?
1. Ione kila dhambi ni kubwa mbele ya Allah SWT. Usidharau udogo wa dhambi, bali uogope ukubwa wa yule unaemfanyia dhambi
2. Usipuzie dhambi ndogo. Kwani kokoto na kokoto hufanya jabali. Usingoje hadi dhambi zikawa nyingi ndio ukaanza kutubu. Tubu kwa ukweli kwa kila dhambi kubwa na ndogo.
3. Tahahadhari na kujitangaza unapofanya dhambi. SubhanAllah! Ndugu zangu tuko kwenye kipindi kigumu mno. Kila kwamba mtenda dhambi haoni raha mpaka ajitangaze. Kwani kuna watu hutaka awe mashuhuri hata ikiwa kwa kufanya dhambi. Mtume SAAW anasema Umma wangu wote ni wenye kesamehewa ila wale wenye kufanya mujahara! (yaani wenye kutangaza madhambi, wenye kujidhihirisha madhambi yao). Na Mtume SAAW anafafanua maana ya Mujahara kwa hadithi kwamba: miongoni mwa watu wenye kujidhihirisha ili watu wasije kudhani ni wale wenye kuzini barabarani tu, au wenye kulewa barabarani tu, kuwa ni wao ndio wenye kudhihirisha madhambi peke yao. Mtume SAAW Aeleza aina nyingine. Akisema ni mtu ambae ametenda dhambi usiku, kisha amelala Mwenyezi Mungu Amemsitiri, akaamka asubuhi akaanza kutangaza kuwaambia watu jana usiku nimefanya hivi na nimefanya vile (ikiwa ni matendo ya madhambi). Mtume SAAW asema huku ndio kufanya mujahara. Amelala Allah Amemsitiri, halafu alipoamka huondosha sitra ya Mweneyzi mungu. Hivyo watu wa aina hii hawana Msamaha wa Mwenyezi Mungu SWT.
4. Jambo jingine litakalo tuepusha na maasiya ni tauba sadiqah. Kurudi kwa Allah SWT. Kurudi kwenye asili yetu. Tumezaliwa wasafi bila madhambi. Tumeishi na tumetenda madhambi sasa turudi kweye asili yetu kwa kutubia. Na hawa wanaotubia kwa SWT ni watu wlio kuwa karibu mno na Allah SWT, na wanao mfurahisha Mwenyezi Mungu. Ni wajibu kujiuliza, mtu unangoja nini usirudi kwa Mola wako Allah SWT. Mtu anaishi katika ardhi ya Allah SWT, anakula katika riziki Yake, anapumua hewa Yake. na hizo neema mtu anafanyia maasi bila kujirudi!! Licha ya hayo Allah SWT Anakwita, ewe mja wangu njoo Kwangu nitakusamehe. Usijali madhambi yote uliyofanya Mimi nitakusamehe. Msamaha Wangu ni mwingi zaidi ya madhambi yako. Ndugu zangu, kuna fadhila zaidi ya hizo? Kuna Rehma zaidi ya hizi ndugu zangu Waislamu?
Siku moja Mtume SAAW alikuwa na Masahaba zake wakamshuhudia mama mmoja ambae amemkosa mtoto wake mdogo anae nyonya ambae anaekimbia kimbia hivi. Mama alikuwa kama aliepungukiwa kwa khofu na nywele zake zimefumuka akienda mbio huku na kule mashariki na magharibi akimtafuta mwanae bila ya kumuona, Na sisi tunajua vipi mama anavyokuwa akimkosa mwanae aliepotea. Mama yule baadae alimpata mwanae. Hakujiamini, alipom’beba na kumweka mikononi na kifuani, machozi yalimtoka kwa furaha. Mtume SAAW akawauliza masahaba zake, mwakiona kinachoendelea mbele yenu? Wakajibu ndio twaona!! Mtume SAAW Akawauliza masahaba, hivi mama huyu anaweza akamtia mtoto wake huyo katika moto? Wakajibu Ya RasuluLlaha, Haiwezekani! Kwa Rehma ya mama huyu na mapenzi ya mwanae haiwezikani akamtia motoni! Mtume SAAW akasema, Allah Arham bi ibadih min hadhil ummu bi waladiha. Yaani Allah Ana Rehma kwa waja wake zaidi ya mama huyu kwa mwanae. Allah hufurahi ikiwa mja hutubu kwa toba sadiqa. Hufurahi kuona mtu alie kuwa akimpiga vita na kumkataa kisha akatambua kuna Mola wa Haqi na akamkurubia kwa toba. Twangoja nini. Inna Allah Yuhibbu tawwabiin wa Yuhibuu Almutatahiriin.

Ndugu zangu Waislamu kuna Qisah hasasi na cha mafundisho.
Qisa hiki kimeelezwa na Sh. Saa’d al Buraqi. Anasema siku moja ya Ijumaa alikuja kijana aitwae Ahmed. Nae alikuja kumsimulia kisa kinacho mhusu rafiki yake nae anaitwa Ahmed. Asema Ahmed, “Kwanza Ya Sheikh, rafiki yangu Ahmed aliniambia nisikieleze qisa hiki ila kwa njia ya Mau’idha. Ili watu wachukuwe ibra na mazingatio, qabla hajaondoka ulimwenguni.” “Ahmed mwenye matukio ya qisa hiki alizaliwa huko Saudia, kwenye familia yenye uwezo. Alivaa alicho taka. Alikula alicho taka na alipanda alichotaka. Kama vijana wengine alioa na akawa ni kijana mwenye dini, alijishughulisha na darsa za dini, da’wa na kadhalika. Lakini siku zote marafiki wabaya ni wenye kuleta uovu. Wakaanza kumfuata na kumshawishi. Wakimwambia, ewe Ahmed wewe kila kitu unacho kwa nini tusisafiri kwenda nje? Tutapata kuona vile ulimwengu ulivyo. Lugha zile zile za sheitan mkubwa Iblis. Tembeeni kwenye ardhi ya Allah na kujifunza mambo. Wakamshawishi hadi wakafunga safari na kuelekea katika nchi ambayo haikuwa ya Kiislamu. Yenye kila aina ya fusqa na maasi na madhambi. Huko katika usiku mmoja wakamshawishi kuwa waende club. Wakimwambia yeye hutocheza wala kunywa basi akae tu awasubiri wao. Kijana huyo akawafuata. Akakaa. Lakini kama mnavyo jua. Mwanaume jinsi gani atakuwa kama simba lakini kwa mwanamke ni mtihani mkubwa sana. (Zuyyina linnasi hubbu shahawaa mina Annisai wal baniin walqanatiri mu qantarati mina dhahabi wal fedha wal khaili muswwamati wal an’ami walharth dhalika matau lhayati dunya), Ahmed akawa amezungukwa na wasichana wa kila aina wakawa wanamtongoza. Akawa anasubiri na kujaribu kujizuia na kujizua. Lakini alijikuta yuko na msichana faragha akizungumza nae, hadi akijikuta anafanya kitendo cha zinaa. Alisema Ahmed, baada kutenda zinaa, alimkumbuka Allah SWT. Bahati yake moyo wake ulikwa hayy. Akaanza kulia na akalia siku hiyo mpaka anakwenda Airport, Na huyo ahmed rafiki yake anasema mwenzie Ahmed alikuwa akilia kilo cha ajabu kama vile mtu amemkosa kipenzi chake. Na waLlahi!! Allah ni Kipenzi chake. Maana Imani BiLlah ndio Kipenzi cha kila Mu’min . Na Mtume SAAW anasema “Mwenye kuzini, Allah Humtoa imani yake kama vile mtu anavyo vua kanzu yake kupitia kichwani. Aliendelea kulia sana na saana. Akawaambia wale rafiki zake, kwamba Kesho InshAllah anawajibika awe katika mji wake kwao. Akarudi mnyonge ajabu. Na ndugu Waislamu mkumbuke kuwa Ahmed alikuwa na mke. Dhambi ile ilimkera ikamfanya aache marafiki. Ikamfanya aihame nyumba yake, ikawa nyumba yake ni msikitini akisoma Qur’an na kusali. Dhambi ile ilimfanya kijana Ahmed afunge saum siku moja na ale siku moja. Alikwenda Umra na wenzake wengine na alikuwa ni mwenye majuto sana hata wenzie wale ilikuwa wakimwita husema “nyie endeleeni nisije nikawaharibia Umra yenu maana mimi ni mchafu na nyie ni wasafi”. Walipomaliza Umra walirejea nyumbai laikini bado hali yake ilikuwa ni ile ile. Hana raha akilia tu usiku na mchana sababu ya ile dhambi aliyo ifanya. Akaamua kufanya kafara. Akamshauri ndugu yake ampeleke mahkamani ili apate hukmu ya sharia, amabyo ni kupigwa mawe hadi afe. Ndugu yake akamsihi asiende akimwambia yatosha toba yako kwa Allah SWT. Ahmed alisema. “La mimi nitakwenda kwani nitakutana vipi na Allah hali yakuwa ni memuasi kiasi kikubwa kama hiki, kuzini na mimi ni mtu nilieoa na nina mke? Mimi nimezaliwia katika nchi takatifu, nimechafua nafsi yangu, Kalla nitakwenda”. Hapo ndugu yake alimkubalia lakini kwa sharti, kwanza wakamuulize sheikh, fatwa ya qadhia hii. Sheikh akikwambia nenda basi mimi nitakupeleka. Wakaenda kwa mmoja wa mkubwa wa ulamaa. Ndugu yake akamuleza shekh kwamba Ahmed alifanya kadha wa kadha na katubia lakini bado hajiamini na anataka hukumu ya sharia. Nae ana watoto wawili hivi akapigwe mawe hadi afe! Shekh akamwambia usidhirishe familia yako. Inatosha toba yako ikiwa ni ya kweli basi Allah atakusamehe dhambi zako. Ahmed akasema kwa sauti ya juu, “Ya Sheikh nataka unipe dalili kwani Siku Ya Qiyama Allah atapo nisimamisha mbele nitakushika KOO lako”. Sheikh akasema “naam unishike koo langu lakini dalili nitakupa”. Akasema Sheikh, “Allah SWT Anasema, “

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْ ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا﴿٦٨﴾
Na wale wasio muomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini – na atakaye fanya hayo atapata madhara, (68
يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾

Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka. (69

Kijana alipoanza kusika aya zile basi aliona kama Sheikh anamtia kisu au khanjar katika moyo wake. Kijana akabadilika rangi ma kuingiwa ganzi yenye maumivu na kulia kwa uchungu.
Lakini Kwa Allah kuna Faraja. Ambazo ndio zilimzomtuliza. Sheikh aliendelea kusoma:

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُوْلَئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. (70)

Kijana Ahmed aliruka na kumkumbatia Sheikh kwa machozi ya faraja kwani sio tu kusamehewa bali dhambi zake kugeuzwa hasanat. Ahmed aliondoka pale na hamu yakufanya ibada zaidi na kuendelea na istighafaar.
Alikuwa amekaa msikitini siku moja ya Akhamisi akiwa na saumu. Imamu wa msikiti alichelewa. Ikabidi yeye Ahmed kusalisha na baada ya kusoma Alhamdu alisoma aya hizo na alilia na kuuliza msikiti mzima. Ahmed alibaki humo msikitini kwa muda mrefu. Baba yake ahmed alimtuma ndugu yake akamwiite, Nduguye alipofika msikitini alimuita Ahmed kwa mara kadha lakini hakuiitikia. Basi alirudi na kumuarifu baba yake. Nae baba yake alikimbilia kumuona Ahmed. Alimkuta Ahmed ameegemea nguzo, basi alimkaribia na akamsikia akisoma kwa sauti iliyotokeza kwa mbali, aya hizo:

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّهِ إِلَهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْ ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا﴿٦٨﴾
يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾
إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُوْلَئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

Baba yake alimuita kwa jina. “Ya Ahmed twende nyumbani, na alikariri kumuita lakini hizo ndizo Ayaat alizosoma kwa mra ya mwisho katika uhai wake. Ikawa Ahmed amefariki msikitini.

Sasa ndugu zangu Waisilamu sisi tunangoja nini. Lini tutabadilsha. Huyo ni Ahmed alietubia. Anagalia dhambi moja ilivyomshughulisa nafsi na maisha yake. Alijua kuwa amekosea. Na si vibaya kukosea lakini ni vibaya kutototubia.
Tizama Husni Al kahtim hiyo. Wewe unangoja nini? Usipime kiwango kwamba nikifikisha umri Fulani ndio nitatubu, au mpaka nikioa au hadi nikifanya kadha wa kadha. Laa! Huna uhakika kama mipango yako hiyo itafika au wewe utafika wakati huo qabla ya mauti hayajakukuta. Na fahamu kuwa siku ya Qiyama hakutakuwa na mali wala mtu wa kukusaidia.

Allah SWT Anasema:
فَإِذَا جَاءتِ الصَّاخَّةُ ﴿٣٣﴾ Basi utakapo kuja ukelele, (33)
يَوْمَ يَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِيهِ ﴿٣٤﴾ Siku ambayo mtu atamkimbia nduguye, (34)
وَأُمِّهِ وَأَبِيهِ ﴿٣٥﴾ Na mamaye na babaye, (35)
وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِيهِ ﴿٣٦﴾ Na mkewe na wanawe – (36)
لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ ﴿٣٧﴾ Kila mtu miongoni mwao siku hiyo atakuwa na lake la kumtosha. (37)

Namuomba Allah Atughufirie Madhambi yetu.

Ewe Mola wetu tujaalie tuwe miongoni mwa wale wenye kusikia mawaidha kisha wakayafuata vyema, Ya Rabbal Alamiin.
Ya Rabbi tujaalie a’mali zetu ziwe khalisan mbele yako ya Kariim.
Ya Rabbi Naomba Utuharamishie nyuso zetu na Moto wa Jahannam
Ya Rabbi Tutakase katika nyumba zetu mbali na kila haramu
Ya Rabbi Utepushie kila waliokuwa wabaya na uhasidi katika jamii yetu na Tujengee mapenzi miongoni mwetu.
Ya Rabbi tughufirie kila madhambi yetu na Utuelekeze ktk Siratal Mustaqiim, Ya ghaffaar Ya Rahiim.
Na Kwa Rehma Zenu Mtuingize Jannat Nnaiim, Ya Rahman Ya Rahiim. Amiin
WasalaLlahu ala Sayyidina Muhammadin wa ala Alihi wa As’habihi ajmaiin.

Share: